Kamati maalum yakutokomeza kipindupindu Zanzibar yakutana kupanga mikakati

Mkurugenzi Tiba na Elimu ya Afya Dkt. Fadhil Mohd Abdalla alieleza hayo alipokuwa akizungumza katika mkutano wa siku mbili uliozishirikisha taasisi za Serikali na taasisi za kiraia katika ukumbi wa uzazi salama Kidongochekundu.
Alisema Wizara ya Afya imeamua kuunganisha sekta mbali mbali za
Serikali, za kirai na washirika wa maendeleo wakielewa kuwa kipindupindu
hakiwezi kumalizika kwa nguvu za Wizara peke yake.
Aliwataka wajumbe wa mkutano huo kila mmoja kwa nafasi ya taasisi
anayotoka kuandaa mpango mkakati utakaosaidia kumaliza kabisa
kipindupindu Zanzibar ifikapo mwaka 2027.
Alisema Wizara ya Afya inafahamu uzito uliopo wa kufanikisha mpango
huo ikiwemo miundombinu isiyoridhisha ya kupatikana maji safi na salama,
ujenzi holela katika baadhi ya mitaa na jamii kutokuwa tayari kubadili
tabia.
“Jamii kukubali kubadili tabia ili kwenda sambamba na mpango huu nina
imani malengo ya kumaliza cholera yanaweza kufikiwa,” alithibitisha
Mkurugenzi Tiba.
Dkt. Fadhil alikumbusha kwamba Wizara bado inaendeleza masharti ya
afya katika kufanya biashara za vyakula na biashara za vinywaji ambayo
ni moja ya vyanzo vikubwa vya kuibuka kipindupindu.
Akizungumza katika mkutano huo Mwakilishi wa WHO Zanzibar Dkt.
Ghirmay Andermichael aliwakumbusha wananchi kufuata masharti ya afya
ikiwemo kutumia vyoo, maji yaliyochemshwa ama yaliyotibiwa na kunawa
mikono kabla na baada ya kula.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Dkt. Yahya
Hamad Shehe alisema katika kuchangia kumaliza cholera, Chuo kinaendeleza
mradi wa kupiga ramani mpya ya visiwa vya Zanzibar kwa kutumia ndege
maalumu ili kujua sehemu zinazopata maradhi hayo mara nyingi na sababu
zake.
Alisema ramani hiyo mpya itakusanya taarifa zote muhimu za Wilaya,
shehia na mitaa ili kupata urahisi wa kushughulikia tatizo hilo.



Picha na Makame Mshenga.
Post a Comment