Masheha Watakiwa Kutunza kumbukumbu za Matukio ndani ya Shehia zao Zanzibar
Masheha wa wilaya ya Magharibi “B” Unguja wametakiwa kutunza vyema
kumbukumbu za matukio za maafa katika shehia zao ili kuisaidia Serikali
kupata takwimu sahihi zinazohusiana na masuala ya maafa.
Afisa ufutiliaji na tathmini kutoka Kamisheni ya kukabiliana na Maafa
Mudrik Abdulla Mussa ameeleza hayo katika kikao maalum cha kuwapatia
mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi hao kilichofanyika katika Afisi za
Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.
Aidha, Afisa Mudrik amesema serikali inahitaji takwimu sahihi
zinazohusiana na masuala ya maafa kwani takwimu hizo zitaiwezesha
serikali kuboresha mipango ya kukabiliana na Maafa sambamba na kufahamu
athari zake kwa uchumi wa taifa. Pia amewataka viongozi wa shehia
kuharakisha na kukamilisha uundaji wa kamati za Maafa za Shehia ili
ziweze kufanya kazi za kukabiliana na Maafa katika Shehia kwa Ufanisi .
Akichangia katika mafunzo hayo sheha wa shehia ya kwa mchina Bi Zam
Zam Ali Rijali ameiomba Kamisheni ya maafa kuendeleza utaratibu wa
kuwapatia mafunzo hayo masheha na wananchi kwa ujumla pale
inapohitajika kutokana na suala la maafa kuwa linalomgusa kila
mwanajamii,
Sambamba na hayo Bi Zam Zam ameomba viongozi wa shehia kupatiwa vifaa
vya kukabiliana na maafa kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji
wa kazi zao.
Mara baada ya kufikishiwa maombi kutoka kwa viongozi hao wa shehia,
Mkurugenzi Mtendaji wa kamisheni ya Maafa Shaaban Seif Mohamed
amewaagiza Maafisa na watendaji wake kusambaza kwa haraka baadhi ya
vifaa hivyo ikiwemo fomu za kutosha za kutunzia kumbukumbu kwa kila
shehia kwa kuanzia na wilaya ya Magharibi “B” ambapo viongozi wake
wameshapatiwa mafunzo.
Afisa: Mawasiliano Kamisheni ya Maafa Zanzibar
Post a Comment