Header Ads

TAMWA Zanzibar yatathimini njia bora za kutumika kuimarisha utoaji wa huduma za Afya ya uzazi salama Zanzibar



CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, TAMWA ZNZ kimefanya utafiti wa kutathmini mchango wa vyombo vya habari katika kuhamasisha masuala ya haki ya afya ya uzazi hapa visiwani Zanzibar.

Utafiti huo umekuja kufuatia utekelezaji wa mradi wa kuendeleza utetezi wa vyombo vya habari juu ya haki ya afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana wa mijini na vijijini, ambao umefanyika katika wilaya tatu za Zanziibar ikiwemo wilaya ya Magharibi “B”, wilaya ya Kati na wilaya ya Chake Chake, Pemba.

Jumla ya wasailiwa 102 walihojiwa kupitia madodoso mbali mbali ikiwemo dodoso la waandishi wa habari, dodoso la wanawake na wasichana, dodoso la wanaume na wavulana na dodoso la taasisi za serikali na taasisi binafsi.

Katika utafiti huo, kumeibuliwa changamoto mbalimbali ikiwemo uelewa mdogo wa masuala ya haki ya afya ya uzazi kwa jamii, kutokuwepo kwa usiri katika utoaji wa huduma hizo, mila silka na tamaduni za mzanzibari, masafa marefu ya kufuata huduma na lugha ambazo haziridhishi zinazotolewa na watoa huduma hizo

Aidha utafiti umeonesha kuwa asilimia 75 ya watu wote waliyohojiwa wamesema kuwa bado huduma za afya ya uzazi hazitoshelezi na hivyo kushauri kuongezwa kwa huduma hizo ili ziweze kusaidia kukuza na kuboresha afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana.

Vilevile asilimia 47.6 ya waandishi wa habari waliyohojiwa wameeleza kuwa hawana uelewa kabisa kuhusiana na masuala haya ya afya ya uzazi.

Kupitia utafiti huu, wasailiwa walitoa ushauri mbalimbali ikiwemo kuboresha upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi kupitia ubora wa vifaa, miundombinu imara ya huduma hizo, pamoja na wataalam bora wa kutoa huduma hizo. 

No comments