Header Ads

MAREKEBISHO YA SHERIA ZA HABARI YA YAENDANE NA MIKATABA YA KIMATIFA INAYOLINDA UHURU WA KUJIELEZA

Zanzibar: - Najjat Omar.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar – TAMWA -Z kimekutana na wadau wa masuala ya kurekebisha sheria mbalimbali wakiwemo Tume ya Kurekebisha sheria, Tume ya Utangazaji,wawakilishi kutoka Wizara ya Habari pamoja na waandishi wa Habari katika kujadili na kuendelea kuzungumza juu ya uwepo wa mikataba ya kimataifa inayolinda na kusimamia masuala ya uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza.

Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa habari Tanzania TAMWA-ZNZ, Dkt Mzuri Issa amesema Zanzibar imesaini mikataba kadhaa inayozungumzia uhuru wa vyombo vya Habari na masuala ya uhuru wa kujieleza hivyo kuwepo wa masahihisho ya sheria ya habari ni kuendana na mikataba ya kimataifa ambavyo kama nchi tumeingia nayo makubaliano.

Dk Mzuri amesema hayo katika mkutano wa kujadili mapungufu ya sheria zinazokwamisha uhuru wa habari Zanzibar uliofanyika Ofisi za TAMWA Tunguu Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, amesema “Kwa Pamoja tunahaja ya kuendelea kukumbusha suala la kurekebishwa kwa sheria zenye mapungufu kwenye masuala ya habari ili mabadiliko yatokee”Amesema Dkt Mzuri wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.

Dkt Mzuri amesema pamoja na kuridhia Mikataba ya Kimataifa na Kikanda bado Tanzania sauti za wananchi hazipewi kipaombele kusikika katika vyombo vya habari ukilinganisha na sauti za viongozi jambo ambalo linawanyima wananchi haki yao ya kikatiba ya kutoa maoni yao.

Miongoni mwa mikataba ambayo imesaini ni Pamoja na Tamko la Kimataifa la haki za binadamu (Universal Diclaration) na mkataba wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCR) ambayo Tanzania ni moja ya nchi iliyoridhia mikataba hiyo, ambapo nchi 172 zimeridhia mkataba wa haki za kiraia na kisiasa.

Mkataba mwengine ni mkataba wa  Bara la Afrika unaojuilikana kama mkataba wa haki za binadamu na haki za watu wa Umoja wa Afrika, uliopitishwa mwaka 1981 (Afrika Charter on Human  Peoples Right) ulianza kutumika (1986) na  mkataba huo hadi kufikia mwaka (2002) tayari ulisainiwa na 153 za Afrika.    

Zaina Abdallah Mzee ni Afisa Mradi wa Uhuru wa Habari kutoka TAMWA- Z amesema sauti za wananchi zikipewe nafasi ya kutoa maoni ni moja ya uhuru ambao wananchi wanao wa kusema na kusikilizwa ili palipo na mapungufu yafanyiwe kazi na wahusika “Hizi sheria na mapungufu yake haziwagusi tu waandishi bali hata wananchi wanapata woga wa kuzungumziaa changamoto zinazpwabakili ” Amesema Zaina.

Hawra Shamte ambaye alikuwa ni muwasilishaji wa hoja katika kikao hicho amesema sheria zinazosimamia sekta ya habari bado zinaonekana kiuhalisia hazifanyi kazi ipasavyo kwa kulinda usalama wa waandishi wa habari na wananchi hivyo zinahitaji kufanyiwa marekebisho.

“Mikataba mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa inalinda tasnia ya habari, waandishi wahabari na watetezi wa haki za binadamu na kulinda wajibu wa Serikali hivyo wananchi wanahaki ya kutoa maoni yao “Amesema Hawra Shamte alipokuwa anawasilisha.

Sheria ambazo zinahitaji mabadiliko ni Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu no 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria no 8 ya mwaka 1997 na Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar no 7 (1997) iliyofanyiwa marekebisho na sheria no 1 (2010).

Mwanasheria kutoka Tume ya kurekebisha Sheria Zanzibar Sabra Mahmoud Iddi amesema wanategemea mchakato wa Sheria ya habari utafanyiwa marekebisho ili kupata sheria bora zinazozingatia maslahi ya waandishi na uhuru wa vyombo vya habari.

“Mchakato wa marekebisho ya sheria unaendelea hili ni jambo la muda mrefu linalopitia ngazi hadi ngazi ili kupata sheria bora, hivyo amewaomba waandishi pamoja na wananchi kuwa na subra kwa lengo la kupata sheria bora zinazokwenda na wakati” Amesema Sabra wakati akitoa maoni kwenye mkutano huo.

Salim Said Salim ni mwandishi mkongwe Visiwani Zanzibar amesema waandishi wanakutana na vikwazo mbalimbali wanapotekeleza majukumu yao “Wakati mwengine hata vyombo vya habari hufikia hatua ya kufungiwa na kutokuendelea na kazi zao za utangazaji.”Amesema Salim.

No comments