MAJENGO NA MATAWI YA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) YATAKIWA KUENDANA NA KASI YA CHAMA HICHO KWA KUJENGA MAJENGO YA KISASA
PEMBA
MAKAMU
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Zanzibar Mhe: Dk Ali Mohamed, amesema
lazima majengo na matawi mengine ya chama hicho, yaendane na kasi ya chama kwa
kujenga majengo ya kisasa.
Alisema wakati wa ASP na TANU, wanchama na viongozi wa vyama hivyo,
walijitahidi kujenga majengo, ambayo kwa sasa yamerithiwa na CCM, hivyo lazima
kuwe na majengo yanayofanana na wakati uliopo.
Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, alieleza hayo kwenye tawi la CCM la Pandani Jimbo
la Mgogoni, kabla ya kuweka jiwe la msingi la tawi hilo, ikiwa ni sehemu ya
ziara yake ya kuangali utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 kisiwani
Pemba.
Alisema, huu ni wakati wa CCM, hivyo majengo yaliorithiwa kutokwa
kwa ASP kwa Zanzibar na TANU kwa Tanzania bara kama hayaendani na kasi, ni
vyema yakajengwa mengine ili yafanane na wakati na hadhi iliopo.
Alieleza kuwa, ujenzi wa tawi hilo jipya uliofanywa na
wanaccm wenyewe na wahisani wao wengine, unafaa kuungwa mkono na kila mmoja,
maana wajenzi wa matawi hayo ni wanaccm wenyewe, kama walivyofanywa waasisi wa
TANU na ASP kwa wakati wao.
“Wana wa ASP na TANU, walijenga matawi ya chama kwa njia ya
kuchangishana, na leo hii tumeyarithi tukiwa na CCM, hivyo lazima na sisi
tuliopo ndani ya CCM, tujenge majengo ya kisasa, ili yafanane na hadhi na
ukubwa wa chama chetu”,alieleza.
Katika hatua nyengine, Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM
Zanzibar, amemshauri Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mberwa Hamad
Mberwa, kuhakikishga shilingi milioni 26, zinapatikana.
Alisema kwa vile taarifa ya ujenzi inaonyesha bado shilingi
milioni 36 ili kukamilisha ujenzi huo hadi kuhamia, yeye atawasilisha shilingi
milioni 10, na fedha nyengine zilizobakia lazima uongozi wa mkoa uzipate.
Alifahamisha kuwa, kwa upande wa Mwakilishi wa Jimbo la
Mgogoni Shehe Hamad Matari, ameshajitahidi kuchangia asilimia 75 ya gharama
zilizofikiwa, hivyo ni vyema na uongozi wa Mkoa huo, kuhakikisha unazipata
fedha nyengine.
“Mwenzetu Mwakilishi wa Jimbo hili la Mgogoni, ameshajitolea
na sasa na wewe Mwenyekiti wa CCM Mkoa lazima shilingi ,milioni 26, zitafuteni
na zangu shilingi milioni 10 zipo, wakati wowote hata leo”,alieleza.
Wakati huo huo Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Mhe: Dk Ali Mohamed Shein mara baada ya uzinduzi wa jengo la jipya
la skuli la madarasa manne ya Mgogoni, aliwataka wanafunzi kuacha ucheza na
kusoma.
Alisema, kazi iliopo mbele yao kwa sasa, ni kusoma na sio
nyengine yoyote, kwani elimu ndio msingi mzuri wa maisha yao ya baadae.
Aidha aliendelea na kauli yake, ya kuwataka waalimu kuingia
madarasani na kuwasomesha wanafunzi hao, na kuweka kando siasa zao wanapokuwa
madarasani.
“Tumeshawawekea mazingira mazuri ya kusomesha kwa ufunguzi wa
jengo jipya, sasa acheni siasa ingieni madarasani kwa wakati ili kuwapa vijana
elimu”,alifafanua.
Hata hivyo, aliendelea na msimamo wake wa kumtaka Mkuu wa
Mkoa kufanya ziara za mara kwa mara kwenye skuli mbali mbali, na iwapo
watawabaini waalimu watoro awasiliane na Waziri husika, kwa hatua.
Akiwa kwenye ukaguzi wa ununuzi wa karafuu kwenye kituo cha
ZSTC Bandarini Wete, Rais huyo wa Zanzibar Mhe: Dk Ali Mohamed Shein, ameutaka
uongozi wa ZSTC, kuhakikisha karafuu zilizokamatwa kutoka Mkoani Tanga,
hazichanganywi na karafuu za Zanzibar.
Aidha aliutaka uongozi wa Mkoa wa kaskazini Pemba, kufauta
taratibu za kisheria katika kukiteketeza chombo aina ya jahazi kilichokamatwa
hivi karibuni na karafuu zilizodaiwa kutaka kusafirishwa kimagendo.
“Angalieni sheria zinasemaje na taratibu zinavayoelekeza,
kwanza kwa hizi karafuu zilizokamatwa zikiingizwa kimagendo Pemba, lakini hata
kwa hicho chombo kilichokamatwa na karafuu kavu gunia 14 za
magendo”,alifafanua.
Kwa upande wakew Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibra
Mhe: Riziki Pembe Juma, alisema anajiskia faraja kuona rais huyo, anazindua majengo
mapya ya skuli, ambapo hiyo ni ishara ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka
2015/2020.
Mapema Mjumbe wa baraza la Mapinduzi na Waziri asiekuwa na
wizara Maalum Mhe: Said Soud Said, alisema ujenzi wa masoko na skuli ni
utekelezaji wa Ilani ya CCM, chama ambacho ndio kilichoshinda kwenye uchaguzi
mkuu.
“CCM ndio chama kilichoshinda na mimi na mwengine yoyote
lazima atekeleze Ilani yake, na asietaka akae pembeni, maana uchaguzi mwengine
hakuna hadi mwaka 2020”,alifafanua Mhe: Said Soud.
Nae Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo
Mhe: Bichumu Kombo Khamis, aliwataka
wanafunzi kuacha kuranda randa ovyo, na badala yake washughulikie masomo yao.
Rais huyo wa Zanzibar na Mwe nyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mhe: Dk Ali Mohamed Shein, ataendelea na ziara yake ya siku tano kisiwani
Pemba, kwa kumalizia Mkoa wa kusini Pemba, ambapo awali, atapokea taarifa ya
kikazi ya mkoa huo, ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Wawi.
Post a Comment