MABILIONI YAVUNWA BAADA YA SERIKALI KUKODISHA MASHAMBA YA MIKARAFUU PEMBA.
PEMBA.
ZAIDI ya shilingi bilioni 14.80
zimepatikana, baada ya serikali kukodisha mashamba yake ya mikarafuu, kwenye
wilaya za Wete na Mkoani kisiwani Pemba, kwenye zoezi lililoanza mwezi Julai,
mwaka huu kisiwani humo.
Awali serikali
ilijiwekea lengo la kukusanya shilingi milioni 200 kwenye zoezi hilo kwa Unguja
na Pemba, ingawa kwa hatua za awali, lengo hilo limeshavuukwa na wilaya mbili
pekee kisiwani Pemba.
Imefahamika
kuwa, wilaya ya Mkoani pekee imeshaiingizia serikali shilingi milioni 760,
ingawa wilaya hiyo yenye mashamba zaidi ya 80 ya serikali, bado zoezi la
ukodishaji halijafungwa rasmi.
Mkuu wa
wilaya hiyo Hemed Suleiman Abdalla, alisema awali baada ya kupokea taarifa ya
makadirio ya serikali kwa msimu kwamba wanatarajia kukusanya shilingi million
200, alisema hizo anatarajia kuzifikia kwenye wilaya yake pekee.
Alisema, kwa
sasa fedha hizo ndani ya wilaya yake pekee, ameshapindukia mara tatu na baadhi
ya wilaya kama za Chakechake, Micheweni na Wete zoezi rasmi halijakamilika.
“Mimi
nilipopokea taarifa za kwamba, serikali inakusudia kukusanya shilingi milioni
200 kwenye msimuu huu kupitia ukodishaji wa mashamba yake, nilitoa taarifa
kwamba kiwango hicho cha fedha anakitarajia kwenye wilaya yake
pekee”,alifafanua.
Aidha
taarifa zinaeleza kuwa, wilaya ya Wete ambako nako zoezi rasmi halijakamilika,
tayari jumla ya shilingi milioni 720 zilishapatikana, wakati wa zoezi la
ukodishaji wa mashamba ya mikarafuu ya serikali.
Kaimu Afisa
Mdhamini wa wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Said Juma alisema
zoezi hilo pamoja na kutarajiwa kuingiza fedha nyingi serikali, lakini pia
litagundua mashamba mengine ya serikali.
“Zoezi hili
linatarajiwa kuingiza fedha nyingi serikali, lakini twatarajia likikamilika na
hata mashamba yasio na idadi yatarudi serikalini”,alifafanua.
Mkuu wa
wilaya ya Chakechake Salama Mbarouk Khatib alisema, tayari jumla ya shilingi
zaidi ya milioni 85 zilishapatika kwa siku ya kwanza ya uzinduzi wa ukodishaji
kwenye wilaya yake.
Alisema
fedha hizo zilizopatikana zilijumuisha mashamba 15 kwa siku ya kwanza ya
uzinduzi wa zoezi hilo, lililofanyika mabonde ya Shemkani shehia ya Chonga
wilayani humo.
“Mimi
naamini kwa msimu huu na kwa utaratibu mzuri uliopo wa kisheria, basi mashamba
yaliokuwa mikononi mwa watu kiholela sasa yatarudi serikali na kuongeza
pato”,alifafanua.
Baadhi ya
wananchi hasa wanayoyatunza mashamba hayo, wameiomba serikali kuwasilikiza
kwanza, iwapo wanahati zinazokubalika kabla ya kutangaaza mnada wa hadhara.
Kombo
Abdalla Kombo wa Vitongoji alisema, jengine ambalo ni vyema serikali ikawapa
kipaumbele, ni kuacha kuwaunganisha na minada ya hadhara, kwani bei huwa kubwa
na kushindwa kuipata.
Kwa upande
wake Hamad Ussi, alisema ijapokuwa wengi wao wanayatumia mashamba hayo kutoka
kwa warithi wao, lakini vyema wakaelekezwa ili waendelee kuwa nayo kisheria.
Wakati zoezi
la ukodishaji wa mashamba ya mikarafuu ya serikali likiendelea, tayari zaidi ya
mashamba 580 yameshagundulika, ambayo mengi yao yalikuwa mikononi mwa wananchi
kinyume na tataribu, huku wilaya ya Mkoani ikigundua zaidi ya 80 pekee.
Post a Comment