Header Ads

WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI ZANZIBAR YATAKIWA KUPELEKA VIFAA VYA MAABARA KATIKA SKULI YA MSINGI NA SEKONDARI CHOKOCHO NDANI YA KIPINDI CHA MIEZI SITA.



Zanzibar                                                                 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, ametoa muda wa Miezi sita kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuhakikisha inapeleka vifaa vya maabara katika skuli ya Sekondari na Msingi Chokocho, ili wanafunzi wapate kujifunza kwa vitendo masomo yao ya Sayansi.
Dk Shein alisema ili wanafunzi waweze kusoma vizuri na kufahamu masomo ya sayansi, lazima maabara ya skuli hiyo iwekewe vifaa vya maabara, ili wanafunzi waweze kusoma kwa vitendo kwani haiwezekani kusomesha sayansi kwa nadharia.
Kauli hiyo alitoa mara baada ya kulifungua jengo la skuli hiyo ya Chokocho iliyopo Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba lililojengwa kwa nguvu za wananchi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kumalizia ujenzi wake ambapo miongoni mwa changamoto iliopo ni ukosefu wa vifaa vya maabara.
“Huwezi kusomesha wanafunzi wa masomo ya sayansi bila ya kuwemo kwa vifaa katika maabara, wanafunzi watasoma vipi masomo hayo, ili kuwa na wataalumu lazima masomo ya vitendo yawepo kwa kiasi kikubwa”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein aliwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Wakaguzi wa Wizara wa Elimu kuhakikisha wanapita katika skuli, kufuatia mahudhurio ya walimu na wakibaini kuwepo kwa mwalimu mtoro wamchukulia hatua za kisheria.
“Tunafuatilia wenyewe maana wasimamizi wanatuangusha na wale walimu ambao hawawajibiki watafukuzwa kazi kwa mujibu wa Sheria na taratibu zilizopo”,alisema Dk. Shein.
Alisema kuwa kuna baadhi ya walimu wamekuwa watoro, wengine huchukuwa likizo bila malipo na kufanya shuhuli zao huku bado wanachukua mishahara, jambo ambalo ni kosa na kupelekea uwepo wa wafanyakazi hewa hasa katika Wizara hiyo ya Elimu.
“Mwalimu yotote atakae bainika kutokuwajibika ipasavyo, mtoleeni taarifa ili achukuliwe hatua kali za kisheria, wapo walimu wengi wanataka ajira sasa wewe umeajiriwa hutekelezi wajibu wako”aliongeza Dk. Shein.
Hata hivyo, aliwataka wazee kuwashajihisha watoto wao kusoma, masomo ya sanyani, kushirikiana na walimu na kuwataka baadhi ya walimu wanaochanganya siasa na elimu kuachana na jambo hilo.
Aliwataka wanafunzi kutambua kuwa Chokocho, Michenzani, Kisiwa Panza itajengwa na wananchi wenyewe baada ya kupata elimu hiyo.
Waziri wa Elimu na Manzo ya Amali, Riziki Pembe Juma, alisema kuwa changamoto za vifaa vya sayansi bado zipo na kuahidi kuwa Wizara yake itazitatua pamoja na uhaba wa walimu.
Katibu mkuu wa Wizara hiyo Khadija Bakari, alisema jengo hilo lenye vyumba vinne na maabara, limejengwa kwa nguvu za wananchi viongozi wa serikali pamoja na Serikali ambapo limegharimu zaidi ya Milioni 96, nguvu za wananchi ni Milioni Milioni 21.
Akiwa katika Kituo cha KMKM, mara baada ya kukiweka jiwe la msingi, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kujenga vituo sita vya uokozi Unguja na Pemba, ili kujilinda na majanga yanayotokea baharini. 
Alisema matukio makubwa mawili yametokea, ikiwemo kuzama kwa meli ya MV Spice Islander na MV Skagit na kupoteza maisha ya watu, hali iliyopelekea kuundwa kwa sheria inayokataza uingizwaji wa meli Zanzibar iliyozidi miaka 15. 
"Meli zinazoingizwa nchini ziwe mpya au chini ya miaka 14, hata MV Maendeleo tumeizuwia baada ya kuona umri wake umekuwa mkubwa, bahari haina fundi wala mwenyewe na ndio maana serikali ikajenga vituo hivi vya uokozi Unguja na Pemba"alisema.
Aidha, aliwaeleza wananchi kuwa, vifaa vya kisasa vilivyowekwa katika kituo cha uokozi Nungwi, vitasaidia kutambua chombo chochote kitakachopata hitilafu kitaonekana moja kwa moja na kuwataka wananchi kukubali mafunzo ya ukozi yatakayotolewa na kikosi cha KMKM yakiwemo kuogolea, ili kuokoa maisha yao yanapotokea majanga.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalumu za Smz, Haji Omar Kheir alisema kituo cha KMKM Mkoani kitawekewa vifaa vya kisasa vya uokozi kama ilivyo vituo vya Unguja kwani tayari vifaa hivyo vimeshawasili.
Nae Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Radhia Rashid alisema kuwa kituo hicho ni miongoni mwa vituo sita vya uokozi vinavyojengwa Unguja na Pemba ambacho kimeanza ujenzi wake 2016 na kinatarajiwa kukamilika Disemba mwaka huu.
Alisema kuwa kitakapokamilika tu kitaanza kutoa huduma kwani tayari vifaa vyake vyote vipo huku akieleza kuwa tayari baadhi ya wananchi wakiwemo wavuvi wameshaanza kukitumia kituo cha uokozi cha Nungwi ambacho Dk. Shein alikiwekea jiwe la msingi tarehe 13 mwezi huu.
Akizungumza baada ya uwekaji wa jiwe la msingi, Tawi la CCM Milimuni Chokocho, DK. Shein amewataka wanaCCM kuendelea kukiimarisha chama chao na kuishi kwa kupendana, kuwa wamoja na washirikiane na sio watengenezeane majungu baina yao. 
Alisema katika Ilani ya CCM hakuna kitu fitna wala majungu, hivyo wanachama wanapaswa kuhakikisha wanashirikiana na kushikamana, kwa ajili ya maslahi ya CCM na kuhakikisha Serekali yao inarudi tena madarakani mnamo mwaka 2020.
Alifahamisha kuwa kazi kubwa ya chama, iko Matawini kwani ndiko kwenye wanachama wa CCM, hivyo aliwataka viongozi kutambua kuwa wana kazi kubwa ya kukiimarisha chama hicho kupitia Matawini, Wadi hadi kwenye Jimbo.
Hata hivyo, DK. Shein aliahidi kuchangia Milioni 10, kwenye jengo hilo ambalo kwa sasa limeshagharimu TZS milioni 20  na zimebaki TZS milioni 16 na makadirio ni kugharimu TZS milioni 36 hadi kukamilika kwake ambapo viongozi wa chama hicho na Serikali walichangia hapo hapo zaidi ya TZS milioni 7. 
Mapema asubihi Dk. Shein akipokea taarifa ya utekelezaji kwa Mkoa wa Kusini Pemba, aliwataka mawaziri wa wizara zote za Serikali na taasisi zake, kukaa vikao na kujitathmini Juu ya utendaji wao wa shuhuli zao, baaada ya kumaliza ziara yake.
Alisema baada ya kufanya hivyo watajuwa wapi taasisi zao hazikuweza kufikia malengo, kutokana na mipango kazi walioipanga ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwanajuma Majid Abdalla akitoa taarifa ya Mkoa huo alisema Mkoa wake bado Ukoa salama na umeweza kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa kiasi kikubwa. Dk. Shein pia, alizindua uchumaji wa karafuu huko  Mgagadu.

No comments