Header Ads

DC AKERWA NA VITENDO VYA USAFIRISHAJI KWA NJIA YA MAGENDO.


PEMBA
MKUU wa Wilaya ya Chake Chake Salama Mbarouk Khatib, amelaani vikali kitendo cha wananchi kutumia bandari bubu, wakati wakisafirisha bidhaa zisizo halali pamoja na wanyama kwa njia ya magendo na kusema kuwa atahakikisha anadhibiti hali hiyo.

Aliyasema hayo Mkumbuu Shehia ya Ndagoni wilayani humo, wakati walipokamatwa wananchi wakisafirisha Ng’ombe na Mbuzi, huku katika mashua zikigundulika kuwepo kwa madawa ya kulevya yanayosadikiwa kuwa ni bangi yaliyokuwemo kwenye ndoo.

Alisema kuwa, kitendo hicho ni kwenda kinyume na sheria ya Zanzibar, hivyo ni vyema kwa jeshi la Polisi kuwachukulia hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa  wengine wenye tabia kama hiyo.
“Kuna mashua moja inayojulikana kwa jina la ‘NIPE TANO namba 2’ imekamatwa na Ngo’ombe 30 wakiwa na kibali lakini mulikuwa na mafurushi mawili ya bangi na kwenye mashua nyengine imekamatwa na Ng’ombe watatu na Mbuzi mmoja”, alisema Mkuu huyo.

Aliwataja watuhumiwa wa bangi kuwa ni Khamis Mwalim Haji (28) na Mohamed Hakimu Said (22) wote wakaazi wa kisiwa cha Makoongwe Wilaya ya Mkoani.
“Watuhumiwa wengine waliosafirisha Ngombe bila kibali ni Omar Haji Khamis na Khamis Mwadini Juma, ambapo mtuhumiwa wa Mbuzi ni Khamis Kombo Khamis wote wakaazi wa kisiwa cha Uvinje Wilaya ya Wete Pemba”, alifafanua.

Mtuhumiwa wa bangi Khamis Mwalim Haji (28)alikubali kosa lake na kusema madawa hayo alinunua Bagamoyo Dar-es-salaam, ambapo mwenzake Mohamed Hakim Said (22) alikataa kutenda kosa hilo, huku akisema nguo zilizokuwemo kwenye ndoo ndio za kwake na sio bangi.

Watuhumiwa waliokamatwa wakiwa wanasafirisha Ng’ombe na Mbuzi bila ya kibali katika mashua inayoitwa ‘Kimeli’ walikubali kosa hilo na kusema walikwenda kwa sheha kutaka kibali, ambapo walidai kuwa aliwambia kwamba wasafirishe tu.

Nahodha wa mashua ya ‘ NIPE TANO namba 2’ yenye namba za usajili Z1323, Makame Kassim Mohamed, alisema mashua hiyo bandari yake ni Malindi Unguja na kueleza kuwa, mtuhumiwa wa bangi (Khamis mwalim)ni baharia wake.
Nae Nahodha wa mashua ya inayoitwa ‘Kimeli’ alisema kuwa Ng’ombe na mbuzi hao, walikuwa wanatoka Uvinje na kuwapeleka Mwambe Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba na sio wa magendo.
Wananchi hao wamekamatwa Augosti 30, majira ya saa 5:00 mchana, ambapo watuhumiwa wa madawa ya kulevya wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoa wa kusini Pemba.

No comments