Header Ads

WALIMU WANAOTOROKA SHULE MUDA WA KAZI KUCHUKULIWA HATUA ZA KINIDHAMU.


PEMBA

NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe: Mmanga Mjengo Mjawiri, amesema hatovumiliwa mwalimu yoyote, ambae atabainika kutoroka skuli, muda wa kufundisha, ili kukomesha tabia hiyo kwa baadhi ya waalimu.

Alisema kuwa, kuna baadhi ya waalimu wamekua wakitoroka Skuli, muda wa kufundisha, jambo ambalo hatoweza kumvumiliwa mwalimu yoyote, atakae bainika atachukuliwa hatua za kinidhamu.

Aliyasema hayo, wakati alipokua akizungumza na maafisa elimu Kisiwani Pemba, sambamba na kuwakabidhi waalimu wa Skuli za Sekondari Chasasa, Shamiani, Konde na Mauwani vitabu vya masomo ya Sayansi kwa wanafunzi wa madarasa ya kumi na mbili, vilivyotolewa na asasi ya ‘Pemba Support Island (PSI)’ katika ukumbi wa Wizara ya Elimu mjini Chake chake.

“Waalimu tujue wajibu wetu, tuwe wabunifu katika ufundishaji wa wanafunzi, naamini vitabu hivi vitawasaidia katika ufundishaji darasani na kupelekea ufaulu mzuri, katika mitihani ya wanafunzi wetu”, alisema Naibu huyo.

Aidha alisema, Skuli sio sehemu ya kushabikia siasa ingawa hakatazwi mwalimu kushabikia au kuwa mwanachama wa chama chochote, lakini haruhusiwi kuzungumza siasa katika mazingira ya skuli.

Hata hivyo aliwataka waalimu hao, kuvitunza vitabu hivyo na kuacha kuvieka katika makabati, na wawazeshe wanafunzi kuwa na  utamaduni wa kujisomea vitabu, ili kuleta mabadiliko katika skuli.

Kwa upande wake, Afisa Mdhamini wa wizara hiyo Pemba, Salum Kitwana Sururu, alisema msaada huo wa vitabu umetolewa kwa ajili ya kusomeshewa wanafunzi, hivyo Wizara itafanya ufatiliaji, katika Skuli hizo ili kujua utaratibu wake.

“Vitabu hivi tunahitaji kuleta mabadiliko makubwa katika skuli zetu, Shirika la PSI, wameamini kuendelea kutupatia msaada kutokana na ushirikiano na Wizara”, alisema.

Mratibu Idara ya Mafunzo ya Ualimu Pemba, Mkubwa Ahmed Omar, alisema Shirika la Pemba Support Island (PSI), limekua ikitoa mashirikiano makubwa kwa Wizara, ambapo awali iliweza kuwasaidia msaada wa kompyuta 116 na laptop 10.

Hata hivyo alisema PSI, wameahidi kusaidia kompyuta 100 na projecta moja moja kwa Skuli za Pemba, ili kusaidia sekta ya elimu kufikia malengo yake.

Naibu Waziri huyo alikabidhi vitabu vya Chemistry, Physics, Biology, Mathmaticals na English kwa waalimu wa Skuli hizo vyenye thamani ya Shilingi milioni 4,000,000 kwa ajili ya kufundishia wanafunzi kisiwani Pemba.

No comments