Header Ads

JESHI LA POLISI LAAHIDI KUIMARISHA ULINZI KWA AJILI YA SKUKUU YA EID ADH'HA.


PEMBA

JESHI la Polisi Kisiwani Pemba, limesema litaimarisha ulinzi na usalama, katika kipindi chote cha kusherehekea sikukuu ya Idd-el-Hajji inayosherehekewa duniani kote leo hii.

Wakizungumza na waandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Sheihan Mohamed  Sheihan na yule wa Mkoa wa kaskazini Pemba Haji Khamis Haji, walisema kuwa wamejipanga vyema kuhakikisha kuwa na usalama unakuwepo katika viwanja vyote ambavyo vitatumika.

Kamanda huyo wa Mkoa wa Kusini Pemba, aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao, hawawavalishi vitu vyenye thamani kubwa kama vile dhahabu na kuwafuatanisha na watu wanaowaamini.

Alisema ingawa Jeshi la Polisi litakuwepo kuendelea na majukumu yake ya ulinzi, lakini lazima kwa wazazi na walezi nao kuchukuta tahadhari, hasa kwa watoto wao wadogo, kuacha kuwafuatanisha na watoto wenzao.

“Suala la ulinzi wa raia na mali zao, ni letu sisi Jeshi la Polisi, lakini wananchi na wao wanayonafasi kubwa aid kulinda au kushirikiana na sisi katika kuimarisha utulivu”,alisema kamanda Sheihan.

Nae Kamanda wa Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba Haji Khamis Haji, aliwataka wananchi kuendelea kuwa  wastaarabu wa kutii sheria bila ya shuti, kwani kushurutishwa kutii sheria kuna gharama kubwa, jambo ambalo Jeshi la Polisi halingependa kutokea hilo.

Aidha makamanda wa mikoa ya kusini na Kaskazini kisiwani humo, wameendelea kupiga marufuku matumizi ya fataki na silaha  za bandia, na watakaobainika kutumia au kuuza watashughulikiwa kisheria.

“Tunawaomba wananchi wafuate sheria kama tulivyoelekeza, kwani sio vizuri kuvutana kwani lengo letu ni kuona wanakuwa na amani katika kipindi chote cha sikukuu”, walisema makamanda hao.

Akizungumzia maeneo ambayo  hayatatumika katika sherehe hizo za Idd, kwa Mkoa wa kusini Pemba, Kamanda wa mkoa huo, Sheihan Mohamed Sheihan, alisema maeneo yote yaliokaribu na barabara yakiwemo Machomanne, Mtambile Kituo cha Mafuta, Kipapo, Chanjamjawiri, Mtuhaliwa na Mgagadu.

“Wananchi na hasa waliomo kwenye maeneo kama hayo, watengeneze sehemu zenye usalama kama viwanja vya mpira, ambavyo hasa viko mbali na barabara kuu”,alifafanua.

Aidha makamanda hao waliwataka madereva kuheshimu sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizokuwa za lazima, kwani Jeshi la Polisi halitosita kuwachukulia hatua wale wazembe, ambao watakiuka sheria hizo.

Skukuu ya Idd-el-Hajji husherehekewa na mamilioni ya waumini wa dini ya kiislamu duniani kote, kila baada ya kumalizika ibada tukufu ya Hijja inayofanyika Makka Saudia raabia.

No comments