WANAFUNZI WATAKIWA KUITUMIA MAKTABA KWA AJILI YA KUJIFUNDISHA
PEMBA
WANAFUNZI
Kisiwani Pemba, wametakiwa kuitumia maktba ya Kituo cha Huduma za Sheria
Zanzibar ZLSC, iliopo Chake chake, ili waweze kufanikiwa katika masomo yao na
kuongeza taaluma ya masuala mbalimbali yanayohusiana na sheria.
Akizungumza na wanafunzi wa skuli ya sekondari ya
Fidel castro wakati wa maonyesho ya maktaba ya Kituo cha Huduma za sheria, Afisa
Mipango wa kituo hicho tawi la Pemba Siti Habibu Mohamed, alisema wanafunzi
wanapoitumia maktaba hupata fursa ya kujifunza mambo mengi zaidi, kuliko vitabu
vya wanafunzi (kiada).
Alisema kituo hicho, kimeanzisha maktaba hio kwa
lengo la kuwasaidia wananafunzi na wananchi wengine kupata taaluma kupitia
vitabu mbalimbali, vikiwemo vya Uraia(civics), General studies, Historia, Kiengereza,
Sheria na Katiba.
“Maktaba ya Kituo cha huduma za sheria ipo kwa ajili
yenu, muje mujisomee vitabu, bure bila ya malipo yoyote yale”,alisema.
Akifahamisha umuhimu wa Maktaba kwa wanafunzi,
alisema wanapata elimu ya ziada, ambayo inaweza kukosekana katika vitabu vyao
vya kujifunzia skulini, hivyo ni vyema wakaanza kuitumia maktaba hiyo, ili
kuweza kufanikiwa katika masomo yao.
Alisema elimu ya ziada, inayopatikana kupitia
maktaba inamuwezesha mwanafunzi, kukabiliana na changamoto mbalimbali,
zinazowakabili ikiwemo uhaba wa vitabu rejea na uhaba wa wataalamu,
wanaohusiana na mada zinazohusiana na sheria.
Mapema akifunguwa maonyesho hayo, mwalimu Omar Juma
Suleiman aliwaasa wanafunzi hao, kujenga utamaduni wa kusoma vitabu mbali mbali,
kwa lengo la kupata elimu ya ziada na kuweza kukabiliana vizuri na mitihani
yao.
Alisema kujisomea vitabu vingi kunamsaidia
mwanafunzi kukukuwa kiakili zaidi, na kuwa na maarifa makubwa hivyo
kumrahisishia kujibu maswali vizuri na kupata ufaulu mzuri.
“Wanafunzi huu ni wakati wenu wa kujishughulisha na
masomo zaidi kwa lengo la kujitayarishia maisha yenu ya badae, kwani hujuwi
utakuwa nani na utakuwa wapi, hivyo unahitaji elimu ya ziada kuweza kuja
kukabiliana na mazingira yoyote utakayokuwa nayo hapo baadae.
Akitowa maelezo kwa niaba ya wanafunzi wenzake,
baada ya kusoma kitabu kinachohusiana na mada ya rushwa mwanafunzi wa kidato cha nne, Sharifa Jongo
Juma alisema amepata elimu kubwa inayohusiana na rushwa, jambo ambalo litampa
uwezo wa kujibu, maswali yanayohusiana na mada hiyo.
Hivyo alikiomba kituo cha huduma za sheria kuwapatia maarifa ya ziada
yanayohusiana na mada ya rushwa, kwani mbali ya kuwasaidia kwa kukabiliana na
mitihani yao, lakini pia itawafanya kua raia wema katika nchi yao.
Nae mwanafunzi wa Said Salim Said wa kidato cha sita
alifurahishwa na elimu waliyoipata, na kuahidi kukitumia kituo hicho, kwa lengo
la kupata taaluma mbalimbali na kuongeza maarifa zaidi.
Tayari Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi
la Pemba katika mpango wake wa kuwafuata wanafunzi kuwahamasisha kupenda vitabu,
wamekamilisha wilaya zote nne za Pemba, kwa kuzitembela skuli za Miti ulaya,
Tumbe, Mauwani na Fidel castro ambapo wanafunzi zaidi ya 350 wamefaidika.
Post a Comment