Header Ads

WAKULIMA WA MWANI KIJIJI CHA TUMBE WILAYA YA MICHEWENI PEMBA WALIA NA BEI YA ZAO HILO


PEMBA

WAKULIMA wa zao la Mwani kijiji cha Tumbe, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, wamesema bei ya kilo moja kwa shilingi 400 ya zao hilo kutoka shilingi 700, kwa sasa haiendani na mahitaji ya maisha yalivyo.

Walisema mwani kwa sasa umeanguka bei, kutoka shilingi 700 ya zamani hadi shilingi 400 ya sasa, jambo ambalo limewafanya, kujitoa katika kilimo hicho, ambacho kinaelekea kuwakosesha faida kwao.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, kwa nyakati tafauti katika kjiji cha Tumbe, walisema kilimo hicho pamoja na bei kushuka, pia kinakazi kubwa ambayo wala haiendani na pato lake.

 Mkulima wa zao hilo Mwinyi Khatib, alisema bado bei imekuwa ni tatizo sugu na kubwa katika kilimo hicho, hali iliyowafanya waliowengi kushindwa kuendelea na kilimo hicho.

Alisema kwa sasa bei ya kilo moja kwa shilingi 400 kutoka shilingi 700, ipo haja kwa serikali kukipandisha bei kufikia walau  shilingi 1,000 kwa kilo, ili kuendana na hali ya maisha ilivyo.

Kombo Haji Shaali alisema Serikali imelitupa zao la mwani, baada ya kuona halina faida, hali ilivyo tofauti na kwenye zao la Karafuu, ambalo bei iko juu na kuwekewa ulinzi.

Alisema licha juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali, kwa kutoa vifaa vya kuvulia mwani na kamba, lakini bado zao hilo limeonekana halina thamani kwa sasa.

Sheha wa shehia ya Tumbe Mshariki Seif Omar Hamad, alisema wakulima hao, wanapaswa kujuwa ushindani wa biashara katika kulima, kuhakikisha bidhaa yao wanaoyolima, inakuwa safi ili kupata bei nzuri.

Alisema bei ya mwani hutegemea na soko la dunia lilivyo, kuna msimu hupanda na kipindi hushuka pale mwani unapokuwa mwingi katika soko hilo.

No comments