VIKUNDI VYA KUWEKA NA KUKOPA VYAWAINUA KIUCHUMI WANAWAKE PEMBA
PEMBA
WANAWAKE wa
shehia ya Vitongoji wilaya ya Chakechake kisiwani Pemba, wamesema kujiunga kwao
kwenye vikundi vya kuweka na kukopa, ‘hisa’ ni hatua muhimu kwao kuwasaidia
waume zao huduma za kila siku, hasa kwa vile hutokezea siku wanakosa.
Walisema wanaume hawana mkataba na Muumba, kwamba kila siku
watakuwa wanakamilisha hudua za ndani ya nyumba, hivyo kuingia kwao kwenye
vikundi hivyo vya kuweka hisa, pamoja na mambo mengine, lakini pia ni
kuwasaidia wenza wao huduma za lazima.
Wakizungumza na waandishi wa habari wa habari vyombo mbali
mbali, wanawake hao walisema, wamegundua iwapo mwanamme ndani ya nyumba atapewa
msaada kwa baadhi ya siku, hata ndoa zao hupata heshima na nidhamu.
Mwenyekiti wa kikundi cha kuweka na kukopa cha ‘wema hauozi’
Maryam Saleh Juma, alisema ni ukweli usiofichika yeye kabla ya kujiingiza kwenye
vikundi hivyo, hakuona sana thamani ya ndoa yake.
Alisema wanaume wanaokuwa na wanawake wanaosubiri kila huduma
kuletewa, hukosa furaha ya ndoa zao, jambo linalohatarisha usalama na uendelevu
wa ndoa husika, ingawa iwapo mwanamke anamchango huwa tofauti.
“Mfano kama mimi sasa nahisi mume wangu ananielewa kwenye
ndoa, na amekuwa akinishirikisha na kunishauri mambo ambayo kabla nikiona
anafanya uamuzi tu peke yake”,alifafanua.
Nae Katibu wa kikundi hicho Zena Khamis Juma, alisema yeye
kupitia uwanaharakati wake wa upandaji wa mboga mboga na kujiwekea akiba, sasa
amefanikiwa kujenga nyumba ya pili kwa kushirikiana na mume wake.
Alieleza kuwa, ingawa kiwango kikubwa cha fedha alizokuwa
akiziweka kwenye hisa akipewa na mume wake, lakini tayari nyumba hiyo
imekamilika na sasa mume wake ameongeza mke wa pili.
“Mimi sijaona vibaya mume wangu kuongeza mke kwa kushirikiana
nguvu zake na zangu, maana nilimruhusu na sasa nimepata nguvu zaidi ya
kuendelea na ujasiriamali na yeye amenikubali”,alifafanua.
Alisema kwa sasa, wameshakamilisha ujenzi wa nyumba ya kisasa
yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 30, na hana wasiwasi wa kuwahudumia
watoto wake kwa vifaa vya madrassa na skuli.
Nae mume wa mjasiriamali huyo Juma Abrahaman Said, alikiri
kuokolewa kimaisha na mke wake huyo kutokana na ujasiriamali wake anaoendelea
nao.
Alifafanua kuwa msaada mkubwa anaoupata kwa mke wake huyo
umemuwezesha kujenge nyumba ya pilia, ambayo anasema asilimia 40 ya gharama
pamoja na nguvu kazi zilitokana na mke wake.
“Mimi hata nikiamua nyumba kutaka kuiza na tukikubaliana
kuiuza kwa shilingi milioni 30, basi twazigawa sawa sawa, maana kama sio yeye
mimi nisingepaya ujasiri wa kujenga nyumba”,alifafanua.
Hata hivyo amewakumbusha wanaume kuacha dhana potofu kuwa
wanawake wanapojiingiza kwenye ujasiriamali ni uhuni na usema huko ndio
wanakofikia ndoto zao.
Nae Mwenyekiti wa kikundi cha Tumain kinachojishughulisha na
ukulima wa mboga mboga Mtuwa Ali Vue, alieleza kuwa lazima wanaume waache mzaha
wa kuwafungia wake zao, na badala yake wawape uhuru wa kujiletea maendeleo.
“Wakati umefika sasa kwa wanawake kujiwezesha, kinachotakiwa ni
kwa wanaume waliomo kwenye ndoa kuhakikisha, wanawaruhusu wake zao maana
wakiwafungia watawazidisha umaskini”,alifafanua.
Hata hivyo Shamim Haji Makame, alisema bado wapo baadhi ya
wanaume hawajaona umuhimu wa wanawake kuwa na chao, jambo linalopelekea ugumu,
kwa baadhi ya wanawake kuijiingiza kwenye vikundi vya ujasiriamali.
Mkubwa Ali Mkubwa ambae ni mjasiriamali aliewaajiri wanawake
watatu kwenye shamba lake la mboga mboga alisema, kama bado kuna wanaume
wamekuwa wazito kuwaruhusu wake zao kuijiingiza kwenye umoja wa kujiletea
maendeleo, wamechelewa kuamka.
“Hivi sasa tofauti ya mwanamke na mwanamme ni ile ya
kimaumbile tu, lakini kwenye kusaka toke, watu wote wako sawa, maana maisha ya
kuwa goli kipa hasa kwenye ndao yamekwisha”,alifafanua.
Omar Mjawiri Hamad yeye anasema, bado hajaamua mke wake
kumpeleka shambani, kushughulikia kilimo kwa vile yeye mwenyewe anamudu kazi
hiyo.
Sheha wa shehi ya Vitongoji Salum Ayoub Suleiman alisema,
kwenye shehia yake, baada ya wanawake kupata elimu ya ujasiriamali, sasa hali
za maisha yao hasa kwa waliomo ndani ya ndoa yamebadilika.
“Sasa mwanamke wa Vitongoji akiwa anahitaji fedha kwa ajili
ya harusi, fedha za vifaa vya skuli, msiba au michango mengine ya familia, basi
hukopa kwenye hisa au huuza mboga mboga”,alifafanua.
Hata hivyo wakulima hao wa mboga mboga shehiani humo, wamesema
kwa sasa changamoto kubwa inayowarejesha nyuma ni ukosefu wa soko la uhakika.
Shehia ya Vitongoji wilaya ya Chakechake pekee, inajumla
vikundi vya mboga mboga 15 na vya ufugaji 20, hisa 45 na vya ufugaji wa nyuki
zaidi ya 10.
Post a Comment