Header Ads

ZANZIBAR NA CHINA ZAIMARISHA MASHIRIKIANO.



Zanzibar
                                                                 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa hatua za Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na kukuza mashirikiano na uhusiano wa kihistoria ni utekelezaji wa misingi madhubuti iliyowekwa na waasisi wa Mataifa hayo.

Dk. Shein aliyasema hayo  Ikulu mjini Zanzibar katika mazungumzo kati yake na  Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania anaemaliza muda wake wa kazi Dk. Lu Youging, ambaye amefika Ikulu kwa ajili ya kuaga.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alieleza kuwa misingi madhubuti iliyowekwa na waaaisi wa Mataifa hayo akiwemo marehemu Maotse Tung, Marehemu Mwalimu Julius Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ndiyo yanayopelekea pande hizo mbili ziendelee kushirikiana kwani bado zinathamini juhudi za viongozi hao.

Dk. Shein alisema kuwa ni miaka 53 hivi sasa tokea Zanzibar na China zianzishe ushirikiano na uhusiano wao wa kihistoria Zanzibar imeweza kupata mafanikio makubwa kutoka kwa ndugu zao wa China ambao wameweza kuiunga mkono Zanzibar kwa hali na mali.

Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Balozi Youging kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kipindi cha miaka mitano aliyofanya kazi hapa Tanzania na kuweza kuendeleza vyema misingi iliyoachwa na viongozi hao waasisi wa Mataifa hayo.

Dk. Shein alieleza kuwa Balozi Youging ameweza kusimamia vyema na kufanikisha azma ya Zanzibar kuimarisha huduma bora za afya, ujenzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee, ujenzi wa jengo la abiria la uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume baada ya mazungumzo yaliyofanyika kati ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Xi Jinping na Dk. Shein huko nchini China.

Pia, alitumia fursa hiyo kueleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar huku akiahidi kuendelezwa na kudumishwa na kusisitiza kuwa  China imeweza kutoa mchango mkubwa katika kufanikisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya afya, viwanda, kikiwemo kiwanda cha sukari, sigara, viwanda vidogo vidogo, elimu, kilimo pamoja na matrekta.

Aidha, Dk. Shein  aliongeza kuwa China na Zanzibar zimekuwa zikishirikiiana katika kuunga mkono jitihada mbali mbali za maendeleo katika mikutano ya Kimataifa hasa katika misimamo yenye kulingana.

Dk. Shein alitoa pongezi kwa juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa  kusaidia kuwaongezea uwezo wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwapa mafunzo ya muda mrefu na mfupi.

Aliipongeza Serikali ya China chini ya kiongozi wake Rais Xi Jingping na Makamo wake wa Rais Li Yuanchao kwa kuendelea kuisaidia na kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo hasa ile iliyotokana na ziara yake nchini humo mwaka   2013 kutokana na mwaliko wa Rais Xi.

Nae Balozi Lu Youging alitoa shukurani kwa Dk. Shein kwa mashirikiano aliyoyapata kutoka kwake pamoja na viongozi wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wa Zanzibar.

Balozi Youging alisifu mafanikio yaliopatikana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein ambapo katika kipindi hicho Zanzibar imeweza kupiga hatua katika kuimarisha sekta za maendeleo sambamba na amani na utulivu.

Alitoa pongezi kwa Zanzibar kupata mafanikio hayo akiwa anayashuhudia wakati akiwepo nchini na kusisitiza kuwa katika muda wake huo wa kazi nafasi za masomo zimeweza kuongeza na wafanyakazi waliowengi wamepata kwenda kujifunza nchini China.

Balozi Youging aliahidi kuwa China itaendeleza uhusiano wake na Zanzibar hasa katika sekta ya kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji, ambapo nchi hiyo italeta wataalamu pamoja na wawekezaji kwa lengo la kukiimarisha kilimo hicho.

Aidha, Balozi Youging alisifu juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya nishati na kueleza kuwa China iko tayari kushirikiana na Serikali katika kuimarisha sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kushirikiana katika kuipatia Serikali wataalamu wa kuendeleza sekta hiyo.

Pia, aliahidi kuwa China iko tayari kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutafuta njia za nishati mbadala kutokana na vianzio mbali mbali ikiwemo umeme wa nguvu za jua, upepo, makaa ya mawe na vianzio vyenginevyo.

Aliongeza kuwa upatikanaji wa nishati ya uhakika ni hatua muhimu katika kuendeleza sekta nyengine za kiuchumi na kijamii kama vile utalii na viwanda huku akisifu juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utalii, hasa kutoka soko la China pamoja na nchi nyengine za mashariki ya mbali.

Alisema kuwa katika kipindi chake cha miaka mitano hapa nchini ameshuhudia ongezeko kubwa la watalii kutoa nchini China na kusisitiza kuwa juhudi hizo zinafaa kuendelezwa huku akiahidi kuwa licha ya kumaliza muda wake wa kazi nchini bado ataendelea kuwa Balozi wa kuitangaza Tanzania ikiwemo Zanzibar.

Pamoja na hayo, Balozi Youging alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kitaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya chama hicho na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Pia, Balozi Youging aliahidi kuwa Balozi mpya anaekuja kushika nafasi yake atahakikisha anaendeleza mashirikiano yaliopo hasa katika kukamilisha miradi yote iliyoanza wakati wa kipindi chake cha Ubalozi ukiwemo Mradi wa ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume, Bandari ya Mpigaduri na ujenzi wa uwanja wa Maotsetung unaoendelea.

No comments