Masheha Pemba waomba msaada kuwapiga ‘stop’ wanaookota Mpeta

MASHEHA
wa shehia za Jombwe, Chambani na Mwambe wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba, wamesema
kama wakiongezewa nguvu kwenye shehia zao, ili kuwazuia moja kwa moja wanawake
na watoto wanaojihusisha na uokotaji mpeta, wako tayari kwa hilo.
Walisema licha ya agizo
la serikali kuu kwamba hakuna ruhusa kwa wanawake na watoto au mwengine kuokota
mpeta, lakini kwenye shehia zao, ndio pekee zinazotoa kundi kubwa la waokotaji
mpeta tokea kuanza kwa msimu huu.
Wakizunguma na
mwandishi wa habari hizi, masheha hao walisema walishatoa elimu ya kutosha, juu
ya kuwakataza kuokota mpeta, ingawa wapo wanaoendelea kupuuzia agizo hilo.
Sheha wa shehia ya
Mwambe Hamad Haji Faki alisema sio vibaya kama serikali ya wilaya, italiingilia
kati hilo, kwa kushirikiana na wao, ili kuwadhibiti wale wanaopinga agizo la
serikali za shehia, wilaya, Mkoa na taifa.
Alisema ameshajaribu
kuyatumia makundi mbali mbali ndani ya shehia yake, kama vile polisi jamii, wazazi,
walezi, waalimu wa madrassa na waalimu wa skuli, ili kuwaelimisha wananchi
ingawa bado hali ni tete.
Nae sheha wa shehia ya
Jombwe Hakim Khamis Omar, alikiri kuwa shehia yake nayo inayo wananchi,
wanaoendelea kupuuzia agizio la serikali, hivyo lazima sasa asaidiwe nguvu.
“Polisi jamii wapo,
jamii ipo lakini suala la kuokota mpeta wapo wanaoona kama hakuna marufuku
yoyote ya kuokota mpeta, maana wamekuwa, wakitoka makundi kwa makundi”,alisema.
Nae sheha wa shehia ya
Chambani Mohamed Abdalla, alikiri kuwa, wapo wananchi wanaoendelea kupuuzia
agizo hilo, ingawa alishakaa nao muda mrefu, kuwaeleza na kuwakataza.
“Mimi nishakaa na
wananchi wangu, na kuwaeleza wananchi wote kuwa, agizo la serikali kuu ni uwepo
wa marufuku wa kuokota mpeta, ingawa bado wanakwenda kwa wingi”,alifafanua.
Baadhi ya wananchi wa
shehia hizo, walisema hakuna uhusiano baina ya uwepo wa zao la karafuu na
udhalilishaji, hasa kwa vile zipo kesi zilizowahi kuripotiwa, kabla ya kuanza
kwa msimu huu.
Mwanakhamis Haji Mcha,
alisema kisingizio cha mpeta kuchangia ubakaji na udhalilishaji sio sahihi, kwa
vile mwenye tabia hiyo hawezi kukaa kwa kusubiri karafuu.
“Kama kuna mwanamke
anafanya matendo machafu, huyo ni tabia yake hata karafuu zikimalizika, basi
atendelea, maana mtu na tabia yake huwa ni kama ngozi”,alisema.
Hassina Shehe Jaku,
alisema wanachojikinga wao kwenye mashamba ya mikarafuu, ni kukatazana kuiba
karafuu za watu, na kutoingia kwenye mashamba, mwenye aliopiga marufuku.
Kwa upande wake Subira
Haji Vuaa, alisema sio rashisi kufanya matendo machafu kwenye mashamba ya
mikarafuu, kwa huwepo makundi makubwa ya
watu.
Wakati huo huo, uongozi
wa Polisi jamii shehia za Mwambe, Jombwe wamefanikiwa kuwazuia wanawake na
watoto kutotoka majumbani mwao baina ya saa 10: 00 na 10:30 alfajiri, kwenda
kwenye uokotaji mpeta na kutakiwa kuanza kuondoka saa 12:00.
Mkuu wa wilaya ya
Mkoani Hemed Suleiman Abdalla, aliendeela kutoa tamko la kuwataka wanawake na
watoto kuacha kwenda kuokota mpeta, kwani matendo ya udhalilishaji huchukua
nafasi.
Post a Comment