Header Ads

Doria Baharini Yawanasa Wavuvi Haramu Micheweni

Image result for UVUVIIdara ya maendeleo ya uvuvi Kisiwani Pemba, imesema katika shughuli za kuendeleza Doria baharini, imechukua hatua ya kuwafikisha katika vyombo vya sheria wanaokiuka kukata leseni pamoja na wanaojihusisha na uvuvi haramu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Afisa Mkuu wa doria Pemba, Halfan Amour Juma, alisema kwa sasa Serikali kupitia Idara inayoshuhulika na masuala ya rasilimali za baharini haitakua tayari kuwavumilia wanaozarau sheria za uvuvi na kuchangia uharibifu wa mazingira ya bahari.

Alisema, wanajamii pia kwa kushirikiana na taasisi husika wanalo jukumu la kulinda rasilimali za bahari kwa kutoa taarifa sahihi za wavuvi wanaoingia baharini bila ya leseni na kutumia mitengo isiokubalika kisheria, ili kuisaidia Serikali kupata mapato kwa ajili ya maendeleo ya nchi yao.

‘’Sisi kama Idara bado tunaendelea na zoezi la doria na watakao kaidi kufuata sheria zilizopo tutawachukulia hatu, kwa kuwa halituhusu peke etu basi hata taasisi nyengine zitoe ushirikiano, tunaweza kufikia mahali pazuri’’,Mkuu wa doria alieleza.

Kwa upande wake, Afisa Uvuvi, Wilaya ya Micheweni, Mzume Juma Faki, amewataka wavuvi kuacha kutumia mitego isiokubalika pamoja na kukata leseni kwa wakati, ili kuepuka matatizo wanapokuwa katika shughuli zao.
‘’Natoa msisitizo kwa wavuvi wasisubiri shuruti za na kuchukuliwa hatua kazi wanazofanya ni za kila siku, wasikimbie kulipia risiti ndimo Serikali inamotengenezea maendeleo yetu’’, Afisa huyo alieleza.

Hata hivyo alisema kuwa, kutokana na ongezeko la watumiaji wa rasilimali za baharini, inapelekea samaki kupungua kwa kasi katika maji madogo na hivyo kulazimika wavuvi kwenda kina kirefu cha maji kwa ajili ya kupata samaki bora.

Nae Mkuu wa Kituo cha Polisi Michwweni, Inspekta Hatib Sauti Haji, alisema, Idara ya Uvuvi inahitaji kuungwa mkono kutokana  na juhudi wanazozifanya, kwani rasilimali za bahari zimekua ni tegemeo kubwa kwa wanajamii na Serikali kwa ujumla,

Amesema, utumiaji nzuri wa rasilimali hizo ni jukumu la kila mwananchi kwani husaidia kwa asilimia kubwa pato la taifa kwa kufuata sheria zilizopo nchini.

‘’Kila mmoja lazima afuate taratibu zilizopo katika shughuli anazofanya kuepusha usumbufu, na hao wavuvi wanaotumia rasilimali za bahari wakate leseni na waachane na uvuvi haramu sababu ndio tegemeo lao’’, alisema Mkuu wa Kituo Polisi Micheweni.

 Sambamba na hayo amesema kuwa, Jeshi la Polisi litaendelea kutoa ushirikiano na Sekta husika kuwadhibiti watakaopingana na sheria baada ya kufuata taratibu zilizopo na kugundua makosa kwa wahusika watakaofikishwa vituoni.

Aidha Inspekta huyo, alisisitiza kwa  wataalamu wa Uvuvi kutoa taaluma inayostahiki kila muda unaporuhusu juu ya athari za uvuvi haramu na kuvua bila ya leseni, ili wavuvi waweze kupata uwelewa mpana kwa faida yao ni vizazi vijavyo.

Jumla ya Wavuvi wanne watatu wakaazi wa Shehia ya Tumbe Mshariki na mmoja kutoka Shehia ya Sizini Kisiwani Pemba, wamefikishwa kituo cha Polisi Micheweni kwa kushindwa kukata leseni za Uvuvi na Vyombo vyao wanavyovulia pamoja na kumiliki mitego haramu.

No comments