Ushirikiano wa UNFPA,SMZ Wamkuna Rais Dk. Shein
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, amelipongeza Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi
ya Watu Duniani (UNFPA), kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika
kuhakikisha huduma za jamii zinaimarika zikiwemo huduma za afya.
Dk. Shein aliyasema hayo
leo Ikulu Mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Mwakilishi mpya wa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Bibi Jacqueline
Mohan.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Shirika
la UNFPA limekuwa na uhusiano na ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwa muda mrefu na tokea wakati huo limekuwa likichukua juhudi kubwa
kutoa ushirikiano wake katika nyanja mbali mbali hapa nchini.
Alieleza kuwa licha ya kuwepo kwa baadhi ya
changamoto lakini juhudi kubwa zimechukuliwa na mafanikio yanaonekana katika
kupunguza vifo vya akina mama na watoto kwa mashirikiano ya pamoja kati ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Washirika wa maendeleo likiwemo Shirika la
UNFPA.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar hivi sasa imelivalia njuga suala la udhalilishaji wa wanawake na watoto,
katika kuhakikisha linakomeshwa kwani limekuwa likiharibu utamaduni, mila, silka
na desturi za Zanzibar.
Hata hivyo, Dk. Shein alimueleza Mwakilishi huyo
wa Shirika la UNFPA kuwa ana matumaini ya mafanikio kutokana na mashirikiano ya
pamoja kati ya Taasisi za Serikali ikiwemo Wizara ya Afya, Wizara ya Kazi,
Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto pamoja na washirika wengine
yakiwemo Mashirika ya UN.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na kuimarisha miundombunu ya hospitali zake na
kueleza jinsi hatua zilizochukuliwa katika ujenzi wa majengo mapya katika
hospitali kuu ya Mnanzi Mmoja, Hospitali ya Abdalla Mzee, Mkoani Pemba na azma
ya kuikarabati hospitali ya Chake Chake Pemba pamoja na hospitali nyengine za hapa
nchini, Pia aliipongeza UNFPA kwa kusaidia ujenzi wa kituo cha afya cha mama na
mtoto huko Junguni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Dk. Shein alieleza kuwa juhudi kubwa zinachukuliwa
na serikali katika kuimarisha huduma za maendeleo zikiwemo huduma za afya, elimu
na nyenginezo licha ya kukua kwa idadi ya watu nchini kwani Zanzibar idadi ya
watu wake imekuwa ikiongezeka kwa asilimia kubwa ikilinganishwa na nchi za
Afrika ya Mashariki na Kati.
Nae Mwakilishi
mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Bibi
Jacqueline Mohan alitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya
uongozi wa Dk. Shein katika kuimarisha sekta za maendeleo pamoja na kuwapatia
huduma wanawake na watoto.
Mwakilishi huyo aliahidi
kuwa Shirika lake litaendelea kuziunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar za kuwaletea maendeleo wananchi wake sambamba na kutekeleza Malengo na
Mikakati yake iliyoiweka ukiwemo MKUZA III.
Katika maelezo yake,
Mwakilishi huyo alieleza uzoefu wake katika kufanya kazi hapa Zanzibar na
kusisitiza kuwa Shirika hilo litahakikisha mipango yote iliyopangwa kwa ajili
ya Zanzibar inatekelezwa sambamba na kuzidisha mashirikiano katika sekta mbali
mbali za maendeleo na huduma za kijamii ikiwemo sekta ya afya.
Wakati huo huo, Dk. Shein
alikutana na uongozi wa Benki ya CRDB ambao ulifika Ikulu mjini Zanzibar kwa
ajili ya kumkabidhi hundi ya TZS milioni 25 zilizoahidiwa na Benki hiyo kwa
ajili ya mchango wa madawati TZS 20 milioni na TZS milioni 5 ni msaada kwa
ajili ya skuli ya Chekechea ya Madungu iliopo kisiwani Pemba.
Fedha hizo ni ahadi
iliyotolewa na uongozi huo mnamo tarehe 29 Julai 2017 wakati Dk. Shein
alipolifungua Tawi jipya la Benki hiyo huko Madungu Kisiwani Pemba ambapo
akikabidhi fedha hizo, Mkurugenzi Masoko, Tafiti na Huduma kwa Wateja Tully
Esther Mwambapa alimuahidi Dk. Shein kuwa CRDB itaendelea kuziunga mkono juhudi
za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuwaletea maendeleo wananchi wake
Nae Dk. Shein kwa upande
wake alitoa pongezi kwa Benki hiyo na kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wake Dk. Charles Kimei
pamoja na uongozi wake huo kwa mchango wao kwa ajili ya madawati pamoja na
msaada kwa watoto wa skuli ya Chekechea ya Madungu kwa azma ya kuwatengenezea
mazingira mazuri ya kusomea.
Post a Comment