Jitihada za Dkt. Shein zamletea pongezi kutoka ‘Help Age International’

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Kuwahudumia Wazee Duniani ‘Help Age
International’ Arun Maira akiwa na ujumbe wake kutoka Shirika hilo
aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazugumzo na Rais Dk. Shein Ikulu
mjini Zanzibar.
Arun Maura alieleza kuwa Mpango uliochukuliwa na Dk. Shein wa
kuanzisha ‘Pencheni jamii’, kwa wazee waliofikia umri wa miaka 70, bila
ya kujali historia ya kazi walizokuwa wakifanya ni jambo ambalo limeipa
sifa kubwa Zanzibar Kitaifa na Kimataifa.
Alieleza kuwa katika ziara yake hapa Zanzibar alivutiwa sana na
ubunifu unaoendelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya
kuzishirikisha taasisi mbali mbali za Serikali katika kuwalinda,
kuwatunza na kuwaendeleza wazee hapa nchini.
Alisema kwamba hali hiyo ni tofauti na nchi nyingi ambazo suala hilo
hufanywa na taasisi moja peke yake jambo ambalo hupelekea ugumu wa
kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili wazee katika maisha yao.
“Kwa hatua hii , Rais Dk. Shein, Shirika hili linakupongeza sana tena
sana kwani kazi kubwa umeifanya wewe na Serikali yako katika suala zima
la kuwaenzi wazee, kuwatunza na kuwaendeleza na tayari nchi nyingi
zimeona choyo cha kimaendeleo na zinataka kuja kuiga mfumo huu…hongera
sana:”alisema Arua Maura.
Aidha, alieleza kwamba licha ya kuwepo nchi nyingi zilizokuwa na
uwezo mkubwa wa kiuchumi katika Bara la Afrika na duniani kwa jumla
lakini bado hazijaweza kuanzisha utoaji wa Pencheni kama hiyo kwa wazee
wa nchi zao.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa hivi sasa ziko nchi mbali mbali
zinataka kuja kujifunza Zanzibar kutokana na mafanikio yalipatikana
baada ya kuanzisha ‘Pencheni Jamii’ hasa baada ya kupata taarifa
kupititia vyombo mbali mbali vya habari duniani ambavyo vimekuwa
vikiitangaza Zanzibar kutokana na mafanikio hayo.
Nae Rais Dk. Shein kwa upande wake alieleza kufurahishwa kwake kwa
kupata salamu na pongezi hizo na kuona kwamba nchi nyingi zimevutiwa na
utaratibu uliozishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuwajali wazee.
Hata hivyo, alieleza kwamba juhudi anazoendelea kuchukua hivi sasa za
kuwatunza, kuwalinda na kuwaendeleza wazee ni mwendelezo wa fikra na
mawazo ya muwasisi wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ambaye
alibuni na kuazisha mipango na taratibu mbali mbali za kuwatunza wazee
ikiwa ni pamoja na kuanzisha nyumba za wazee Unguja na Pemba.
Hivyo Dk. Shein alieleza kuwa atahakikisha kwamba Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba inaendeleza fikra na mfumo huo
kwa nguvu zake zote hasa ikizingatiwa kwamba wazee wanamchango mkubwa
katika maendeleo yaliofikiwa hivi sasa katika Taifa hili.
Dk. Shein alieleza kuwa wazee ni hazina kubwa hapa nchini na kuahidi
kuwa Serikali anayoiongoza itahakikisha inaendelea kuwaunga mkono wazee
kwa mashirikiano ya pamoja na Mashirika mbali mbali ya ndani na nje ya
nchi.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi maalum kwa Shirika hilo
linalowahudumia wazee Duniani kwa juhudi zake inazoziendeleza katika
kuiunga mkono Zanzibar katika suala zima la kuimarisha ustawi wa wazee
kwa kipindi kirefu tokea kuanzishwa kwake.
Aidha, Dk. Shein alilipongeza Shirika hilo kwa kuendelea kushirikiana
na nchi mbali mbali duniani katika kuwaenzi na kuwatunza wazee.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza kwamba itakuwa ni vyema kwa
ofisi hiyo kuimarisha ofisi zake hapa Zanzibar hatua ambayo itaisaidia
Serikali kufanya kazi kwa karibu na Shirika hilo katika kulinda ustawi
wa wazee.
Post a Comment