Header Ads

Rais Dk. Shein Aipongeza Idara Maalum SMZ kwa Kuzidi Kusimamia Amani Nchini

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akizungumza na Uongozi wa Wizara ya NchI Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa,Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ  katika  kikao cha siku moja cha Utekelezaji wa Mpango kazi kwa kipindi cha robo ya kwanza Julai- Septemba 2017 kilichofanyika leo katika ukumbi wa  Ikulu Mjini Unguja
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amezipongeza Idara Maalum za SMZ kwa kuendeleza vyema majukumu yake ikiwa ni pamoja na kushirikiana na vikosi vya ulinzi na Usalama vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kusimamia amani na utulivu nchini.

Dk. Shein aliyasema hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa , Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ  ilipowasilisha utekelezaji wa Mpango Kazi kwa Mwaka 2016/2017, Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa mwaka 2017/2018 na Utekelezaji wake kwa  kipindi cha robo ya kwanza ya Julai hadi Septemba, 2017.

Dk. Shein alieleza kuridhika kwake na ulinzi wa unaofanywa na Idara Maalum za SMZ na kuweza kufanya kazi kubwa ya kulinda nchi, watu pamoja na mipaka yake na kuzitaka kuendeleza juhudi hizo kwa kutambua kuwa hata wananchi nao wamekuwa wakiridhika na majukumu yao hayo.

Dk. Shein alieleza kuridhishwa na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na uongozi wa Wizara hiyo na kuupongeza uongozi huo kwa kazi nzuri ya uwasilishaji wa Mpangokazi wake katika Idara Maalum za SMZ.

Katika maelezo yake, Dk. Shein aliueleza uongozi wa Wizara hiyo kuwa vikao hivyo ni vya maendeleo ambavyo husaidia kwa kiasi kikubwa kuziwezesha Wizara na Idara zake kuweza kujipima na kujipa uwezo katika utekelezaji wa kazi  zao.

Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja ya umoja na uwajibikaji katika kutekeleza wajibu wa Idara hizo Maalum za SMZ hasa kwa kutambua kuwa vikosi vyenyewe vimekuwa na maadili na nidhamu nzuri ya kazi hivyo ni vyema vikayaendeleza.

Dk. Shein alieleza haja kwa uongozi huo kupitia Idara ya Zimamoto kukaa pamoja na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) wakati utakapoanza mradi wa maji katika mji wa Zanzibar chini ya Benki ya Maendeleo Afrika (ADB) utakapoanza kulaza mabomba kwa kuangalia uwezekano wa kuweka vituo maalum vya maji kwa ajili ya gari za zimamoto kama ilivyokuwa hapo siku za nyuma.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa utafiti kwa Wizara hiyo na kueleza kuwa Serikali imeunda Idara ya Mpango, Sera na Utafiti kwa kila Wizara ikiwa na lengo moja wapo la kufanya tafiti na kusisitiza kuwa Idara Maalum za SMZ ina nyanja nyingi za kufanya utafiti.

Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd aliipongeza Wizara hiyo kupitia Idara zake Maalum za SMZ kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuilinda nchi, nyumba za viongozi pamoja na kusaidia katika suala zima la ujenzi.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza ‘Idara Maalum za SMZ’ kupitia Wizara hiyo kwa mafanikio makubwa iliyoyapata na kuwataka kuimarisha mashirikiano ili waweze kupata mafanikio zaidi .  

Waziri wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri  alisema kwua Ofisi yake imeanza kutekeleza Mpango wa Ugatuzi hatua kwa hatua kama ilivyoelekezwa katika Mpango Mkakati wa Ugatuzi wa mwaka 2016/2017-2018/2019, ambapo kadhaa yametekelezwa.  

Alieleza kuwa pamoja kazi hizo, mambo mengine yaliyofanyika ni pamoja na kujenga uelewa wa dhana ya ugatuzi katika ngazi tofauti, mikutano ya mashauriano ya kisekta ya mafunzo na mikutano na wahusika wengine wakiwemo wahisani.

Aidha, Waziri Kheir alieleza kuwa katika ziara za Rais Dk. Shein za kuitembelea Mikoa ya Unguja na Pemba mnamo mwezi wa Agosti, 2017, maagizo na maelekezo aliyoyatoa kwa Ofisi hiyo yanaendelea kufanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na udhibiti wa magendo ya karafuu na bidhaa nyengine kupitia bandari bubu.

Aliongeza kuwa ni pamoja na kuimarisha mapato katika Serikali za Mitaa ili kuzipa nguvu ya kuhudumia wananchi, kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto, kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya pamoja na kudhibiti utoro wa watoto maskulini.

Uongozi huo ulitoa pongezi kwa Serikari ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa kununua gari za zimamoto pamoja na vifaa vyake katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume hatua iliyopelekea kiwanja hicho kuimarika zaidi na kueleza juhudi zinazochukuliwa katika kuhakikisha suala la mafunzo linapewa kipambele kwenye vikosi vyote vya SMZ.

Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa kuwa boti maalum ya kisasa ya kuzimia moto inatarajiwa kuwasili mwezi ujao pamoja na vifaa vyake huku ukieleza mikakati wanayoendelea nayo katika ujenzi wa chuo cha kikosi hicho huko Kitogani.

Aidha, uongozi huo ulitumia fursa hiyo kufikisha pongezi kwa Rais Dk. Shein zinazotoka kwa wafanyakazi wa Idara Maalum za SMZ kwa kuwaongezea mishahara hatua ambayo imewasaidia katika mabadiliko makubwa ya kimaisha sambamba na kuwasaidia wazee kupata pencheni jamii kwa wale waliofanyakazi na wasiofanyakazi.

Pia, uongozi huo ulieleza juhudi maalum zilizochukuliwa katika kuhakikisha wafungwa wanapata huduma bora na muhumu za kimaisha ikiwemo chakula bora cheye virutubisho vyote vya mwili kwa mpangilio maalum wa kula kutwa mara tatu.

No comments