Rais Dk Shein akunwa na Juhudi za Wizara ya Ujenzi,Mawasiliano na Usafirishaji
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameupongeza uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasilaino na
Usafirishaji kwa juhudi kubwa unazozifanya katika utekelezaji wa kazi zake na
kusisitiza haja ya kuongeza kasi sambamba na kuimarisha umoja na mashirikiano.
Dk. Shein aliyasema hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar
alipokutana na uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji ilipowasilisha
utekelezaji wa Mpango Kazi wake kwa Mwaka
2016/2017, Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa mwaka 2017/2018 na Utekelezaji wake
kwa kipindi cha robo ya kwanza ya Julai
hadi Septemba, 2017.
Aliongeza haja ya kuendeleza vyema majukumu na
utekelezaji wa kazi na kusisitiza umuhimu wa kutekeleza uongozi kwa kuonesha
njia kwa mashirikiano na umoja ili kufikia malengo yaliokusudiwa.
Alieleza kuwa Mpango Kazi wa Wizara hiyo umewafanywa
vizuri na kupongeza kwa hatua hiyo iliyotokana na kuongozwa vyema na uongozi wa
uliopo Wizarani na kusisitiza kuongeza zaidi viwango vya kuongoza ili na wale
wanaoongozwa wapate kufuatia njia sahihi katika kuleta ufanisi na tija katika
kazi zao.
Aidha, Dk. Shein alieleza haja ya kuwepo kwa vikao
kati ya viongozi na watendaji wao hatua ambavyo husaidia kwa kiasi kikubwa
kuondosha changamoto zilizopo sambamba na kujenga uhusiano, mapenzi na
mustakabali mwema kati ya viongozi na watendaji wote wa Wizara.
Alieleza kuwa kwa vile Wizara hiyo ina mambo
matatu makubwa yakiwemo ujenzi, mawasiliano na usafirishaji hivyo, ni vyema
uongozi huo ukafanya kazi kwa pamoja katika kuyatekeleza mambo hayo ambayo ni
makubwa na muhimu katika kuwatumikia wananchi pamoja na kuleta maendeleo
endelevu kwa Zanzibar.
Pia, Dk. Shein alisisitiza suala zima la utafiti
katika Wizara hiyo na kueleza kuwa kila eneo la Wizara hiyo linahitaji kufanyiwa
utafiti kwa azma ya kutoa majibu kutokana na changamoto zilizopo, na kueleza
kuwa kuundwa kwa Idara za Sera, Mipango na Utafiti katika kila Wizara za SMZ
kuna lengo la kuinua Utafiti na kueleza kuwa fedha za utafiti zipo jambo kubwa
ni kujipanga na kuwa tayari katika kutekeleza suala hilo.
Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Idd aliupongeza uongozi wa Wizara hiyo pamoja na watendaji wake wote kwa
mafaniki waliyoyapata na kusisitiza umuhimu wa kuimaarisha mashirikiano ili
Wizara hiyo izidi kupata mafanikio zaidi.
Aidha, alisisitiza haja ya kuangaliwa vyema
miundombinu ya Mji Mkongwe wa Zanzibar zikiwemo nyaya za umeme katika kuta za nyumba
za mji huo na kueleza haja ya kushirikiana kati ya uongozi wa Mji Mkongwe na
Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) ili kuziweka vyema nyaya hizo ili mji huo
uwendeleze haiba yake sambamba na usalama kwa wananchi.
Nae Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Barza
la Mapinduzi ambaye pia, ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Salum Maulid alitoa pongezi za kwa Wizara hiyo na kusisitiza haja
ya uwajibikaji kazini huku akieleza umuhimu wa kwenda kwa mwendo kasi katika
suala zima la mawasiliano hasa kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia
ulimwenguni.
Waziri wa Wizara ya ya Ujenzi, Mawasiliano na
Usafirishaji Balozi Ali Abeid Karume alisema
kuwa Wizara inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia miongozo mbali mbali
ambayo imewekwa na Serikali ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo (Vision 2020),
MKUZA III, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020, Sera ya Taifa ya
Usafiri Zanzibar (2008), Sera ya TEHAMA, Sera ya Taifa ya Nyumba na Mpango Mkuu
wa Usafiri yaa mwaka 2009.
Kwa upande wa usalama wa vyombo vya moto pamoja na
watumiaji wote wa barabara, alieleza kuwa Wizara imefanikiwa kufanya ukaguzi wa
vyombo vya moto vya aina mbali mbali Unguja na Pemba ili kuhakaikisha viko
katika hali uzima na usalama.
Aidha, alieleza kuwa Wizara imekamilisha kuandaa
kanuni za adhabu za papo kwa papo kwa lengo la kuwadhibiti madereva wanaovunja taratibu
za usafiri wa barabara na kwa sasa taratibu za kuanza kutumika kanuni hizo
zinaendelea.
Aliongeza kuwa Wizara katika udhibiti wa maeneo ya
wazi ndani ya Mji Mkongwe imefanya uhakiki wa maeneo ya wazi pamoja na kufanya
vikao na watumiaji wa maeneo hayo juu ya namna ya kuweza kushirikiana katika
kuyahifadhi.
Pia, alieleza kuwa Wizara imefanikiwa kufanya
usajili wa Kampuni inayojulikana kwa jina la ‘Zanzibar Internationa Maritime
Service Limited’ nchini Falme za Kiarabu UAE na hivi sasa Kampuni hiyo
imeshaanza kufanya kazi ya usajii wa meli za Kimataifa kwa niaba ya Mamlaka
ambapo pia, Wizara imefungua Ofisi ya Usajili wa meli za Kimataifa huko Dubai.
Sambamba na hayo, Waziri Karume alieleza kuwa Wizara
imenza maandalizi ya kununua meli mpya ya mafuta ambayo itasaidia kuongeza
huduma za upatikanaji wa mafuta hapa Zanzibar.
Aliongeza kuwa katika vipaumbele vilivyowekwa na
Wizara hiyo katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 ambavyo miongoni mwao ni kuanza
kwa ujenzi wa barabara ya Bububu-Mahonda hadi Mkokotoni wenye urefu wa kilomita
31, kuendeleza ujenzi wa barabara ya Ole hadi Kengeja kilomita 35, kuanza kwa ujenzi
wa barabara ya Koani hadi Jumbi kilomita 6.3 pamoja na kutekeleza ahadi za Rais
wa Zanzibar katika kukamilisha barabara za Unguja na Pemba.
Nao uongozi wa Wizara hiyo ulitoa pongezi kwa
hatua ya Rais Dk. Shein ya kuka pamoja na viongozi wa Wizara za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na kujadili kwa pamoja masuala mbali mbali ya Mpangokazi
hatua ambayo inajenga zaidi ufanisi wa kazi na kuzidisha ari ya kwenda
kuwatumikia wananchi.
Uongozi huo pia, ulieleza kusikitishwa kwake na
hujuma za makusudi zinazofanywa na baadhi ya watu wasioitakia mema Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake kwa kufanya hujuma za makusudi
katika meli mpya ya MV Mapinduzi II.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
Post a Comment