Ujenzi Holela wahatarisha Afya za Wananchi Wilaya ya Wete
WAKAZI wa Mji wa Wete wanaweza kupata athari kiafya zao kutokana na kuendelea kwa shughuli za ujenzi bila ya kufuata taratibu na sheria za ujenzi wa mipango Miji.
Utafiti uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini maeneo mengi yaliyokubwa na janga la mafuriko yamejengwa kinyume na sheria na kuzuia njia ya maji , hivyo kuyafanya yapoteze mwelekeo .
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi jana , wamesema kuwa tatizo hilo la mafuriko ambalo limekuwa likijitokeza limesababisha baadhi ya makazi yao kuharibiwa klwa kuingia maji .
“Maisha yetu kwa kweli yako hatarini iwapo mvua zitaendelea kunyesha , hii imetokana na baadhi yetu kujenga kiholela sehemeu za njia za maji ”alisema Omar Said .
Kutokana na hali hiyo wito wa wasimamizi wa miradi ya ujenzi wametakiwa kufanya tathimini ya mazingira kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi hiyo ili kuepusha athari za kimazingira zinazoweza kutokea .
Farhat Ali Mbarouk kutoka Idara ya Mazingira Zanzibar amesema ujenzi holela wa makazi bila ya kufuata mipango Miji unachangia athari kimazingira ikiwemo mafuriko na mmong’onyoko wa ardhi.
Akichangia kwenye uzinduzi wa kamati ya udhibiti ujenzi Mkoa wa Kaskazini Pemba , amesema kuwa amewataka wananchi hususani wasimamizi wa miradi mikubwa ya ujenzi kuwasiliana na Idara ya Mazingira kufanya tathimini kabla ya kuanza kutekelezaji wake.
“Wapo baadhi ya wananchi hususani wawekezaji wa miradi mikubwa hawafanyi tathimini ya mazingira wakati wanapotaka kuanza utekelezaji wa miradi hiyo jambo ambalo husababisha kutokea majanga kwa jamii ”alisema .
Katibu Tawala Mkoa wa Kaskazini Pemba Ahmed Khalid Abdalla ameeleza kwamba utekelezaji wa ujenzi unaofuata mipango Miji , ni lazima uende sambamba na usafi wa mazingira kwa kuhakikisha kunaandaliwa sehemu maalumu za kuhifadhia takataka .
Amesema Halmashauri na Baraza la Mji wanapaswa kuwa na mfumo mzuri wa ukusanyaji na utumiaji wa taka ngumu ili kusiwepo na tofauti kati ya Halmashauri na Baraza la Mji hali ambayo inachangia uchafuzi wa mazingira .
“Ni lazima utuige kwa nchi za wenzetu ambazo zimefanikiwa katika suala hili , kwani wapo baadhi ya wananchi hawaelewi kwamba ardhi ni mali ya Serikali na kuwafanya waendelea kuvamia na kujenga makazi ”alieleza .
Mkuu wa Wilaya ya Wete Abeid Juma Ali amesema kamati hiyo inatakiwa kuanza na viongozi wa Serikali kwani baadhi yao wanachangia ujenzi holela aidha kwa kutoa vibali au kuwatetea wanaohusika na vitendo hivyo .
Mgeni rasmi kwenye uzinduzi huyo Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Omar amewataka wajumbe wa kamati hiyo kuondoa muhali wanapotekeleza majukumu ya kazi zao
Sambamba na hayo Mkuu huyo wa Mkoa ameitaka kamati hiyo kufanya kazi zake kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizowekwa ili kufanikisha lengo la serikali la kuwepo na makaazi bora ya wananchi .
Amesema taratibu za ujenzi zimeainishwa kisheria , hivyo ni vyema kamati hiyo kuona sheria za ujenzi za ujenzi wa zinasimamiwa na kufuatwa ili zisaidia kupatikana makazi bora .
Mkuu huyo wa Mkoa amesema uwepo wa kamati hiyo , itasaidia kudhibiti shughuli za ujenzi holela wa makazi usiozingatia suala la mipango Miji.
Na Masanja Mabula –Pemba
Post a Comment