CCM ZANZIBAR YAWATAKA WATUMISHI WAKE KUBUNI MIKAKATI ENDELEVU ITAKAYOLETA MABADILIKO CHANYA YA KIMAENDELEO NDANI YA CHAMA
CHAMA Cha
Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka watumishi wake kubuni mikakati
endelevu itakayoleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo ndani ya
Chama katika nyanja za kiuchumi , kijamii na kisiasa.
Wito huo umetolewa na Naibu
Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar , Dk. Abdulla Juma Mabodi wakati akifunga mafunzo
elekezi ya siku moja kwa watendaji wa Afisi Kuu CCM Zanzibar, yaliyofanyika
Kisiwandui Unguja.
Amesema Watendaji ndio
nyenzo muhimu ya kuleta maendeleo ndani na nje ya Chama hicho ili
kiendelee kuwa kinara wa Demokrasia iliyotukuka na Sera zenye manufaa kwa
wananchi wote.
Dk. Mabodi ameeleza kwamba
dhamira ya mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watendaji hao ili waweze kutekeleza
majukumu yao kwa ufanisi.
Akiwasilisha mada ya muundo
wa CCM na namna unavyofanya kazi, Mkufunzi kutoka Makao Makuu ya CCM Dodoma, Filbert
Mdaki Mampwepwe amesema chama hicho ni zao la muungano wa vyama
vya ukombozi vya ASP na TANU, hivyo ni wajibu wa kila mwanachama kulinda na
kutetea urithi huo popote bila hofu.
Ameeleza kwamba toka
kuzaliwa kwa chama hicho 5 februari, 1977 kimepitia katika mabadiliko mbali
mbali ya kisera na kimuundo yenye malengo ya kwenda sambamba na matakwa ya
Katiba ya CCM na Kanuni zake.
Nao baadhi ya washiriki wa
mafunzo hayo waliahidi kuyafanyia kazi kwa vitendo katika sehemu zao za
kiutenda kwa lengo la kuimarisha uhai wa Chama.
Post a Comment