Waziri Aboud: bei mpya ya karafuu bado sana
![]() |
Waziri wa nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa rais Zanzibar Mhe: Mohamed Aboud Mohamed, akielezea namna bora ya kuliimarisha shamba la serikali la Makuwe, wakati waziri huyo alipotembelea shamba hilo.
|



PEMBA
WAZIRI wa Nchi Afisi ya Makamu wa
Pili wa rais Zanzibar Mhe: Mohamed Aboud Mohamed, amesema bado serikali
haijafikiria, suala la kuongeza bei mpya ya zao la karafuu, na kuwataka
wananchi na wakulima kuridhika na bei iliopo kwa sasa.
Alisema,
serikali hufika wakati hulifidia ZSTC kutokana na kujiendesha kihasara, hasa
kutokana na bei ilipo sasa ya shilingi 14,000 kwa kilo moja, ambao inambeba
mkulima kwa kupata asilimia 80 ya bei hiyo.
Mhe: Aboud
alieleza hayo, kabla ya kulitembelea shamba la serikali lililoko Makuwe wilaya
ya Wete, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua shughuli za uchumaji na
uuzaji wa zao la karafuu, linaloendelea kisiwani Pemba.
Alisema ZSTC
halifanyi biashara ya karafuu na wananchi, bali ni kutekeleza agizo la serikali
kuu, kuwahudumia wananchi na hasa wakulima wa zao la karafuu, ili kutimiza
malengo yao kwenye sekta hiyo.
Alisema
tayari serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwajali wananchi wake,
imshajidhatiti kuwa haitoshusha bei iliopo sasa, hataka kama soko la dunia bei itashuka.
Hivyo,
Waziri Aboud alisema, kutokana na ZSTC kujiendesha kihasara na wakati mwengine
kulazimika kuomba kuwezeshwa na serikali kuu, suala la kupandisha bei mpya kwa
sasa bado halijakuwa la kuwaweka kitako na kulizungumza.
“Bei iliopo
sasa ya zao la karafauu, ipo kwa ajili ya kuwaneemesha zaidi wakulima wetu, na
serikali imeshatamka mara kwa mara kuwa, bei hiyo haitoshushwa, maana
vyenginevyo, ni kuwaumiza wakulima wetu”,alisema.
Katika hatua
nyengine Waziri Aboud, aliitaka Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi
kupeleka mpango kazi wa kuliimarisha shamba hilo la Makuwe, ili liimarike
zaidi.
Alisema
shamba hilo ambalo ni tegemeo, kwa sasa linaonekana kuanza kuchakaa kwa miti
yake ya matunda na biashara, hivyo lazima uongozi wa Wizara, ukae na wataalamu
wake, ili wawe na andiko la kuliimraisha.
“Sasa
inaoenekana miti kama mikarafuu imeshakuwa mikongwe, sasa hebu tuleteeni mpango
maalum wa kitaalamu, mutuombe ili kuliimarisha, maana hii ndio hazina
yetu”,alisema.
Katika hatua
nyengine Waziri huyo kutoka Afisi ya Makamu wa Pili wa rais, Mhe: Mohamed Aboud
Mohamed, amewataka wale waliokodi mashamba ya mikarafuu ya serikali, kufanya
hima kurejesha fedha hizo.
Alisema kama
kunachangamoto iliojitokeza baada ya zoezi la ukodishaji kukamilika, wafike kwa
wahusika ambao ni Wizara ya Kilimo, ili kufanya mazungumzo ambayo yatasababisha
kuondoa mivutano.
Mapema Mkuu
wa Idara ya Misitu kisiwani Pemba, Said Juma Ali, alimueleza waziri huyo, kuwa
shamba hilo lenye hekta 79.7 linaundwa na ploti 10, ambapo ndani yake mna
mashamba sita yaliokwisha kodiwa kwa thamani ya shilingi milioni 294.8.
Alisema kati
ya fedha hizo, zilizokwisha lipwa na waliokodi ni shilingi milioni 154, ambapo
shamba hilo linaiingiza mapato makubwa serikali, maana misimu iliopita ilianza
na shilingi milioni 80, na sasa kufikia shilingi milioni 294.8.
Mmoja kati
ya wananchi waliokodi mashamba ya serikali, Jecha Mohamed Faki, aliomba
serikali kumuongezea muda wa kurejesha fedha alizotakiwa kulipa, kutokana na
msimu kuingiliwa na mvua.
Alisema,
alikodi mashamba sita ya serikali kwa thamani ya zaidi ya shilingi milioni 217,
na tayari wastani wa shilingi milioni 120, amesharejesha, ingawa ujio wa mvua
zimesitisha uwanikaji na uvunaji.
Mapema
Mdhamini wa ZSTC Pemba, Abdalla Ali Ussi, aliwataka wananchi na wamiliki wa
mashamha ya mikarafuu, kuendelea kufuata taratibu, ikitokezea mchumaji ameangua
mkarafuu.
Alisema ZSTC
imeshakabidhi kiasi kikubwa cha fedha kwa Shirika la Bima, kwa ajili ya kuwafanyia
tathimini wananchi walioanguka wakati waliokoa zao la taifa na kisha kulipwa.
“Hivi sasa,
tunao tayari idadi ya watu 60 kwa Mkoa wa kaskazini Pemba, pekee wakiwa
wameshanguka kutoka juu ya mkarafuu, hivyo wakitokea wengine waripoti kwa
sheha, wapite Polisi na waende hospitali na kukusanya taarifa zao”,alisema.
Wakati huo
huo Waziri huyo na ujumbe wake, ulikagua kitalu cha miche ya aina mbali mbali
na wanakaya masikini wa shehia ya Mtambwe kaskazini, waliojifufua upya, baada
ya kitalu chao cha awali kutiwa moto.
Mratibu wa
TASAF Pemba Mussa Said Kisenge, alisema kwa hatua za awali wanakaya hao
maskini, waliigawa bure miche kwa wananchi, ingawa kwa mvuno wanatarajia
kupanga namna ya kuwauzia ili nao kurejesha gharama zao.
Post a Comment