DC MICHEWENI: Wazazi Jiepusheni na Rushwa Muhali, Atakaebainika Tutamshughulikia
MKUU wa Wilaya ya Micheweni Salama Mbarouk Khatib amewaonya wazazi wanaofanya suluhu ya matendo ya udhalilishaji na kusema atakaye bainika atachukulia hatua kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani .
Amesema wazazi wanaofanya suluhu juu ya matendo hayo wanachangia kuendelea kutokea katika maeneo yao .
Akizungumza na wakazi wa shehia ya Tondooni akiwa katika ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi , Salama amesema lengo la Serikali ni kuona kwamba wanaotuhumiwa kuhusika na matendo hayo wanawajibishwa kisheria .
“Ole wenu wanaosuluhisha vitendo hivi , sitakuwa tayari kuona familia zinakaa na kukubaliana kulipana fidia kwani athari wanazopata waathirika hayawezi kulipika ”alisema.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi kushirikiana na watendaji wa Serikali katika kupambana na matendo hayo ambayo yanawaathiri zaidi wanawake na watoto na hivyo kufifisha ndoto zao kimaisha.
Ameongeza kwamba kila mmoja anapaswa kuwaogopa kama ukoma wahusika na vitendo vya udhalilishaji na kuacha kuwakumbatia badala yake watoe taarifa kwa viongozi ili waweze kuchukuliwa hatua zinazofaa.
Naye Afisa wa wanawake Wilaya hiyo Bizume Haji Zume amewasisitiza wakazi wa shehia kujiepusha na rushwa muhali na kuhakikisha kila mmoja anakuwa mchunga kwa mtoto wake na jirani yake.
Amesema yapo matukio ya udhalialishaji yanayotokea ndani ya jamii lakini yanashindwa kuripotiwa kutokana na jamii kuona aibu kuyaripoti ngazi husika.
“Acheni rushwa muhali , hakikisheni wahusika wote wa matendo hayo wanaripotiwa kwenye vyombo vya sheria sambamba na kujitokeza kutoa ushahidi ili waweze kutiwa hatiani ” alisisitiza.
Nao wakazi wa Shehia hiyo wamepongeza uwamuzi wa Mkuu wa Wilaya wa kufanya ziara ya kuwatembelea na kusikiliza kero ambazo zinawakabili pamoja na hatua nzuri ambazo anazichukua kutafuta usumbuzi wake.
Post a Comment