Wadau wa Mazingira Kisiwani PEMBA Wajipanga kupambana na Athari za Manadiliko Tabia ya Nchi
WADAU wanaopambana na athari za mabadiliko ya Tabianchi kisiwani Pemba, wamesema ili suala la kupambana na mabadiliko ya tabianchi liweze kufanikiwa Zanzibar, lazima nishati mbadala iweze kupatikana kwa bei rahisi.
Hayo yameelezwa na washiriki wa warsha ya uwasilishaji ya mradi wa uimarishaji uwezo, kwa asasi za kiraia juu ya mabadiliko ya Tabianchi, huko katika Ofisi za CFP Minyenyeni Wilaya ya Wete.
Wadau hao walisema, nishati hiyo ikipungua na elimu ikitolewa kwa kiasi kikubwa, basi wananchi hata wa vijijini wataweza kuitumia na kuondoka na matumizi ya kuni na mkaa.
Hamad Othman Khamis kutoka Wilaya ya Micheweni, alisema bado mwelekeo wa jamii ni mgumu katika suala la kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi, hivyo wakati umefika nishati ya Umeme na Gesi kuwa rahisi ili wananchi waweze kutumia.
Nae Hamdu Salum Abdalla kutoka Jumuiya ya wakulima wa Viungo Pemba, alisema katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar, lazima kuwepo na matumizi bora na rahisi ya nishati, ili kupunguza utumiaji wa kuni na upigaji wa mkaa.
Ameiyomba ZACCA kuhakikisha wanatoa elimu kwa vijana ili waweze kujiajiri wenyewe, kwa kuwapatia misaada mbali mbali itakayoweza kuwasaidia na kuondokana na uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Zanzibar Soud Mohammed Juma, alisema suala la Mabadiliko ya Tabianchi ni janga kubwa kwa Zanzibar, licha ya juhudi mbali mbali zinazochukuliwa katika kukabiliana na athari hizo.
Amesema dunia imekuwa ikipiga kelele sana juu ya suala la kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Zanzibar ni sehemu ya Visiwa imekuwa ikiathirika sana, licha ya juhudi mbali mbali zinazochukuliwa ikiwemo mkakati wa mabadiliko ya tabianchi Zanzibar wa mwaka 2015, umeweka vipaombele mbali mbali ambavyo asasi za kiraia wanautumia.
Amesema maneo mengi yameharibika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, shuhuli za kilimo kusimama, samaki wamekimbia baharini, mashamba yameingi maji chumvi, visima vimeingia maji chumvi baada ya maji matamu.
Nae Mratib wa Mradi na Afisa Tathmini kutoka Jumuiko la Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar (ZACCA) Habiba Juma amesema lengo la mradi huo ni kupeana ujuzi juu ya suala zima la kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aliwataka wadau kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ili Zanzibar iyendelee kuwa salama.
Mkurugenzi mtendaji wa CFP Pemba Mbarouk Mussa Omar, alisema mradi huo ulitekelezwa katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba, miti mingi aina ya mikoko ilipandwa katika maeneo mbali mbali kwa matumizi endelevu ya baadae.
Post a Comment