Header Ads

Mtuhumiwa wa Ubakaji Watoto wake Pemba Atupwa Jela Miaka 5

Image result for UDHALILISHAJI PEMBA 
MAHAKAMA ya Mkoa wa Kaskazini Pemba imemhukumu kwenda chuo cha mafunzo kwa kipindi cha miaka mitano Hamad Omar Hamad (55) wa Kiungoni Wete baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kubaka mtoto wake wa kambo mwenye umri wa miaka 11.

Hamad Omar Hamad mbali na adhabu hiyo pia ametakiwa kulipa faini ya shilingi laki saba (700,000) akishindwa aongezewe mwaka mmoja jela pamoja na kulipa fidia ya shilingi laki tatu (300,000) kwa mwathirika .

Awali Hakimu wa mahakama hiyo Makame Mshamba Simgeni majira ya saa nne asubuhi (siku ya Ijumaa) alilazimika kuahirisha kusoma hukumu baada ya mtuhumiwa kuanguka na kuzimia muda mfupi alipomaliza kutoa utetezi wake , ambapo hukumu ilisita hadi saa tisa na nusu za jioni .

Kesi hiyo ambayo imechukua muda mfupi kuliko kesi nyengine za udhalilishaji zilizoripotiwa katika mahakama hiyo ilifunguliwa Novemba 10  mwaka huu na jumla ya mashahidi wanne walijitokeza kutokeza kutoa ushahidi wao.

Mapema mwendesha mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka wa Serikali Ramadhan Suleiman Ramadhan ameiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa kwani makosa ya ubakaji wa watoto yamekithiri katika jamii .

Akisoma hukumu , hakimu Makame Mshamba Simgeni amesema mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka , hivyo kumuona mtuhumiwa huyo kuwa ni mkosa kisheria , na kumtaka aende chuo cha mafunzo kwa kpindi cha miaka miaka mitano , kulipa faini ya shilingi laki saba (700,000) pamoja na fidia ya shilingi laki tatu (300,000) kwa mwathirika.

Aidha ameeleza kwamba mahakama imetia hatiani mtuhumiwa kwa mujibu wa kifungu cha 126 (i) cha sheria namba 6/2004  sheria za Zanzibar.

Licha ya hukumu hiyo pia ikumbukwe kwamba mtuhumiwa huyo anakesi nyengine katika mahakama ya Wilaya ya Wete ya shambulio la aibu .

Hamad Omar Hamad anadaiwa kuwabaka watoto wake watatu wa kambo wenye umri wa miaka 16, 14,na miaka 11 ambapo mwenye umri wa miaka 16 tayari amempa ujauzito.

Kutokana na hukumu hiyo , sasa Hamad atalazimika kusherekea sikukuu ya mwaka mpya wa 2018 akiwa ni mwanafunzi wa  chuo cha mafunzo akitumia adhabu ya miaka mitano aliyopewa na mahakama ya Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Na Massanja Mabula

No comments