Header Ads

Wakulima Bonde la Koowe Wilayani Micheweni, Waanza Kujipanga Kikabiliana na Athari Tabia ya Nchi

WAKULIMA wa mpunga katika bonde la Koowe Wilaya ya Micheweni wameanzisha kampeni ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa  kupanda miti pembezoni mwa tuta ili kuzuia maji ya bahari yasiyavamie maeneo ya kilimo.

Wamesema kuwa  uwamuzi wa kupanda miti , umekuja baada ya  misimu ya iliyopita bonde hilo kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi  yaliyosababisha  kupungua mavuno ya mpunga.

Wakizungumza na Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Pemba uliofika kukagua maendeleo ya kilimo cha Kunde pamoja na maandalizi kwa ajili ya kilimo cha Mpunga , wamesema mabadiliko ya tabianchi yalisababisha tuta lililojengwa kwa ajili ya kuzuia maji ya bahari kukatika na kuruhusu maji ya chumvi  kuingia kwenye maeneo ya kilimo .

Mwenyekiti wa wakulima katika bonde hilo Faki Khamis Faki amefahamisha kuwa wamekaa na kubaini kwamba  dawa pekee ambayo inaweza kulirejesha bonde hilo katika hali yake za zamani ni kupanda miti pembezoni mwa tuta hilo .

“ Baada ya bonde hili kuvamiwa na maji ya bahari , kulisababisha uzalishaji wa mpunga kushuka , lakini kwa sasa tumeamua kuanzia uatartibu wa kupanda miti ambayo ikiiota itaimarisha bora wake na hivyo kuwawezesha wakulima kuendelea na kilimo kwa ufanisi ”alieleza.

Naye Kaimu Mkuu wa Idara ya Kilimo Pemba Juma Mwalim Faki amesema wamekuwa wakiwashirikisha wakulima katika kusaidia mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kupanda miti.

Ameeleza kwamba katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi , Wizara kupitia Idara ya Kilimo imeandaa uataribu wa kuwashajihisha wakulima kulima kwa wakati  pamoja na kuzingatia ushauri wa kitaalamu .

Katika nasaha zake kwa wakulima hao , Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Omar Khamis Othman amewataka kushirikiana na watendaji wa Wizara ya Kilimo , Maliasili , Mifugo na Uvuvi  katika kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili zikiwemo za mabadiliko ya tabianchi .

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amewashukuru wakulima katika bonde hilo kutokana na juhudi walizozianzisha za kupanda miti ili kuzuia maji ya bahari kuvamia maeneo ya kilimo .

Ameahidi kuwa Serikali ya Mkoa itaongeza nguvu kwa kuzungumza na viongozi wa Wizara husika ili bonde hilo liingizwe kwenye m pango wa mfuko wa maendeleo ya Jamii nchini TASAF .

“Serikali ya Mkoa itaongeza nguvu zake kwa kuomba Wizara husika ili bonde hili liingizwe kwenye mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini TASAF ambao watasaidia kuimarisha tuta hili ”alifahamisha.

Bonde la Koowe lililoko Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba lina ukumbwa wa eka172.25 ambalo kwa sasa nusu limepandwa kunde na arizeti .
Na  Masanja Mabula

No comments