Rais Dk. Shein: Kiswahili Lazima Kiheshimiwe
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza haja ya
kuithamini, kuiendeleza, kuipenda na kuitumia lugha ya kiswahili na kuizungumza
bila ya kuichanganya na lugha ya kiengereza.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo huko katika ukumbi wa Baraza la zamani la Wawakilishi, Kikwajuni mjini
Unguja katika ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili
lililowashirikisha wataalamu wa kiswahili kutoka sehemu mbali mbali duniani.
Katika hotuba hiyo,
Dk. Shein alieleza haja ya kuitunza lugha hiyo na kuendeleza na pale
panapokuwepo wageni basi waandaliwe mazingira ya kuweza kupata machapisho ya
lugha zao lakini lugha ya kiswahi ndiyo itumike huku akieleza kuwa tangu miaka
ya awali ya iliyokuwa Tanganyika sasa Tanzania Bara na Zanzibar baada ya
kujikomboa, Serikali zote mbili zilitambua umuhimu wa kukienzi na kukitunza
Kiswahili.
“Rais wa Kwanza wa
Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume alituasa kwa kusema ‘Tukuza kilicho
chako, mpaka usahau cha mwenzako’ kwa hivyo tuna wajibu mkubwa wa kuitunza
lugha yetu ya Kiswahili”,alisema Dk. Shein.
Alisema kuwa upande wa
Tanzania Bara, Hayati Mwalimu Nyerere wakati akihutubia Bunge mwaka 1962,
alitumia lugha ya Kiswahili kabla ya lugha hiyo haijatangazwa kuwa lugha rasmi
na lugha ya Taifa mwaka 1967 ambapo pia, katika mwaka huo, lilianzishwa Baraza
la Kiswahili Tanzania (BAKITA.
Kwa upande wa
Zanzibar, Dk. Shein alieleza kuwa muasisi wa Mapinduzi Matukufu na Rais wa
Zanzibar , Marehemu Mzee Abeid Amani Karume katika mwezi wa Machi, 1964
alitangaza kuwa lugha ya Kiswahili ndio lugha rasmi na lugha ya Taifa. Kufuatia
hatua hizo za kutoa matamko ya kisera, Dk. Shein anaeleza kuwa Serikali zote
mbili zilianza kuunda taasisi za kukikuza na kukiendeleza Kiswahili.
Aidha, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kueleza jinsi waaandishi mashuhuri walivyochangia
kukiendeleza Kiswahili ikiwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili la
Zanzibar, Dk. Mohammed Seif Khatib pamoja na mabingwa wengine bila ya Marehemu
Siti bint Saad ambaye alichagia kutokana na tungo zake.
Aliongeza kuwa hivi
sasa Kiswahili ni lugha inayotumiwa na watu takriban milioni mia moja na
hamsini duniani ambayo ni lugha ya
Kiafrika inayoongoza kwa kuwa na watumiaji wengi pamoja na kuwepo zaidi ya vyuo
vikuu mia moja duniani vinavyofundisha lugha hiyo na vituo vya redio zaidi ya
idadi kama hiyo.
Dk. Shein alieleza
kuwa mwitikio mkubwa wa washiriki wa kongamano hilo la Kiswahili la Kimataifa
hapa Zanzibar ni kielelezo cha watu kuelewa umhimu wa Kiswahili na ni ishara
nzuri ya kuimarika na kukubalika kwake.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alieleza makosa ya kadhaa ya matumizi ya maneno mbali mbali katika
Kiswahili yanayofanywa na watu kwa kujua au kutokujua na usahihi unaotakiwa kwa
mujibu wa lugha ya Kiswahili fasaha.
Hivyo, kupitia hadhara
hiyo, Dk. Shein alitoa rai kwamba kubainisha makosa ya matumizi yasiyo sahihi
katika lugha kusisubiri wakati wa makongamano na kuitaka BAKIZA, BAKITA pamoja
na wataalamu wote wa lugha hiyo kutekeleza jukumu lao.
Alieleza kuwa Kiswahili
kina utajiri mkubwa wa msamiati la lahaja, hivyo, si lazima watu watohoe maneno
kutoka lugha nyengine na yatumiwe kwenye Kiswahili rasmi.“Kwanza mzingatie
lahaja za lugha ya Kiswahili na baadae lugha za Kibantu, si kila mtu aje na
maneno yake katika mnasaba huu”,alisema Dk. Shein.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alisisitiza haja ya kufikiria kuanzisha kituo maalum ambapo kazi mbali
mbali za waandishi wa Kiswahili wa ndani na nje ya Zanzibar na Tanzania
zitawekwa pamoja na picha za wataalamu wao huku akilishauri BAKIZA kwa
kushirikiana na SUZA kuimarisha vipindi vya lugha ya Kiswhahili kupitia redio
na televisheni ili kuongeza ubora wake.
Mapema akitoa salamu
za vyama vya Kiswahili duniani, Dk. Mahiri Mwita alieleza jinsi lugha ya
Kiswahili inavyozidi kuimarika kutokana na mashirikiano ya vyama hivyo ambapo
Profesa Alwiya Omar Saleh anaefundisha lugha ya Kiswahili katika chuo kikuu cha
Indiana Marekani alieleza jinsi ya lugha hiyo inavyozidin kukua duniani.
Viongozi mbali mbali
walihudhuria katika ufunguzi wa Kongamano hilo la siku mbili akiwemo Makamo wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.
Post a Comment