Utafiti wa Udongo kwa Wakulima Wahimizwa Pemba
WIZARA ya Kilimo , Maliasili , Mifugo na Uvuvi imeshauriwa
kufanya utafiti wa udongo katika mabonde ya Likoni na Kichangani ili
kuwapa maelekezo ya kitaalamu wakulima juu ya udongo na mbolea
ambazo zinaendana na kuwafanya wakulima waweze kuzalisha chakula cha
kutosha kujikimu .
Katibu Tawala Wilaya ndogo Kojani Makame Khamis Makame
amelazimika kutoa ushauri huo baada ya kutembelea bonde ya Likoni na Kichangani
ambapo wakulima wamedai kuwa ni mabadiliko ya tabianchi baada ya mazao yao
kutostawi vyema .
Amesema pamoja na mabadiliko ya tabianchi , lakini iko haja kwa
Wizara ya Kilimo kufanya utafiti wa udongo katika bonde hilo ili wakulima
waweze kujua aina ya mbolea ambazo zinafaa kutumika katika mashamba yao.
Makame ameeleza kwamba wakulima wa kunde katika mabonde hayo
wameitikia wito wa Serikali kulima kwa wakati pamoja na kuzitumia mvua za vuli
ambazo zimenyesha , lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya kutojua aina ya
mbolea inayofaaa kutumiwa .
“Tutaikumbusha Wizara ya kilimo kufanya utafiti wa udongo katika
bonde hili , kwani wakulima bado wanabahatisha kutumia mbolea wakati mwengine
haziendani na udongo uliopo ”alieleza.
Nao wakulima wa kunde katika bonde hilo wamesema kwamba mbali na
changamoto hiyo pia wanakabiliwa na tatizo la wadudu a ina ya wadudu
mafuta (Aphids) wanaoharibu mazao yao .
Kiula Juma Hija amesema kwamba wadudu hao wanakuwa ni kero kubwa
kwa wakulima wa kunde , ambapo hata utaalamu wa kunyunyiza dawa wanaufanya kwa
njia ya kienyeji .
Amefahamisha kwamba , njia ambazo wanazitumia ni kuchanganya
dawa kwenye ndoo , na kuanza kunyunyiza kwa kutumia vitambaa na baada ya hapo
chombo ambacho kimetumika hurejea na kutumika kwa mahitaji mengine ya nyumbani.
Akizungumzia changamoto hiyo , Afisa Maendeleo ya Kilimo Wilaya
ya Wete Makame Hamad Said amefafanua kwamba wanajipanga kuwapatia mabomba ya
kunyunyiza dawa kwa kila kanda bomba moja ili kulinda usalama wa afya zao.
Amesema njia ambazo wanatumia wakulima hao zinahatarisha usalama
wa maisha yao kwani dawa ni sumu na wanatakiwa vyombo wanavyovitumia visitumike
kwa shughuli nyengine majumbani.
“Hii ni hatari sana kwa usalama wa maisha yao , tunajipanga
kuwapatia bomba moja kila kanda kwa kuanzia ili kuwafanya watekeleze majukumu
yao kwa ufanisi zaidi ”alifahamisha.
Aidha mwandishi wa habari amebaini kwamba Zanzibar
hakuna maabara ya udongo ambapo , uchunguzi wa udongo hulazimika kupelekwa
kwenye maabara ya Arusha pamoja na Mlingani Mkoa wa Tanga.
Na Massanja Mabula
Na Massanja Mabula
Post a Comment