Kamanda wa Polisi Mkoa Kusini Pemba: Vifo vilivyotokana na Ajali za Barabarani 2017 ni Watu Wanane, 10 Majeruhi
JUMLA ya watu wanane (8) wamefariki
dunia na wengine kumi (10) kujeruhiwa, kwa ajali za barabarani zilizotokea
mwaka jana Mkoa wa Kusini Pemba.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Sheikhan Mohamed Sheikhan,
alisema jumla ya matukio 18 ya ajali
barabarani yaliripotiwa Mkoani humo.
Alieleza kati ya watu wanane waliofariki, wanaume
walikuwa saba na mwanamke mmoja, ambapo waliojeruhiwa walikuwa ni watu kumi kutokana
na ajali za barabarani zilizotokea mwaka 2017.
“Tunashukuru
ajali za barabarani zimepungua, kuna punguzo la matukio mawili sawa na asilimia
kumi, kwani mwaka 2016 yalipotiwa matukio 20 na mwaka jana yaliripotiwa matukio
18 ya ajali barabarani”, alisema Sheikhan.
Kamanda huyo,
alisema jumla ya makosa 2,928 ya usalama
barabarani yalikamatwa mwaka jana, ambapo makosa 1135 yalipelekwa mahakamani,
makosa 85 yako kwenye upelelezi, kesi 70 zinaendelea mahakamani, kesi 1071
zilifungwa Polisi na kesi 1692 zilipata hatia.
Alieleza kutokana na makosa hayo ya usalama
barabarani waliweza kupata tozo ya Tshs, milioni 36,666,100/= kwa mwaka 2017
katika Mkoa wa Kusini Pemba.
Kamanda
sheikhan, alisema mwaka huu wamejipanga katika kuhakikisha ajali za barabarani
zinaepukika, kwa kuendelea kufanya doria, msako na kuengeza Askari makoti
kusaidia Askari wa barabarani.
Aidha
Kamanda huyo, aliwataka watendaji wa Jeshi hilo kuepuka tabia ya kudai na
kuchukua rushwa, ili kuondosha kabisa makosa ya usalama barabarani yasitokee.
“ Mwaka huu tumejipanga
katika kuhakikisha rushwa haitendeki maana iwapo Askari watakula rushwa makosa
ya haya yataendelea kuwepo kila siku”, alisema Kamanda.
Hivyo
aliwataka madereva kutii sheria bila shuruti, ili kuepuka makosa hayo na
kupunguza ajali zinazoweza kuepukika.
Post a Comment