Mbaroni kwa Kumrawiti Mtoto Miaka Minne WETE-PEMBA
BAKAR Khamis (25) mkaazi wa Mitondooni Wilaya ya Wete, anadaiwa kumnajisi (kumlawiti) mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minne huko Shehia ya Piki Wilaya hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi baba mzazi wa mtoto huyo alisema mtuhumiwa alimchukuwa
mwanawe hadi Bahanasa na kuingia kwenye gari ya abiri na kumpeleka bonde la
Hindi na kumfanyia ulawiti.
Alisema mtuhumiwa
ni mgeni katika shehia hiyo, alikwenda kwa kutembea, ingawa alichokifanya ni
kumchukua mtoto wake na kwenda kufanyia kitendo cha ulawiti, jambo ambalo
linamtia huzuni kila anapofikiria.
“Huyo mtuhumiwa ni mgeni hapa
kijijini kwetu, alipoona tu washamzoea watoto ndipo alipoamua kumchukua mwanangu
kwenda kumlawiti na huko kwao tumesikia kaondoshwa kwa kuwafanyia watoto
kitendo hicho”, alisema baba huyo.
Kwa upande wake mama wa mtoto,
alisema aliondoka na kwenda mazikoni, ambapo mara baada ya kufika
alipigiwa simu na kuambiwa kuwa mwanae amemfuata na ndipo alipofanya haraka ya
kurudi, ingawa alipofika hakumkuta.
“Alimpelea katika bonde la Tangoni
– Hindi na wakati anamlawiti wakatokea watoto wanaochuma mabungo na mtuhumiwa
akakimbia, ndipo walipomuuliza anapoishi na kusema na wakamleta nyumbani”,
alisema mama huyo.
Alieleza mara baada ya kufika mtoto
wao walimuhoji na kusema kuwa kaka Bakar, alimchukua na kwenda kumfanyia
kitendo cha ulawiti na kisha kumpa maandazi, ambapo aliporudi alikuwa nayo
kwenye mfuko.
“Walikuja wazazi wa upande wa
mtuhumiwa tufanye suluhu ili tusiifikishe kesi Polisi, lakini kwa kitendo
alichofanyiwa mwanangu siwezi kusamehe, kwani huu ni ukatili”, alisema mama
huyo.
“Huyu mtoto ana kawaidi ya kucheza
na mwanangu, sasa alikuja mwanangu na kilio na kuniambia kaka ananikimbia,
nikatoka nje nikamwita lakini na mtuhumiwa ikawa anamwita, sasa ikawa kama
tunavutiana, ingawa sikuwa na wasiwasi nae nikaona labda anamfuata tu kwa vile
washamzoea”, alisema jirani wa mtoto huyo.
Nae, kijana mmoja anaeishi mtaa
huo, alisema alimshuhudia mtuhumiwa akiingia kwenye gari na mtoto huyo maeneo
ya Bahanasa na kuteremka Mzambarauni majira ya saa 3:00, ingawa hakujua
alikompeleka kutokana na yeye alikuwa anaenda Wete.
“Mimi sikufanya wasiwasi maana
nilijua ni mdogo wake wa maduguni, kwa hiyo niliporudi ndio nikapata taarifa
hiyo na ndipo nilipokumbuka wakati nilipomuona anapanda nae gari”, alisema kaka
huyo.
Mratibu wa shehia ya Piki, Bikombo
Shazil Makame, alisema tukio hilo limetokea katika shehia yake na tayari
wameshalifikisha kituo cha Polisi Wete, ambapo aliwataka
wazazi kuwa mstari wa mbele kwenda kutoa ushahidi mahakamani, ili kesi iweze
kupata hatia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini
Pemba, Haji Khamis Haji, alisema tukio hilo lilitokea Januari 2 mwaka huu saa
6:00 mchana huko Piki, mtuhumiwa huyo alimnajisi mtoto wa kiume mwenye miaka
minne shehia ya Piki Wilaya ya Wete.
Kamanda huyo, alisema mtuhumiwa
huyo ameshakamatwa na Jeshi hilo linaendelea na upelelezi, ambapo watampeleka
mahakamni mara baada ya uchunguzi kukamilika kujibu tuhuma zinazomkabili.
Matukio ya udhalilishaji kwa watoto
ikiwemo ulawiti yamekuwa yakiongezeka kila siku, kutokana na sababu mbali
mbali, ikiwemo wanajamii kukataa kutoa ushahidi pamoja na kesi kukaa muda mrefu
mahakamani bila ya kupatiwa hukumu.
Post a Comment