Rais Dk. Shein: Zanzibar Itaendelea Kushirikiana na Comoro
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Zanzibar
itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na visiwa
vya Comoro hasa katika kukuza mila na utamaduni ikiwa ni miongoni mwa
utekelezaji wa Mkataba wa Makubaliano kati ya pande mbili hizo.
Akizungumza
na Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini Tanzania Mohammed Fakih Al Baadawy
aliyefika Ikulu mjini Zanzibar, Rais Dk. Shein alimuahidi Balozi huyo kuwa Zanzibar
inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo ambao ulitiwa nguvu zaidi baada
ya kusainiwa Mkataba wa Makubaliano mnamo mwaka 2014, wakati alipofanya ziara
nchini humo.
Mbali ya
uhusiano wa kimaendeleo kati ya Zanzibar na Comoro, Dk. Shein alisema kuwa nchi
mbili hizo zimekuwa na uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu katika kukuza mila
na tamaduni sambamba na mafunzo hasa katika elimu ya dini ya Kiislamu
Katika
maelezo yake, Rais Dk. Shein alimuhakikishia Balozi huyo kuwa Zanzibar
itashiriki kikamilifu katika Kongamano la kimataifa juu ya maisha ya Marehemu Sheikh
Sayyid Omar Abdallah, maarufu Sheikh Mwinyi Baraka litakalofanyika mjini
Moroni, Comoro kuanzia April 03 hadi 06, 2018.
Rais Dk.
Shein aliyapongeza malengo ya Kongamano hilo ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha
vijana juu ya masuala muhimu aliyoyahubiri Sheikh Mwinyi Baraka na kusisitiza
kuwa kwa upande wa Zanzibar wapo wanaomfahamu wakiwemo walimu na wanazuoni wa
zamani ambapo wapo baadhi yao ambao wako hai hivyo, ushiriki wa Zanzibar ni
muhimu katika Kongamano hilo.
Aidha,
Rais Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inathamni sana ushirikiano
na uhusiano uliopo kati yake na Comoro katika sekta ya elimu, hasa elimu ya
Dini ya Kiislamu ambapo wananchi waliowengi wa Visiwa vya Comoro waliipata elimu
hiyo hapa Zanzibar na kwenda kuifanyia kazi katika nchi hiyo.
Aliongeza
kuwa Masheikh, Wanazuoni, na Maulamaa kama vile kina Sheikh Mwinyi Baraka
waliweza kufanya vyema katika kuhakikisha wanakuwa Mabalozi wazuri na
kuitangaza vyema Zanzibar katika sekta ya elimu ya dini ya Kiislamu hivyo, ni
vyema wakakumbukwa kwa juhudi zao hizo.
Hivyo,
Rais Dk. Shein alikubaliana na kupongeza wazo la Balozi huyo wa Comoro katika Ushirikiano
wa Vyuo Vikuu vya nchi hizo kikiwemo chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA )
na Chuo Kikuu cha Comoro katika maandalizi ya Kongamano hilo la Kimataifa
ambalo litazidi kutoa mwanga wa ushirikiano katika sekta ya elimu.
Aidha,
Rais Dk. Shein alisisitiza ushiriki wa Zanzibar katika Kongamano hilo pamoja na
kuunga mkono wazo la kuwepo kwa Makumbusho maalum ya Sheikh Mwinyi Baraka
nchini Comoro ambapo akiwa katika ziara yake nchini humo mwaka 2014 alizuru
kaburi la Sheikh huyo.
Nae
Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini
Tanzania Mohammed Fakih Al Baadawy alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Comoro na
Zanzibar zina uhusiano na ushirikiano mkubwa kati ya nchi mbili hizo pamoja na
watu wake ambao wana udugu wa kihistoria.
Balozi Al Baadawy alimueleza Dk. Shein kuwa Comoro itaendeleza
na kudumisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya pande mbili hizo hasa
katika sekta mbali mbali za maendeleo na zile za kijamii kwa kutambua udugu wa
damu uliopo kwa watu wa nchi mbili hizo.
Aidha,
Balozi huyo alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuendeleza vyema uhusiano na
ushirikiano uliopo kati ya pande mbili hizo ikiwa ni pamoja na kuendelea
kutekeleza Mkataba wa Makubaliano ambapo suala la Mila na Utamaduni
lilihusishwa na limekuwa likifanyiwa kazi vyema na kuanza kuzaa matunda.
Hivyo,
Balozi huyo wa Comoro alitumia fursa hiyo kumueleza Rais Dk. Shein azma ya nchi
yake kufanya Kongamano la Kimataifa kwa ajili ya kumuenzi Sheikh Mwinyi Baraka,
ikiwa ni miaka 100 ya kifo chake sambamba na kumuelezea Sheikh huyo ili azidi
kufahamika na vizazi vilivyopo na vijavyo wakiwemo vijana, ili waweze kuutambua
mchango wake.
Alieleza
kuwa ushiriki wa Chuo Kikuu cha SUZA katika kongamano hilo ni muhimu sana na
utasaidia kupata mambo mengi muhimu kutoka kwa wasomi wa chuoni hapo pamoja na
wadau wengine ikiwemo Taasisi ya Mwinyi Baraka ya Zanzibar huku akieleza
ushiriki wa wadau wengine kutoka Marekani, Uengereza, Ufaransa, Ujerumani na
sehemu nyengine duniani.
Alisisitiza
kuwa Sheikh Mwinyi Baraka alikuwa na
mchango mkubwa katika kuendeleza elimu hasa elimu ya dini ya Kiislamu ambapo
mbali ya elimu ya dini ya Kiislamu pia, alibobea katika elimu ya dunia ambapo
alisoma vyuo mbali mbali duniani na kupata Shahada ikiwemo Chuo Kikuu cha Makerere
Uganda, Oxford cha Uingereza na Vyuo vyengine
vya nchi za Kiarabu.
Sheikh
Mwinyi Baraka alizaliwa Zanzibar mnamo mwaka 1918 na kufariki Comoro mwaka 1988
ambaye alikuwa msomi na mwanachuoni mashuhuri ambapo Kongamano hilo la kwanza
la Kimataifa litaweza kuhamasisha na kuelimisha watu juu ya safari na sifa za
Sheikh huyo ambaye alikuwa mwalimu, mbunge, mwanadiplomasia, mhadhiri, mwanasayansi,
mwanasheria na msomi wa dini.
Post a Comment