Header Ads

Uchimbaji Mawe Karibu na Ikulu ndogo Micheweni Wapigwa Marufuku


Image result for uchimbaji wa mawe pemba
MWENYEKITI  wa Kamati ya Baraza la Mapinduzi Haji Omar Kheir ameelezea kutoridhishwa na uharibifu wa mazingira katika eneo la Ikulu ndogo Micheweni na kuagiza kuchukuliwa hatua kudhibiti vitendo vya uchimbaji wa mawe karibu na jengo hilo .
Amesema ni jambo la kushangaza kuona vitendo vya uchimbaji wa mawe na uvunjaji wa kokoto vinaendelea kushamiri karibu na eneo hilo  jambo ambalo pia linahatarisha usalama wa maisha ya binadamu.
Kheir alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Viongozi wa Majimbo , Madiwani , Masheha pamoja na wajumbe wa kamati za ulinzi na Usalama Wilaya ya Micheweni na Mkoa wa Kaskazini Pemba katika ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Elimu Mbdala Wingwi.
‘‘Iko haja kwa taasisi husika kuhakikisha vitendo vya uchimbaji wa mawe katika eneo la Ikulu Micheweni vinakomeshwa ili kuyalinda mazingira ya jengo hilo ’’alisisitiza.
Aidha Mwenyekiti huyo ambaye aliambatana na baadhi ya Mawaziri , ametumia fursa hiyo kumtaka sheha wa Shehia ya Majenzi pamoja na Diwani wa Wadi ya Micheweni kushirikiana katika kuwaelimisha wachimbaji wa mawe njia mbadala za kufanya kujiepusha na vitendo vya uharibifu wa mazingira.
Katika kukabiliana na vitendo hivyo , wakaazi  wa shehia ya Majenzi wamekubaaliana kuunda kamati ambayo itakuwa na jukumu la kupita sehemu za machimbo ya mawe na kuwaeliisha wananchi kutambua athari za kimazingira.
‘Mbali na kutoa elimu kwa wananchi pia tutafanya mazungumzo na Serikali watutafutie eneo jengine la kuwafanyia kazi zetu ’’ alisema mmoja wa wanawake wa shehia hiyo.
Aidha Mbunge viti Maalumu wanawake Mkoa wa Kaskazini Pemba Maida Hamad ameitaka Serikali kuendeleza marufuku ya zoezi la uchimbaji wa mawe na kokoto katika eneo hilo na kushauri wananchi waruhusiwe kuuondosha mawe na kokoto  zao.
Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Omar Khamid Othman alifanya  ziara ya kutembelea eneo hilo na kusema Serikali inaandaa utaratibu wa kuwapatia elimu ya ujasiriamali ili waache kutegemea kazi ya uchimbaji wa mawe kuendesha maisha yaao .

No comments