Utawala bora waimarika Zanzibar
MIAKA saba imetimia ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ikiangaza nuru ya utawala bora
ambao ni muhimu kwa maendeleo ya nchi kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Bila ya shaka viashiria na chechea za nuru hiyo kwake vilichomoza
tangu Novemba 26 mwaka 2000 hadi 2001 wakati Dk.Shein akiwa kiongozi wa
mwanzo kwa Zanzibar kusimiamia Wizara inayoshughulikia utawala Bora.
Wizara hiyo ilikuwa na jukumu la kuratibu kwa mapana zaidi masuala ya
katiba, utawala bora, sheria pamoja na kusimamia taasisi za kidini.
Kama itakumbukwa mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambapo Dk.
Shein alishinda nafasi ya urais kupitia Chama cha Mapinduzi na
kuzinduliwa kwa serikali ya awamu ya saba ya Zanzibar yenye muundo wa
Umoja wa Kitaifa iliundwa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma
na Utawala Bora. Bila ya shaka kuundwa kwa wizara hiyo imedhihirisha
wazi kwa kiasi gani Dk. Shein amelipa kipaumbele suala hili.
Pamoja na yote hayo suala la utawala bora ni jambo ambalo Rais wa
Zanzibar Dk. Shein analipa kipaumbele na ndio mana analisisitiza katika
kila hotuba zake kwa viongozi na wananchi.
Aidha neno Utawala bora ni kauli ambayo imezoeleka kutoka midomoni
mwa watu wengi hasa kwa wale wenye uelewa juu ya dhana hii maarufu
nchini na ulimwenguni kote.
Hivyo, inapozungumzwa dhana ya utawala bora kimaana halisi ni ile
hali ya utumiaji wa madaraka kiufanisi, uaminifu, usawa, uwazi na
uwajibikaji katika ngazi tofauti serikalini au hata katika asasi za
kiraia na jamii kwa jumla.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akiwahutubia wanasheria katika kilele cha siku ya sheria iliyofanyika ukumbi wa zamani wa baraza la Wawakilishi |
Katika maana nyengine ni mfumo mzima ambao unawapa uwezo wananchi
kuamua namna ya viongozi watakavyosimamia masuala yote ya kiutawala wa
nchi yao.
Ofisa wa haki za binaadamu Hassan Vuai Mchanda, anasema
tunapozungumzia miaka saba ya uongozi wa Dk.Shein juu ya sekta ya
Utawala Bora, kwa hakika hatua iliyofikiwa ni kubwa hasa ikizingatiwa
inatekelezwa kivitendo ambapo mambo mengi yamefanywa katika kuhakikisha
kwamba wananchi wanapata huduma bora.
Kama ilivyo desturi nchi nyingi duniani huongozwa na katiba, hivyo
uongozi wa serikali ya awamu ya saba unahakikisha kwamba Utawala wa
sheria unashika hatamu kwa kuongozwa na sheria mama ambayo ni katiba ya
Zanzibar ya Mwaka 1984 na mabadiliko yake, pamoja na kuhakikisha
mihimili mitatu inafanya kazi bila ya kuingiliana.
Katika kipindi hichi cha miaka saba cha uongozi wa Dk.Shein, kuna
taasisi mbalimbali ambazo zimeanzishwa kwa kuzingatia matakwa ya
wananchi na kuhakikisha misingi ya utawala bora inatekelezwa ipasavyo.
Taasisi hizo ni Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi
(ZAECA),Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Serikali Mtandao
(E-Government), Mamlaka ya Kamisheni ya Utumishi Serikalini, Mahakama ya
Watoto, Mamlaka ya Udhibiti huduma za Maji na Nishati (ZURA) na
nyenginezo.
Katika jitihada hizo Serikali pia kupitia Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ imeanzisha Mkakati wa
upelekaji madaraka kwa wananchi (UGATUZI).
Katika kipindi hiki cha miaka saba ya Dk. Shein ametia saini Sheria
mbalimbali ili ziweze kutatua masuala ya kijamii. Pia Sheria nyingi
zimefanyiwa mapitio ili ziendane na wakati pamoja na mikataba ya
kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.
Aidha watu wa mwambao wa Afrika Mashariki hutumia methali ya kwamba
“Mwenye macho haambiwi tazama” lakini mwandishi wa makala hii ameona
kutimiza wajibu wake kuionesha jamii ufanisi na uwajibikaji uliotukuka
wa Dk.Shein akiwa ndio msimamizi mkuu wa utawala bora Zanzibar.
Hivyo miongoni mwa mambo muhimu mengine yanayoimarisha utawala bora
ambayo yamesimamiwa ipasavyo ni pamoja na Ukarabati wa majengo ya
mahakama mbali mbali, majaji na Mahakimu wameongezeka nchini ili haki
ipatikane kwa wakati.
Kama inavyoeleweka kwamba amani na utulivu ndio dira ya maendeleo,
hivyo alihakikisha msingi huo unachukua nafasi yake ipasavyo na kwa sasa
Zanzibar watu wanaishi kwa upendo na mshikamano bila ya kujali itikadi
zao za kisiasa au tafauti nyenginezo.
Dk. Shein katika kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua ya maendeleo kwa
nafasi alizonazo kikatiba amewateuwa Wawakilishi kutoka vyama vya
upinzani na kuwashirikisha kwa kuwateuwa kuwa wajumbe wa Baraza la
Mapinduzi bila ya kujali itikadi zao za kisiasa. Bila ya shaka hicho ni
kielelezo tosha cha utawala bora nchini.
Mafanikio kwa ujumla katika Taasisi zilizoanzishwa chini ya Dk.Shein katika kuimarisha Utawala Bora.
Kuwepo wa Sera ya Utawala Bora ya mwaka 2011 kumefanikisha uundwaji wa Taasisi hizi kisheria.
ZAECA
Mamlaka ya kuzuia rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) ni
taasisi mpya ambayo iliundwa mwaka 2012 ikiwa na lengo la kupambana na
rushwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Mussa Haji, alisema miongoni mwa
mafanikio ya taasisi hiyo ni kuweza kusaidia kuinua hisia za wananchi
juu ya madhara ya rushwa na uhujumu wa uchumi yanayotakana na vitendo
hivyo pamoja na kuwajenga uelewa wa wananchi kuhusu uhalisia wa madhara
ya vitendo hivyo kupitia taarifa mbalimbali hatimae kupunguza mianya na
vitendo vinavyoashiria rushwa.
Sambamba na hilo,alisema kwa kiwango kikubwa mamlaka hiyo imefanikiwa
kushajihisha wananchi na kuwaelimisha kupitia njia mbali mbali ambapo
hivi karibuni imeanzisha mfumo uwasilishaji taarifa ya vitendo vya
rushwa kwa njia ya simu ambao huduma zake ni bure (Tollfree) kwa namba
ya simu 113 ukiwa na lengo la kurahisisha kuripoti matukio.
Aidha alisema ZAECA inaendelea kuwashughulikia wanaotuhumiwa kufanya
vitendo vya rushwa kwa kuwachunguza na baadhi yao kufikishwa mahakamani,
ambapo alisema kwa mwaka 2017 jumla ya tuhuma 37 zimechunguzwa na
ripoti zake kuwasilishwa na kesi tano kufikishwa mahakamani.
TUME YA MAADILI YA VIONGOZI
Kwa upande wa Tume ya Maadili ya Viongozi ambayo iliundwa 2014, lengo ni kukuza uadilifu kwa viongozi.
Pamoja na mambo mengine, Tume hii inawajibika kusimamia matendo yote
ya viongozi wan chi waliotajwa katika sharia. Miongoni mwa mambo hayo ni
kujua kwa kuhakiki kila mwaka mali za viongozi ili kuelewa ni kwa kiasi
gani hawakushiriki katika kutumia madaraka yao kwa maslahi binafsi na
kujilimbikizia mali.
Pia inafuatilia kwa kupokea malalamiko ya wafanyakazi wa Serikali
kuhusiana na udhalilishaji ama upendeleo wa aina yoyote unaofanywa na
viongozi wa taasisi hizo kinyume na sharia.
Tume imesaidia japo kwa nidhamu ya woga, kudhibiti nyendo chafu,
ukiukwaji maadili na kuvunjwa Sheria kwa viongozi wa taasisi za umma,
jambo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha utawala bora
nchini.
Haya yote yamefanywa na Dk. Shein ili kuweka misingi imara ya utawala
bora nchini ambayo hata atapoondoka madarakani baada ya kumaliza muda
wake ataiacha nchi na wananchi katika merikebu inayosafiri kwenye bahari
tulivu ya utawala bora.
Kabla ya kuundwa Tume hii, mambo yalikuwa yakiwavunja moyo wananchi
na hata kujiuliza kama Serikali ni ya wote au hawa viongozi waliopewa
vyeo tu, kwani ubinafsi, upendeleo na udhalilishaji wa aina tafauti
ulikithiri katika uendeshaji taasisi za umma.
UTAWALA WA SHERIA
Katika kipindi hichi cha miaka saba, Dk.Shein, ili kuhakikisha
Zanzibar unadumu utawala wa sheria amefanikiwa kusaini sheria
zisizopungua 117 ambazo zinasimamia msuala mbalimbali kwa ajili ya
maslahi ya wananchi.
Miongoni mwa mambo muhimu yaliyojenga historia mpya na kuweza
kujivunia katika kipindi cha miaka saba ya uongozi wake kuhusu utawala
bora ni uundaji wa sera ya msaada wa kisheria ambayo katika nchi za
Afrika Mashariki haikuwahi kuwepo.
Naibu Mrajis wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Ali Ameir Haji, amesema
mafanikio mengine katika uongozi wa Dk. Shein ni pamoja na kufanya
uteuzi wa majaji sita kati ya hao watatu ni wanawake ambapo hakujawahii
kutokea kwa Zanzibar tangu Mapinduzi ya mwaka 1964.
“Dk. Shein ameandika historia mpya kwa kuwateuwa majaji watatu
wanawake katika kipindi cha miaka saba cha uongozi wake na kutimia idadi
ya majaji wanane kwani ni jambo jema na la kupongezwa”, alisema.
Nae Ofisa Mipango wa Mahakama Kuu Thuwaiba Amour Haji,alisema eneo
jengine ni kuanzishwa kwa Mahakama za watoto nchini katika mikoa minne
ya Zanzibar, ikiwemo Mahakama ya watoto katika mkoa wa Kaskazini Unguja
ambayo upo Mahonda, nyengine lipo Vuga Mjini Magharibi,Chakechake Pemba
na Wete zenye dhamira ya kulinda haki zao, kurahisisha uendeshaji wa
kesi za watoto na kuweka miundombinu rafiki ya kuwawezesha watoto kutoa
ushahidi kwa wepesi.
“Mahakama ya Mahonda ni jengo jipya lilojengwa na serikali kwa
kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto
(UNICEF)….”,alisema.
Anasema serikali pia imefanikisha kuyafanyia ukarabati majengo matano
ya mahakama ili kuwa na mazingira bora ya utendaji kazi,kuimarisha
mfumo wa kisasa wa kuendesha kesi(Case Managemement systerm) ukiwa na
lengo la kurikodi na kuendesha kesi kwa njia ya kielektroniki.
Bila ya shaka mafanikio yaliyopatikana ni mengi jambo la msingi kwa
kila mmoja wetu kwenye eneo lake la msingi kubuni njia muafaka za
kukabiliana na changamoto zilizopo ili zisiendelee kuwa kikwazo na
badala yake ziwe fursa zitakazo zaa ufanisi na tija.
Kama itakumbukwa Dk.Shein, katika kujenga misingi bora maeneo ya kazi
aliunda sekta ya utumishi wa umma, ambayo inafanyakazi kwa karibu na
taasisi za umma kwa kuhakikisha zinasimamia kwa umakini mipango
iliyojipangia ikiwa kulingana na shughuli zilizopo.
Kuhusu uimarishaji uwajibikaji wa wafanyakazi serikali chini ya
uongozi wa Dk.Shein imeanza uwekaji wa vifaa vya kielektroniki vya
kufuatilia uingiaji na utokaji wa kazini kwa wakati ili kuongeza nidhamu
katika kazi inayopelekea uwajibikaji ambao utakuza ufanisi serikalini
na kuimarisha huduma kwa wananchi.
Katika sekta ya fedha kuna mafanikio makubwa kwa kuanzishwa kwa
mfiumo ya kisasa ya kibenki kwa njia ya simu, hatua hiyo imepelekea
mapato ya serikali kuongezeka na kupunguza uvujaji wa mapato pamoja na
kuharakisha upatikanaji wa huduma kwa wateja na imepunguza mianya ya
rushwa. mwenendo huo umekuza tija katika uhamishaji fedha na kuimarika
kwa huduma kwa urahisi zaidi.
Kama hilo halitoshi, kumekuwa na maendeleo makubwa katika huduma za
kibenki na kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo kwa kutumia simu za
mkononi, mtandao na kadi za ATM na kuwezesha miamala ya kibenki
kuwezekana kufanywa kwa simu au mtandao popote mtu alipo.
UGATUZI
Miaka saba ya Dk.Shein, katika kuimarisha Utawala Bora imeanzisha
mfumo wa Ugatuzi ukiwa na lengo la kupeleka mamlaka za Serikali karibu
na wananchi hususan kwenye ngazi za chini ili kuimarisha na kuharakisha
upatikanaji wa huduma, kurahisisha ushiriki wa jamii katika miradi
mbalimbali ya maendeleo pamoja na kukuza uwajibikaji, uwazi,
ushirikishwaji pamoja na kuzingatia mahitaji ya wananchi. Hatua hiyo
imelenga kuleta ufanisi na tija katika kuleta maendeleo ya wananchi.
Nae Mkurugenzi Idara ya Uratibu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,
Khalid Abdalla Omar,anasema masuala ya ugatuzi yamo katika sheria namba
7 ya mwaka 2014,yakiainishwa kwenye MKUZA 1,11 na 111,hivyo anasema
ndani ya uongozi wake pia imeandaliwa sera ya serikali za mitaa mwaka
2012 ambayo imetoa imetoa tamako la masuala ya Ugatuzi.
Anasema utekelezaji wa ugatuzi umeanza rasmi Julai mosi mwaka
2017,ambapo majukumu ya sekta tatu yamegatuliwa kutoka serikali kuu
kwenda serikali za mitaa.
Anataja sekta ambazo majukumu yake yamegatuliwa ni Wizara ya
Afya,Elimu na Mafunzo ya Amali na Wizara ya Kilimo, Maliasili,Mifugo na
Uvuvi ambapo anasema kwa upande wa elimu ni usimamizi wa elimu ya
maandalizi na msingi,aidha kwa upande wa afya ni huduma za afya ya
msingi na kwa upande wa Wizara ya Kilimo ni huduma ya elimu kwa wakulima
na wafugaji.
“Huduma hizo zote zinatekelezwa na mamlaka za serikali za mitaa
zinakuwa ni Halmashauri za wilaya, Manispaa pamoja na Mabaraza ya
miji”anasema.
Anasema lengo la serikali ni kupeleka zaidi madaraka kwa wananchi ili
waweze kuibua, kupanga, kutekeleza na kutathimini utekellezaji wa
shughuli zao za maendeleo kupitia serikali zao za mitaa.
Hatua nyengine anasema ni pamoja na kuandaliwa kwa mkakati wa miaka
mitatu wa upelekaji wa madaraka kwa wananchi ambao utatumika kwa kipindi
cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2016 hadi 19,ukiwa na vipaumbele vitano
ikiwemo kujenga uwelewa kwa wananchi kuhusu masuala ya Ugatuzi,kuanisha
sera na sheria ili ziweze kukithi matakwa ya ugatuzi,masuala ya ugatuzi
wa fedha kutoka vyanzo mbali mbali,kuwajengea uwezo rasilimali watu na
mwisho kupitia miundo ya kitaasisi.
“Mpango huo utaleta muendeleo na upatikanaji wa huduma muhimu zinazohitajika ndani ya jamii”,anasema.
DIRA NA MALENGO MAKUU
Katika eneo hilo, dira ya Serikali ya Zanzibar ni kuwa nchi
iliyostawi kiuchumi yenye sifa za ukuaji mkubwa wa uchumi wake, umoja,
mshikamano na ustawi wa Taifa.
Katika mtazamo huo,imeelezwa taswira ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais
Katiba na Utawala Bora ni kuwa na nafasi ya juu, heshima na nguvu za
kuweka mifano mizuri kitaifa na kieneo katika kujenga na kuratibu
misingi fanisi na yenye maana ya utawala bora na huduma kwa umma.
Miongozi mwa malengo ya makuu ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
kupitia Wizara hiyo ni kuhakikisha kuwepo kwa utekelezaji wa utawala
bora wenye kuheshimu utawala wa sheria, Haki za Binadamu,
ushirikishwaji, uadililifu na kupiga vita rushwa.
Aidha lengo jengine kuzidisha uwazi katika kushughulikia masuala ya
uwajibikaji wa viongozi na watendaji wa umma na taasisi katika kazi zao
kuhakikisha ufanisi katika taasisi za Serikali. Na kuimarishwa kwa
ufanisi kwenye taasisi za umma na mashirika,ikiwa ni pamoja na kufikisha
huduma muhimu za jamii kwa ufanisi.
WANANCHI
Wananchi mbalimbali wanasema wamefurahishwa na uongozi wa Dk.Shein
kuhusiana na utawala bora nchini hatua inayosaidia upatikanaji wa huduma
kwa baadhi ya taasisi umekuwa ukifuata misingi ya kisheria.
Fatma Mwadini anasema pamoja na mafanikio ya sekta ya utawala bora
ipo haja kwa serikali kuwawajibisha viongozi wote wanaokiuka misingi
yake ili kufikia malengo.
Kwa upande wa Miraji Mpatani (49) anasema wapo baadhi ya viongozi
wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea na kufumbia macho sheria, sera na
katiba hivyo ni vyema serikali ikawaacha mkono ili iwe fundisho kwa
wengine.
Mwanafunzi Ahmeid alisema,pamoja na jitihada za serikali juu ya
usimamizi wa utawala bora nchini wangeanzisha somo maalumu maskulini ili
vizazi na watarajiwa viongozi wawe na taaluma hiyo.
Changamoto katika Utekelezaji Utawala Bora
Miongoni mwa changamoto zinazo ukabikli utawala bora katika kipindi
cha miaka saba ya Dk. Shein ni kukithiri kwa vitendo vya ubakaji zidi ya
wanawake na watoto jambo ambalo limekuwa likileta wasiwasi mkubwa kwa
wananchi.
Changamoto nyengine inaonekana katika suala uwajibikaji. Baadhi ya
watendaji wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea bila ya kufuata sheria na
taratibu za utmishi.
Imefika wakati upo umuhimu kwa jamii kuthamini na kutambua kwamba
kuwepo kwa utawala bora nchini ni nafasi ya kila raia kuweza kutambua na
kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
Post a Comment