Miaka 7 Uongozi wa Dk.shein
Haijawahi kutokea
- Mishahara yapandishwa mara nne
- Uchumi wakua kwa kasi, pato la mwananchi laongezeka
- 437.195b/- zaingia mifukoni mwa wakulima wa karafuu
- Sekta za kijamii zapata msukumo mkubwa
- Utawala bora, amani yaimarishwa
NA MWANDISHI WETU
JUHUDI kubwa zimechukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, katika kipindi cha miaka
saba ya uongozi wake.
UCHUMI
Katika kuimarisha uchumi, amefanikiwa kuongeza ukusanyaji wa mapato
ambapo jumla ya shilingi bilioni 548.571 zilikusanywa mwaka 2017
ikilinganishwa na shilingi bilioni 487.474 zilizokusanywa mwaka 2016.
Aidha katika mwaka 2017, mapato yaliongezeka kwa shilingi bilioni
61.097, ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi cha mwaka 2016, ikiwa ni
sawa na ongezeko la asilimia 12.5.
Aidha katika kipindi hicho, serikali ya Dk. Shein ilifanikiwa
kuongeza pato la taifa kutoka shilingi bilioni 2,308 mwaka 2015 na
kufikia thamani ya shilingi bilioni 2,628 kwa mwaka 2016.
Pato hio lilikadiriwa kufikia shilingi bilioni 2,827 mwaka 2017, kwa
bei za soko. Kutoka na jitihada zilizochukuliwa na serikali tokea
2011/2012, utegemezi wa bajeti kwa mwaka 2017/2018, ulifikia asilimia
7.3, ikilinganishwa na asilimia 30.2 mwaka 2010/2011.
Kuhusu uchumi, Dk. Shein, amefanikiwa kuongeza kasi ya uchumi kwa bei
halisi imekua kwa asilimia 7.0 kwa mwaka 2017, ikilinganishwa na
asilimia 6.8 kwa mwaka 2016.
Pia pato la mtu binafsi nalo limeongezeka na kufikia shilingi 1,806,000 ikilinganishwa na shilingi 1,632,000 kwa mwaka 2015.
MIRADI YA MAENDELEO
Kwa upande wa miradi ya maendeleo, katika kipindi cha Januari hadi
Septemba 2017 miradi 25 iliyopangwa kuingiza mtaji wa dola milioni
276.84 iliidhinishwa na serikali, miradi hii itakapokamilika inatarajiwa
kutoa ajira zisizopungua 915.
Katika mwaka 2017, ujenzi wa mji mpya wa kisasa wa Fumba na Nyamanzi
imeendelezwa kwa lengo la kuimarisha maisha ya wananchi na kubadilisha
taswira ya Zanzibar ambapo jumla ya nyumba 170 zimejengwa katika mradi
wa ujenzi wa “Fumba Satellite City” na nyumba 60 katika mradi wa “Fumba
Town Development”, Nyamanzi.
Pia mradi wa nyumba za kisasa katika eneo la Mbweni unaotekelezwa na
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) wa ujenzi wa majengo 18 yenye
urefu wa ghorofa 7 unatarajiwa kukamilika, karibuni.
Pia mradi wa ujenzi wa hoteli ya kisasa ‘Hotel Verde’ ya nyota tano,
inayojengwa Mtoni Unguja ambao unatekelezwa na kampuni ya SS Bakhressa,
umekamilika.
Aidha katika kipindi cha miaka saba, hoteli ya kisasa ya Park Hyatt imejengwa katika Mji Mkongwe wa Zanzibar.
UIMARISHAJI MIJI
Uimarishaji wa miji umeendelezwa kupitia mradi mkubwa wa huduma za
jamii mijini (Zanzibar Urban Services Project – ZUSP) ambapo awamu ya
kwanza imetekelezwa kwa mkopo wa dola milioni 38 kutoka Benki ya Dunia
ambapo ulijumuisha ujenzi wa miundombinu mbali mbali, ikiwemo misingi ya
maji, uwanja wa Mnazimmoja, majengo, ununuzi wa gari kwa Unguja na
Pemba na ujenzi wa ukuta unaolikinga eneo la Forodhani lisiathiriwe na
bahari.
Ujenzi wa awamu ya pili ya mradi huo umeshatayarishwa na Benki ya Dunia imekubali kutoa mkopo wa dola milioni 55.
UTALII
Katika kipindi cha miaka saba, sekta ya utalii imeendelea kuimarika,
ambapo jumla ya watalii 433,116 waliingia nchini katika mwaka 2017,
ikilinganishwa na watalii 379,242 walioingia nchini mwaka 2016, hilo ni
ongezeko la asilimia 14.2, kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaoingia nchini, kunaonesha wazi
kwamba lengo la kufikia watalii 500,000 ifikapo mwaka 2020, litafikiwa
kabla ya mwaka huo.
UMEME
Kuhusu huduma ya umeme, inapatikana katika shehia zote za Unguja na
Pemba na wananchi wananufaika na huduma hiyo muhimu. Miundombinu ya
huduma hiyo imekamilishwa kwa asilimia 91 na mahitaji ya umeme kwa
Unguja na Pemba yametekelezwa kwa asilimia 60, kwa kadri wananchi
walivyojitokeza kuunga umeme.
Kwa mwaka 2016/2017 jumla ya vijiji 76 vimefikishiwa umeme na mwezi
wa Julai, 2017 umeme umefikishwa katika kisiwa cha Fundo na Januari 6,
2018 ulizinduliwa rasmi.
Azma ya Dk. Shein ni kuufikisha umeme katika kisiwa cha Uvinje hapo
2017/2018, Kokota 2018/2019 na Njau 2019/2020. Hadi sasa umeme
umefikishwa katika visiwa saba vya Zanzibar.
KILIMO
Kwa upande wa kilimo, serikali inaendelea kuwapa wakulima ruzuku ya asilimia 75 ya pembejeo na huduma za matrekta.
Hatua hiyo imepelekea, mavuno ya mpunga kuongezeka kutoka tani 33,655.06 mwaka 2013 hadi tani 39,000 mwaka 2017.
Katika kuwahudumia wakulima kwa msimu wa mwaka 2017/2018, tani 1,800
za mbolea, tani 350 za mbegu ya mpunga na lita 15,000 za dawa za kuulia
magugu zimenunuliwa na kusambazwa kwa wakulima.
Aidha, katika kuhakikisha huduma za matrekta zinakua za uhakika,
serikali imeanzisha Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na zana
nyengine za kilimo. Mbali na matrekta ya zamani yaliyopo kwenye kiwanda
cha matrekta Mbweni, serikali imetiliana saini hati ya maelewano (MoU)
na kampuni ya Mahindra Mahindra ya India ya kununua matrekta 100.
BARABARA
Aidha serikali ya Dk. Shein, katika miaka saba imeendelea na ujenzi
wa miundombinu ya barabara mpya katika maeneo mbali mbali ya Unguja na
Pemba.
Ujenzi wa barabara ya Jendele-Cheju-Unguja Ukuu (km. 11.7), kwa kiwango cha lami na bara bara ya Kwarara-Matumaini zimekamilik.
Vile vile, ujenzi wa barabara ya Bububu-Mahonda-Mkokotoni (km 31)
unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa kwa mkopo wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Ujenzi wa barabara ya Chwale (Madenjani) hadi Mzambarau Takao (km.
5.0) na barabara ya Mgagadu hadi Kiwani (km 7.6), kwa kiwango cha lami
Pemba nao umekamilika.
Pia ujenzi wa barabara ya Ole-Kengeja, (km. 35) unaendelea vizuri,
ambapo kazi ya utiaji lami kutoka Ole hadi Vitongoji (km.7) umefanyika
na jitihada zinaendelea. Aidha barabara ya Mwanakwerekwe-Fuoni
imekamilka na inaendelea kutumiwa.
Mbali na hayo serikali itazijenga kwa kiwango cha lami barabara mbali mbali za vijijini za Unguja na Pemba katika mwaka 2018.
USAFIRI
Katika kuimarisha usafiri wa baharini na usafirishaji wa mafuta,
Disemba 2, 2017, serikali ilitiliana saini na kampuni ya Damen Shipyard
kutoka Uholanzi kwa ajili ya kuanza kutengeneza meli mpya ya mafuta.
Meli hiyo itakapomalizika itachukuwa nafasi ya meli ya MT Ukombozi;
utengenezaji wa meli hiyo utachukua miezi 18.
Katika kumaliza tatizo la usafiri kati ya wananchi wa Pemba na
Unguja, serikali ilitumia zaidi ya dola milioni 30 kutengeneza meli ya
Mv. Mapinduzi II.
Katika kuimarisha usafiri wa anga, ujenzi wa jengo jipya la abiria
linalojengwa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume,
uliosita kwa muda mrefu kutokana na sababu mbali mbali; unaendelea.
Kutokana na hilo mashirika ya ndege yanayotoa huduma katika uwanja huo
yameongezeka.
Kuhusu ujenzi wa bandari mpya ya Mpiga Duri, ujenzi wake utaanza wakati wowote kupitia mkopo kutoka Benki ya Exim ya China.
Aidha, huduma za bandari ya Malindi zimeimarishwa kwa kununuliwa
vifaa vipya vya kuchukulia na kupimia makontena pamoja na vifaa vya
kukagulia mizigo na abiria wanaopita kwenye bandari hiyo na Mkoani.
Katika mwaka 2017, bandari ya Malindi ilihudumia tani za mizigo
mchanganyiko 366,918 na makontena 41,967. Bandari ya Mkoani ilihudumia
jumla ya tani 56,849.53 za mizigo mchanganyiko.
MISHAHARA
Mezi wa Aprili, 2017, serikali ilitimiza ahadi yake, ambapo
ilipandisha mishahara kwa watumishi wa umma katika ngazi mbali mbali,
ikiwa ni mara ya nne tangu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya
saba ilipoingia madarakani mwezi Novemba, 2010. Mishara ilipandishwa
mwaka 2011, 2012, 2013 na hatimae mwaka jana ilipandisha tena mara ya
nne.
Mshahara wa kima cha chini umeongezwa kwa asilimia 100, kwa watumishi wote wa umma, sambamba na kuimarisha maslahi yao mengine.
Pia waajiri katika sekta binafsi, wametekeleza agizo la serikali la kupandisha mishahara ya kima cha chini kwa wafanyakazi wao.
KARAFUU
Katika kipindi cha miaka saba, Dk. Shein amepandisha bei ya zao la
karafuu ambapo pishi moja sasa inanunuliwa kwa shilingi 22,000.
Katika kipindi cha miaka saba, tani 31, 085.60 zenye thamani ya
shilingi bilioni 437.195 ambazo zimeingia kwenye mifuko ya wakulima.
AFYA
Dk. Shein, amefanikiwa kuimarisha sekta ya afya kwa kuhakikisha
hospitali na vituo vya afya vinakuwa na dawa za kutosha kwa ajili ya
wananchi. Katika kipindi cha miaka saba amefanikiwa kusimamia sera ya
afya bure ambayo iliasisiwa na Rais wa kwanza wa Zanzibar, marehemu
Abeid Amani Karume. Hivyo, amefanikiwa kusimamia matengenezo makubwa ya
hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani yaliyofanywa na serikali ya China
pamoja na kuwa na vifaa vya kisasa.
Pia amefanikiwa kuasisi ujenzi wa wodi mpya ya kisasa ya wazazi katika hospitali kuu ya Mnazimmoja.
ELIMU
Katika kuhakikisha kila mwananchi wa Zanzibar anaelimika, Dk. Shein
aliendelea kusimamia sera ya elimu bila malipo. Kufanikisha hilo
ameongeza ujenzi wa skuli za kisasa za ghorofa katika wilaya huku ujenzi
mwengine wa skuli za aina hiyo ikiendelea kutekelezwa kwa kasi. Pia
ameongeza maslahi ya walimu.
Dk. Shein pia ameendelea kutoa mikipo kwa wanafunzi wa elimu ya juu
lengo ni kuhakikisha Zanzibar inakuwa na idadi ya kutosha ya wataalamu
wake katika kada mbali mbali.
Maendeleo haya yanategemea sana kuwepo kwa amani na usalama nchini,
ambao umesimamiwa kwa kiasi kikubwa na serikali ya Dk. Shein.
CHANZO: ZANZIBARLEO
Post a Comment