Header Ads

DC MICHEWENI AKABIDHIWA DUMU 36 ZA GONGO ZILIZO KAMATWA


JUMLA ya Madumu 36 ya Pombe za Kienyeji aina ya Gongo zimekabidhiwa kwa kamati ya ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, ili kuweza kuteketezwa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Mratibu wa Polisi jamii wa Shehia, Koplo Issa  Farouk amesema kuwa kukamatwa kwa Dumu hizo ni kutokana na juhudi zinazofanywa na Kikosi cha Ulinzi Shirikishi katika Shehia mbalimbali.

Amesema kuwa baada ya Polisi jamii katika Shehia za Kifundi na Matanga Tuani Wilaya ya Micheweni kubaini kuwepo kwa watu wanaojihusisha na utengenezaji wa Pombe hizo walifanya doria na kufanikiwa kukamata Pombe hizo.


“tumekuwa tukipata taarifa kuwa kuna watu huku wanajihusisha na uuzaji wa Pombe haramu hivyo Polisi jamii kwa mashirikiano tuliamua kufanya doria katika maeneo hayo na hatimaye tukafanikiwa kukamata madumu haya 36 ambayo yalikuwa yanaandaliwa kwaajili ya kutengeneza Pombe,” alisema Farouk.

Fatuma Omar Mkaazi wa Shehia ya Kifundi amesema kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la matendo ya uharifu yanayotokana na athari za Madawa ya Kulevya na Pombe jambo ambalo limepelekea wanaume kufanywa wanawake kwa kulawitiwa.

“Hivi sasa hali imebadilika, imefikia hatua hadi mzazi anaona ni bora kuzaa mwanamke kutokana na vitendo vya aibu vinavyozidi kuongezeka katika jamii yetu ambavyo kwa kiasi kikubwa vinasababishwa na haya madawa ya kulevya na hizi Pombe haramu,” alisema  Omar.

Wakipokea madumu hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambae pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Salama Mbarouk Khatib amewataka wananchi kuendelea kutoa mashirikiano katika vita ya kupambana dhidi ya dawa za kulevya na Pombe haramu katika wilaya hiyo.
"nikuombeni tutoeni mashirikiano kwa viongozi wetu, na kwa hili naomba kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake, unapohisi kunasehemu vitendo hivi vinfanyika,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

Kwa upande wao baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wamesema kuwa hali imekuwa mbaya kwa sasa kutokana na kila siku kuendelea kuongezeka kwa uhalifu katika jamii.

Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Micheweni kwa kuongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo inaendesha Oparesheni katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha dawa za kulevya na Pombe haramu zinamalizika.
KIKUNDI CHA ULINZI SHIRIKISHI (Polisi Jamii) KIKITOA MADUMU YA POMBE HARAMU AINA YA GONGO YALIYOKAMATWA TAYARI KWA AJILI YA KUYAKABIDHI MBELE YA KAMATI YA ULIZNI NA USALAMA WILAYA YA MICHEWENI. (PICHA NA GASPARY CHARLES).

No comments