'Kujibu hoja za CAG ni kinyume cha Sheria'- ZITTO
Mbunge wa Kigoma
(ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amesema kitendo cha mawaziri kujibu hoja za
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ni kinyume cha Sheria ya
Ukaguzi wa Hesabu za Umma na kifungu 38 (1 na 2).
Akizungumza leo Aprili 15
mjini hapa, Zitto amesema kifungu hicho kinaeleza namna hoja hizo zinavyotakiwa
kujibiwa na kwamba mawaziri wamekuwa hawatajwi kabisa katika kifungu hicho.
“Wanaopaswa kujibu hoja za CAG ni maofisa masuhuli ambao ni makatibu
wakuu wa wizara, siyo kujibu kwa kuita mikutano na wanahabari bali kujibu kwa
kutokea katika kamati (za Bunge za Hesabu),”
amesema.
Amesema kinachofanwa na
mawaziri ni kinyume cha sheria na kwamba, sheria imeweka adhabu kwa makosa hayo
ya juu kabisa ikiwa ni kifungo cha miaka miwili jela au faini ya
Sh5 milioni.
“Nawasihi mwenyekiti wa kamati ya PAC na mwenyekiti wa kamati ya LAAC
wafikishe jambo hili kwa Spika ili amuandikie Waziri Mkuu kumweleza kuwa,
mawaziri wanavunja sheria. Kinachonisikitisha ni kuwa baadhi ya mawaziri
waandamizi ndiyo wanaongoza zoezi hili,”
amesema.
Amesema anafahamu
wanachokifanya mawaziri hao ni kuhamisha mjadala, kwa kuwaondoa watu katika
hoja za msingi ambazo CAG ameziibua ili zisijadiliwe.
Post a Comment