Mpango wa lishe kwa kaya masikini wazinduliwa
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii
Tanzania (TASAF III), kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la
kuhudumia Watoto (UNICEF), umezindua mradi wa kustawisha maisha kwa ajili ya
kuboresha afya na lishe kwa akinamama na watoto wanaoishi katika kaya masikini.
Mratibu wa TASAF III
Zanzibar, Makame Ali Haji alieleza hayo katika uzinduzi wa mradi huo hafla
ambayo iliyofanyika Bumbwini wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.
Alisema imebainika kwamba
akina mama na watoto wamekuwa wakikabiliwa na tatizo ya ukosefu wa lishe ya
kutosha na hivyo kushindwa kumudu kuendesha familia zao vizuri.
Alisema mpango huo kwa kiasi
kikubwa utatoa nafasi kwa akinamama kupata lishe bora kwa kutumia vyakula
vyenye mpangilio ikiwemo mboga na matunda.
Mratibu huyo alifahamisha
kuwa mpango huo umeanza kwa majaribio katika mikoa miwili ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, ambapo kwa Zanzibar ni mkoa wa Kaskzini Unguja na
halmashauri ya Mbeya vijijini Tanzania bara.
”Mpango wa kustawisha maisha
ni sehemu ya utekelezaji wa mfuko wa maendeleo ya jamii wa kunusuru kaya
masikini awamu ya tatu ambapo kwa sasa tumelenga zaidi katika kuwahusisha
akinamama na watoto katika kuimarisha lishe zao kuwa bora”,alisema.
Alisema TASAF III imejikita
zaidi katika kupambana na umasikini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya
Chama cha Mapinduzi na mpango wa kukuza uchumi mkuza namba tatu.
Mtaalamu wa mafunzo na
ushirikishwaji jamii kutoka makao makuu ya Tasaf Dar es Salaam, Mercy Mandawa
alisema mpango huo umebuniwa na Tasaf kwa kushirikiana na shirika la Umoja wa
Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa ajili ya kuimarisha na kukuza afya za
akinamama na watoto kuwa bora.
CHANZO: ZANZIBARLEO
Post a Comment