RAIS DK. SHEIN: SMZ KUPITIA WIZARA ZAKE TUTAENDELEA KUTOA MASHIRIKIANO KWA WAWEKEZAJI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Kampuni ya ‘Kunshan Asia
Aroma Cooperation Limited” kutoka nchini China kwa uamuzi wake wa kuja kuekeza
hapa Zanzibar.
Dk. Shein
aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na ujumbe
kutoka Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” kutoka nchini China
ambayo imedhamiria kuekeza katika kiwanda cha Makonyo, kilichopo Wawi Pemba kwa
kushirikiana na Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC).
Katika
mazungumzo hayo, Dk. Shein aliihakikishia Kampuni hiyo kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar itatoa ushirikiano wake mkubwa kupitia Wizara yake ya
Biashara na Viwanda pamoja na Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC).
Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kuipongeza Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation
Limited” chini ya Mwenyekiti wake Zhou Junxue kwa kusaini Makubaliano ya Awali
kati ya Kampuni hiyo na Shirika la (ZSTC).
Aidha, Dk.
Shein aliueleza ujumbe wa Kampuni hiyo kuwa Kiwanda cha Makonyo kilichopo Wawi
ni cha muda mrefu ambacho kimekuwa kikizalisha mafuta ya aina mbali mbali hivyo,
ushirikiano wa pamoja katika uzalishaji kiwandani hapo kutasaidia kuinua ubora
wa kiwanda sambamba na kuongeza pato la Taifa na soko la ajira.
Alieleza
kuwa uwamuzi wa Kampuni hiyo ni mzuri na umekuja katika wakati muwafaka ambapo
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imo katika kutekeleza Sera ya Uchumi wa
Viwanda, hivyo hatua hiyo itakuwa chachu katika kufikia malengo yaliyowekwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Pamoja na
hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar imejaaliwa kuwa na viungo vya vyakula
vya aina nyingi ambavyo miongoni mwao vimekuwa vikitoa mafuta bora ambayo
yamekuwa ni bidhaa muhimu iliyoingia katika soko la ndani na nje ya Tanzania
yakiwemo mafuta ya makonyo, mafuta ya karafuu na mafuta ya mikaratusi.
Hivyo, Dk.
Shein aliongeza kuwa kuanza kwa uwekezaji huo kutazidi kuitangaza Zanzibar na
kuwa kiwanda cha pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kinachozalisha
bidhaa hizo za mafuta.
Sambamba
na hayo, Rais Dk. Shein alieleza haja ya Kampuni hiyo kushirikiana na ZSTC
katika kutekeleza makubaliano hayo yaliotiwa saini hapo jana ikiwa ni pamoja na
kuongeza zaidi uzalishaji huku akisisitiza suala zima la ufanyaji utafiti
katika kilimo cha mazao hayo yanazotoa mafuta.
Aidha, Dk.
Shein alisisitiza suala la mafunzo ambalo litasaidia sana kuendesha kiwanda
hicho pamoja na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za aina mbali mbali za mafuta ya
viungo kutoka katika kiwanda hicho cha Makonyo Wawi jambo ambalo pia,
litaongeza soko la ajira hapa nchini.
Nae Mwenyekiti
wa Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” ya China, Zhou Junxue
alimpongeza Rais Dk. Shein kwa juhudi zake katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar
kwa kupitia sekta ya viwanda vikiwemo viwanda vidogo na vya kati.
Mwenyekiti
wa Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” alimueleza Rais Dk.
Shein mikakati iliyowekwa na Kampuni yake katika kuhakikisha makubaliano
waliyosaini yanatekelezwa kwa lengo la kuleta manufaa kwa pande zote mbili.
Junxue alimuhakikishia
Rais Dk. Shein kuwa Kampuni yake itatoa mashirikiano makubwa kwa Serikali
kupitia Shirika lake la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) katika kuhakikisha
kiwanda hicho kinatoa mafuta yalio bora sambamba na kuongeza uzalishaji wa
bidhaa zitakazozalishwa katika kiwanda hicho cha Wawi.
Kampuni ya
“Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” ya nchini China ambayo ndio mnunuzi mkubwa
wa mafuta ya viungo vya Zanzibar tokea Julai mwaka 2017, ilitiliana saini Makubaliano
ya Awali na Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) katika kuendesha mradi
ndani ya miaka kumi utaohusisha uimarishaji wa utendaji na utaalamu katika
kiwanda cha Makonyo Wawi.
Jambo
jengine ni uendelezaji wa mazao ya karafuu na mikaratusi ili kuongeza
uzalishaji kutoka tani 60 zinazozalishwa hivi sasa hadi kufikia tani 2,000, ubadilishanaji
uzoefu kati ya watendaji wa taasisi hizo, upatikanaji wa mafunzo, mbinu na
upatikanaji mbegu bora za mikaratusi ni
miongoni mwa makubaliano hayo.
Post a Comment