Header Ads

Dk. Shein: 'CCM Itashinda kwa Kishindo Uchaguzi Mkuu Ujao'



 
MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amewahakikishia Mabalozi wa Wilaya ya Micheweni kuwa CCM itashinda kwa kishindo Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020 kwani hakuna mbadala wa CCM.

Dk. Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Barazza la Mapinduzi aliyasema hayo leo katika ukumbi wa Skuli ya Micheweni wakati alipokuwa akizungumza na Mabalozi wa Wilaya ya Micheweni Pemba.

Alieleza kuwa CCM imefanya mambo mengi na uongozi wa CCM ndio ulioleta amani ya kudumu na wengine hawawezi kuleta amani hiyo kama ilivyoletwa na chama hicho kikubwa.

Alisema kuwa CCM lazima ishinde ili ipate kuendelea kuyalinda Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 ambayo yamemnufaisha kila mtu katika nchi hii na kueleza haja ya kuanza kuandaa mazingira ya ushindi.

Aidha, alisisitiza haja ya kuendelea kuulinda, kuuendeleza na kuudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao hatimae ilipatikana Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar na Tanzania kwa jumla ni sehemu yenye amani na utulivu mkubwa hatua ambayo imefikiwa kutokana na uongozi thabiti wa CCM.

Pia, Dk. Shein kuwa tayari sheria mpya yab udhalilishaji wa kijinsia ameshaisaini hivi karibuni ambayo itafanyiwa kazi na ambao watakapatikana na tuhuma hizo baada ya kusaini sheria hiyo watahukumiwa kwa mujibu wa sheria hiyo ili lazima Zanzibar iendelee kuwa na heshima yake kama ilivyokuwa siku za nyuma.

Aliwahakikishia Mabalozi hao kuwa changamoto ya kufika kwa huduma ya umeme katika jijiji cha Kijangwani Micheweni litapatiwa ufumbuzi pamoja na kujengwa kwa bweni la skuli ya Chwaka Tumbe, na ujenzi wa barabara ya Micheweni-Kiuyu na Kiuyu na Maziwang’ombe pamoja na kuendelea kuwaajiri walimu.

Dk. Shein alisema kuwa tayari kisiwani Pemba kumeshapelekwa walimu 265 na sio walimu wanane ambao wamepelekwa Chokocho kama inavyovumishwa na baadhi ya wanasiasa wa upinzani.

Pia, Dk. Shein alisisitiza kuwa Serikali imo katika juhudi za kupambana na rushwa na kueleza kuwa ndani ya CCM rushwa itaendelea kupigwa vita huku akieleza haja ya viongozi hao kuunga mkono mapambano ya biashara ya dawa za kulevya na kuvitaka vikosi vya ulinzi kuendelea kuchukua hatua.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdalla Juma Mabodi aliwapongeza Mabalozi wa Wilaya ya Micheweni kwa uvumilivu mkubwa walionao hatua ambayo imewapelekea kuendelea kupata mafanikio makubwa katika maeneo yao.

Nao Mabalozi wa Wilaya ya Micheweni Pemba kwa upande wao wamemuhakikishia Makamo Mwenyekiti huyo kuwa wataendelea kumuunga mkono katika kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020. 

Wakizungumza katika risala yao iliyosomwa na Ismail Ali Mabalozi hao waliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein kwa utekelezaji wake wa  Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa kasi kubwa.

Mabalozi hao walieleza kuwa wanaunga mkono utekelezaji wa Ilani hiyo ya Uchaguzi ya CCM sambamba na kuahidi kuendelea kukipigia debe chama chao cha CCM ili kiendelee kushinda chaguzi zijazo kama ilivyo lengo kuu la chama hicho.

Aidha, Mabalozi hao wameeleza kuridhishwa kwao na utendaji kazi wa Rais Dk. Shein kwa upande wa Serikali na kwa upande wa Chama na kutumia fursa hiyo kumpongeza kwa ushidni mkubwa alioupata katika uchaguzi Mkuu wa Chama uliofanyika Dodoma mwishoni mwa mwaka jana.

Walieleza kuwa ushindi alioupata Dk. Shein unadhihirisha wazi kuwa wanachama, wananchi wapenda amani bado wanaimani na uzalendo wake katika kukitumikia Chama Cha Mapinduzi na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza na Mabalozi wa Wilaya ya Chake Chake huko katika ukumbi wa Skuli ya Fidel Castro, Dk. Shein aliwataka Mabalozi wa Wilaya hiyo kusimamia Ilani ya Uchaguzi ya CCM sambamba na kueleza mafanikio makubwa yaliopatikana ndani ya  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye sekta za maendeleo ikiwemo elimu, afya, miundombinu ya barabara, mawasiliano, maji, umeme na nyenginezo.

Aidha, aliongeza kuwa uongozi katika chama cha Mapinduzi ni tofauti na uongozi katika vyama vyengine vya siasa na kueleza kuwa CCM ina historia yake kwani ndio iliyozikomboa Zanzibar na Tanganyika kupitia vyama vya TANU na ASP, hivyo chama hicho kina historia kubwa na ushindi kwa chama hicho ni wa lazima na kuwahakikishia kuwa CCM itashinda kwa kishindo uchaguzi mkuu ujao.

Alieleza kuwa Tanzania imepata mafanikio makubwa na inatambulikana dunia nzima kutokana na mafanikio yaliopatikana.

Dk. Shein aliwasisitiza Mabalozi hao kutekeleza wajibu wao kwa lengo la kukiimarisha chama hicho huku akisisitiza umuhimu wa kujitolea ambao hivi sasa umepungua ikilinganishwa na hapo siku za nyuma

Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdalla Juma Mabodi alieleza kuwa Mabalozi wa Wilaya ya Chake Chake wamefanya na wanaendelea kufanya kazi kubwa katika kuiimarisha CCM ikiwa ni pamoja na kusimamia vyema kazi zao.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba, Yussuf Ali Juma kwa upande wake alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa juhudi zake katika kutekeleza Ilani pamoja na uongozi wake madhibuti katika Serikali anayoiongoza. 

Katika risala ya Mabalozi iliyosomwa na Bi Kiembe Ramadhan Khamis, Mabalozi walitumia fursa hiyo kumpongeza kwa kutekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM kwa kuwapatia wananchi huduma mbali mbali za kijamii zikiwemo  maji safi na salama kwa asilimia kubwa, huduma za afya, umeme, barabara na nyenginezo.

Walieleza kuibuka kwa wimbi la vijana wanaojihusisha na madawa ya kulevya na unyanyasaji wa kijinsia jambo ambalo linavunja mila na silka ya Kizanzibari.

“Sisi kama wazazi tunaungana na serikali yetu katika kupiga vita kwa nguvu zetu zote jambo hili na tunaomba yeyote atakaejihusiaha na vitendo hivi hatua kali zichukuliwe ili kurudisha heshima ya nchi yetu”, ilieleza risala ya Mabalozi hao.

Kwa upande hali ya usalama na utulivu, Mabalozi hao walieleza kuwa katika Wilaya yao wanaendelea vizuri na hakuna tatizo lililojitokeza kwa hivi sasa na wanaendelea kufanya shughuli zao za kijamii kwa pamoja kama vile sherehe na misiba.

No comments