Header Ads

Neema kwa Waathirika wa Mvua Z'bar kusaidiwa kujengewa Nyumba


SERIKALI kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo, ina mpango wa kujenga nyumba za makazi kwa ajili ya wananchi wanaoathirika na mvua zinazonyesha kila mwaka.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Vuga mjini Unguja.

Alisema kwa kuanzia itaanza na ujenzi wa nyumba 50 ili kuwasaidia wananchi ambao huathirika zaidi katika maeneo ambayo yanajaa maji na kuacha maji yapite kwenye njia zake.

Aidha, alisema mvua zinapokuwa kubwa mitaa mengi inaingia maji na wananchi kulazimika kuyahama makazi yao.

“Baada ya kukamilika mpango huu, nyumba zilizoathirika zitabomolewa ili kupisha maji kuendelea kupita katika njia yake ya kawaida kwani imeonekana wananchi wengi wamejenga mabondeni na kwenye njia za maji,” alisema.

Mbali na hayo, alisema mpango mwengine wa serikali ni kujenga nyumba za ghorofa ili kuhakikisha wananchi wanaepuka kujenga nyumba kiholela.

“Kimsingi hatuwezi kumuondosha mtu mahali na tusimpe makaazi,hivyo utaratibu utafanyika na kwa wale walokiuka taratibu za kujenga nyumba, mpango huu hautawahusu  wao watauziwa,” alisema.

Alisema kwa sasa nyumba zaidi ya 1,576 ambazo zimeathirika na mvua serikali kupitia mradi wa ZUSP imechukua hatua kuondosha maji katika maeneo hayo.

Alisema awamu ya pili ya mradi huo ni kuondoa maji katika bwana la Mwanakwerekwe na kuinyanyua barabara hiyo na Kibondemzungu.

No comments