Taasisi za Elimu zaonywa kuwepo kwa Vyuo visivyokidhi vigezo Zanzibar
TAASISI
na Mamlaka zinazohusika na usimamizi wa vyuo vya elimu ya juu na mafunzo ya
ufundi nchini zimetakiwa kuchukua hatua zinazostahiki wanapogundua uwepo wa
taasisi zisizokidhi vigezo.
Akifungua
mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa shirikisho la vyuo vikuu Zanzibar
(ZAHLIFE) kuhusiana na usajili wa taasisi za elimu ya juu, mkuu wa mkoa wa
mjini magharibi mhe; ayoub mohammed Mahmoud amesema kufanya hivyo kutasaidia
kupatikana rasilimali watu yenye tija na kuondoa usumbufu kwa wanafuzi na
wazazi wao.
Amesema
Mamlaka ya mafunzo ya amali Zanzibar, Baraza la taifa la usimamizi wa taasisi
za elimu ya juu (NECTA) na Wizara ya elimu na mafunzo ya amali kwa pamoja
wanapaswa kusimamia upatikanaji wa watu walioelimika na wenye ujuzi
utakaochochea maendeleo ya taifa.
Amesema
katika utafiti uliofanywa na ZAHLIFE imegundulika uwepo wa vyuo ambavyo
vinafanya kazi kinyume na matakwa ya sheria ya uanzishwaji wa vyuo vya elimu ya
juu na mafunzo ya amali jambo linaloleta usumbufu kwa wanafunzi wanaomaliza
katika vyuo hivyo wanapotaka kujiunga katika ngazi nyengine ya elimu.
Mkuu
huyo wa mkoa ambae pia ni mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya ZAHLIFE
alizishauri mamlaka hizo kukaa pamoja na kuviondoa vyuo hivyo katika mfumo wa
elimu nchini ili kuwaokoa wanafunzi wanaosoma na hasara watakayoipata pindi
watakaposhindwa kuendelea na mafunzo yao katika ngazi nyengine.
Aidha
aliupongeza uongozi wa ZAHLIFE kwa kuamua kuandaa mafunzo hayo na kuwataka
kuendelea kufanya kazi kwa mashirikiano na kutoa taarifa kwake na mamlaka
nyengine pindi wanapogundua uwepo wa vyuo au taasisi za elimu ya juu na
mafunzoo ya amali visivyokidhi vigezo.
Nae
Mkuu wa kanda ya Zanzibar wa Baraza la usimamizi wa taasisi za elimu ya juu na
mafunzo ya ufundi Tanzania (NACTE) Halima Mbilinyi amesema taasisi yake imekuwa
ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa taasisi na vyuo vya elimu ya juu ili
kuhakikisha taasisi hizo zinazingatia sheria zilizopo.
Amesema
hadi kufikia mwezi aprili mwaka huu vyuo na taasisi 16 zimeshasajiliwa baada ya
kukidhi vigezo na masharti, vyuo viwili vimefungiwa na vyengine 8 vilifutiwa
usajili baada ya kushindwa kufikia vigezo vinavyohitajika.
Akitoa
shukrani kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Mwenyekiti wa ZAHLIFE
Abdullatif Kadir Mussa aliwataka wanafunzi nchini kufanya utafiti kabla ya
kujiunga na baadhi ya vyuo ili kujiridhisha kama vyuo hivyo vimesajili kozi
wanazotaka kujifunza kwa lengo la kuepuka madhara katika siku za baadae.
Amesema
licha ya kuwepo kwa vyuo vilivyosajiliwa, baadhi yao hutoa kozi ambazo
hazikusajiliwa jambo ambalo ni kosa kisheria na kushauri kurejeshwa kwa
kwa mpango wa kurudia mitihani ili kuongeza sifa za kujiunga na vyuo kwa
wanafunzi ambao hawajatimiza sifa za kujiunga na vyuo vya elimu ya juu.
Mafunzo
hayo ya siku mbili yaliendeshwa na wataalamu mbali mbali kutoka Wizara ya elimu
na mafunzo ya amali Zanzibar, Bodi ya mikopo ya elimu ya juu na Baraza la
usimamizi wa vyuo na taasisi a elimu ya juu Tanzania ambapo pamoja na mambo
mengine washiriki walijifunza namna mpya ya kuomba mikopo inayotolewa na bodi ya
mikopo ya elimu ya juu kwa lengo la kwenda kuwasaidia wanafunzi wengine katika
vyuo vyao.
Post a Comment