'Vitendo hivi Visipodhibitiwa Mapema Tujiandae Kukipoteza Kisiwa hiki'
KUSHAMIRI
kwa vitendo vya ukataji wa miti ovyo vinavyofanywa na baadhi ya wananchi ,
vimeanza kutishia kutoweka kwa kisiwa kidogo cha Njao kilichopo Wilaya ya Wete
Mkoa wa Kaskazini Pemba .
Hali hiyo
inayoafanywa na baadhi ya wananchi katika kisiwa hicho imetokana na
kuwepo na biashara ya magogo, kilimo kisichozingatia hifadhi ya mazingira
pamoja na vitendo vya uchomaji wa mkaa.
Mussa Juma
Mohammed ameiambia REDIO JAMII MICHEWENI kuwa wakulima katika kisiwa
hicho wameanza kupata athari ya kupungua mazao ya chakula na biashara na
hivyo kusababisha njaa na umaskini.
Ameeleza
kwamba iwapo vitendo hivyo havitadhibitiwa, baada aya miaka kumi ijayo, kisiwa
hicho kitakuwa jangwa na wananchi wanaokitegemea watakumbwa na hali ya
umaskini ulikithiri.
“Shughuli za
kibinadamu ambazo zimeshamiri katika kisiwa hichi, zimeanza kusababisha
kupungua hali ya uzalishaji wa chakula pamoja na kukosa sehemu za malisho ya
mifugo’’ alieleza.
Naye Khatib
Kombo Khamis amesema awali ndani ya Kisiwa hicho hakukuwa na tabia ya wafugaji
kufunga mifugo yao, walikuwa wanaiachilia kutokana na kuwepo sehemu kubwa ya
malisho tofauti na sasa ambapo wafugaji wanaifunga kwa hofu ya kuharibu vipando
vya wakulima.
Sheha wa
Shehia hiyo Ali Abdalla amesema kuwa vitendo hivyo vina athari kimazingira na
unachangia maji ya bahari kuvamia maeneo ya kilimo katika kisiwa hicho .
Akizuzngumzia
hatua ambazo uongozi wa shehia umechukua, amesema kuwa ni pamoja na kufanya
mikutano ya mara kwa mara na wananchi na kuwataka washirikiane na Serikali
kuyahifadhi mazingira ya kisiwa hicho.
Mkuu wa
Wilaya ya Wete Abeid Juma Ali ameutaka uongozi wa Shehia hiyo kuimarisha doria
katika kisiwa hicho ili kudhibiti vitendo vya ukataji wa miti pamoja na
uchimbaji wa mawe.
Amesema ili
kudhibiti vitendo hivyo ni vyema uongozi wa shehia kuondoa muhali na
kuhakikisha kwamba rasilimali katika kisiwa hicho zinabaki salama na
zinaendelea kunufaisha jamii ya sasa na baadaye .
“Katika
kufanikisha udhibiti wa vitendo hivyo , hakuna budi kuondoa rushwa muhali ili
kufanya mazingira kurejea kwenye uhalisia wake’’ alisisitiza.
Kisiwa cha
Njao ni moja visiwa vidogo vidogo katika Wilaya ya Wete ambacho umaarufu wake
katika uzalishaji wa chakula umeanza kupungua , na kunahitajika hatua za
makusudi kuweza kurejesha uhalisia wa uoto wake .
Post a Comment