Header Ads

'Wananchi Micheweni jiungeni na Vyama vya Ushirika ili kuweza kujikomboa kimaendeleo'


WANANCHI katika Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba wametakiwa kuendelea kujitokeza kujiunga na vyama mbalimbali vya Ushirika ili kuweza kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.
Daktari dhamana wa Hospitali ya Micheweni, Dok. MBWANA SHO SALIM(katikati), akipokea Msaada wa Vifaa vya usafi kutoka kwa Mkuu  wa Wilaya ya hiyo Salama Mabarouk Khatib (kushoto), vilivyotolewa na wanaushirika Wilayani hapo.
Akizungumza katika shamra shamra za kuelekea kilele cha siku ya Ushirika Duniani, zilizo ambatana na zoezi la usafi katika Hospitali ya Micheweni, Mkuu wa Wilaya ya hiyo Salama Mabarouk Khatib amesema ili jamii iweze kukua kimaendeleo ni budi kuvitumia kikamilifu vyama vya ushirika.
Amesema kujiunga katika vyama vya ushirika hutoa fursa mbalimbali ikiwemo kujifunza mbinu bora za ujasiriamali ikiwa ni pamoja na kupata nafasi kubwa ya kujiwekea akiba ya kipato chao.

Awali akizungumza na wanaushirika waliojitokeza katika zoezi hilo, Afisa Ushirika Wilaya hiyo, Rashid Khatib Hamad, amesema kuwa zoezi hilo ni mwendelezo wa utekelezaji wa kanuni za ushirika ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Aidha Rashid amewataka wanaushirika na wananchi kujitokeza katika maadhimisho ya kilele cha sherehe hizo yatakayofanyika Julai 06 mwaka huu, katika viwanja vya Tibirinzi SACCOS Wilaya ya Chake chake.

Daktari dhamana wa Hospitali hiyo, Dok. MBWANA SHO SALIM, amewapongeza wanaushirika hao kwa maamuzi yao ya kuadhimisha sherehe hizo kwa kushiriki zoezi la usafi katika Hospitali hiyo.
Daktari dhamana wa Hospitali ya Micheweni, Dok. MBWANA SHO SALIM(katikati), akitoa maelekezo kwa Mkuu  wa Wilaya ya hiyo Salama Mabarouk Khatib, (kushoto) kuhusu Utendaji kazi wa Jengo la Upasuaji linalotarajia kuanza kutoa huduma hivi karibuni. (PICHA NA GASPARY CHARLES- MICHEWENI REDIO)
Maadhimisho ya sherehe hizo mwaka huu, yanabebwa na ujumbe wa ‘matumizi endelevu na uzalishaji wa bidhaa na huduma unatoa fursa kwa vyama vya ushirika kuonesha ni kwajinsi gani vinaendesha biashara kwa ufanisi vikiwa vinazingatia utunzaji wa mazingira na rasilimali zinazopatikana.’



No comments