Tani Mbili za Bidhaa Feki zateketezwa Pemba, Wizara yatoa Onyo kali kwa Wafanya Biashara
JUMLA ya Tani mbili
za bidhaa zilizomaliza muda wa matumizi zenye thamani ya Shilingi Milioni Tano,
zimeteketezwa na Kitengo cha kusimamia mwenendo wa Biashara na kumlinda mlaji katika
Eneo la Mikindani, Wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba.
Akizungumza wakati
wa zoezi hilo, Afisa Biashara, Wizara ya Biashara na Viwanda Pemba, Bi Mgeni
Khatib Yahya, amesema huo ni mwendelezo wa juhudi za Wizara kupitia kitengo
hicho wa kuhakikisha wanadhibiti uuzaji wa bidhaa feki madukani.
Afisa Biashara, Wizara ya Biashara na Viwanda
Pemba, Bi Mgeni Khatib Yahya, akionesha namna ambavyo Wafanya Biashara wanazifuta namba za kuisha muda wa matumizi na kubandika feki.
|
Afisa huyo amesema
kuwa bidhaa hizo zilizoteketezwa zilikusanywa kutoka kwenye maduka ya maeneo
tofauti ya kisiwa cha Pemba baada ya kufanyika msako wa kubaini uwepo wa bidhaa
hizo madukani.
Gari lililobeba Bidhaa hizo likizimwaga katika eneo la kutupia taka la Mikindani, Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba tayari kwa kuteketezwa. |
Bi Mgeni amebainisha
kwamba kumekuwepo na tabia za baadhi ya wafanya biashara kufuta muda uliowekwa wa
kuisha matumizi kwenye bidhaa na kubandika chapa nyingine feki ili ziendelee kuwa
sokoni.
“baada ya kufanya
msako kwenye maduka, tumebaini kuwa kuna wafanyabishara wanafuta namba za muda
wa kuisha matumizi kwenye bidhaa na kubandika namba nyingine za bandia.”
Baadhi ya Bidhaa zilizoteketezwa |
Katika hatua
nyingine afisa huyo amewataka wananchi kuwa makini wanaponunua bidhaa ili
kuepuka kununua bidhaa zisizokidhi viwango ambazo zinaweza kuhatarisha maisha
yao.
“Nitoe wito kwa
jamii, wanapohitaji kununua bidhaa yoyote madukani wahakikishe wanaziangalia
kwa umakini ili kuondokana na kununua bidhaa zilizomaliza muda wake wa matumizi
ambazo ni hatari kwa afya zao.”
Ameongeza kwamba
Wizara, kupitia idara ya Biashara itaendelea kuwachukulia hatua wafanyabiashara
wanaokiuka sheria za biashara kwa kuuza bidhaa zisizositahili.
Baadhi ya Maafisa kutoka Kitengo cha kusimamia mwenendo wa Biashara na kumlinda mlaji, idara ya Biashara Zanzibar wakishiriki zoezi la uteketezaji wa Bidhaa hizo. |
Baadhi ya wananchi
wamepongeza hatua hiyo ya Wizara ya Biashara kufanya ukaguzi wa bidhaa feki
kwani wao ndio waathirika wakubwa wa suala hilo.
Akizungumza na
mwandishi wa habari hizi mwananchi, Juma Omar Alawi amesema maamuzi ya kitengo
cha kusimamia mwenendo wa biashara na kumulinda mlaji ya kuteketeza bidhaa hizo
yamekuja muda mwafaka kutokana na kuongezeka kwa bidhaa hizo madukani.
“Naipongeza sana Serikali
kupitia Wizara ya biashara na Viwanda kwa kutekeleza zoezi hilo kwa vitendo
kwani bidhaa hizi zinatuathiri zaidi sisi wananchi wa kawaida.” Alisema Alawi.
Zoezi la ukaguzi na
uteketezaji wa bidhaa feki kisiwani Pemba ni mwendelezo wa juhudi za Wizara ya
Biashara na Viwanda wa kusimamia na kutekeleza azima ya serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar ya kuhakikisha inamlinda mtumiaji dhidi ya matumizi ya bidhaa feki.
MATUKIO ZAIDI
(PICHA ZOTE NA GASPARY CHARLES-PEMBA)
Post a Comment