CYD: Wazazi tuwafunzeni maadili mema Vijana wetu kulinda Amani ya Nchi
JAMII kisiwani
Pemba imetakiwa kukaa karibu na vijana ili kuwaelimisha mbinu za kueneza amani
kwa kuepuka kujiingiza katika makundi maovu ya kiharifu yanayoweza kuleta
athari katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Rai hiyo imetolewa
na Mratibu wa Mradi wa kuwaelimisha vijana juu ya umuhimu wa amani katika jamii
kutoka taasisi ya Majadiliano kwa Vijana, (Center for Youth Dialogue –CYD),
Moza Kawambwa Nzole, wakati akizungumza na vijana kisiwani hapa.
Amesema kuwa ili
kijana aweze kukua katika misingi adilifu ndani ya familia, wazazi wanatakiwa
kukaa karibu na vijana ili kuwawezesha kujiepusha na kujiingiza katika makundi
maovu.
Mratibu wa Mradi kutoka taasisi ya Majadiliano kwa Vijana, (Center for Youth Dialogue –CYD), Moza Kawambwa Nzole, akiwasilisha mada, katika Viwanja vya Polisi Madungu, Chake chake Pemba. |
“Malezi ya watoto
yanahusisha baba na mama, kwahiyo wakati mwingine wazazi wanaweza kuwa chanzo
cha vijana kupotoka pale malezi ya pamoja yanapokosekana katika familia,”
alisema Moza.
Akizungumza katika
Mafunzo hayo, Mratibu wa Taasisi ya Jukwaa la Vijana Zanzibar –ZYF-, Almas
Mohamed, alisema ni jukumu la kila mwanajamii kuhakikisha anaeneza amani ili
kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuleta vurugu.
Mratibu wa Taasisi ya Jukwaa la Vijana Zanzibar, (Zanzibar Youth Forum)–ZYF-, Almas Mohamed, akizungumza na washiriki wa Mafunzo yaliyofanyika katika Uwanja wa Polisi Madungu, Chake chake Pemba. |
“Kuna njia
mbalimbali sahihi za kudai haki ambazo tukizifuata basi tunaweza kumaliza
tofauti zetu na kuendelea kuishi kwa amani na upendo katika jamii zetu,”
alisema Almas.
Mmoja wa washiriki wa Mafunzo akichangia Mada. |
Kwa upande wake
Hemed Khamis Khatibu mkaazi wa Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, amesema umefika
wakati ambapo wazazi wanatakiwa kulea familia zao kulingana na tamaduni
walizokuwa nazo.
“Silka
tulizotokanazo ni tofauti na sasa, saizi mtoto anaweza kukuta baba unamkoba na
chakula unaleta kwao lakini mtoto yule anakuangalia na pengine mzazi hasemi
chochote,” alisema.
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo hayo wakifuatilia mafunzo. |
Nae Bi Rabia Omar
Saleh, alisema kuwa wazazi wana wajibu wa kutambua marafiki wa watoto wao ikiwa
ni pamoja na kuwafahamisha aina ya marafiki wanaotakiwa kuambatana nao ili
wasiweze kujiingiza katika makundi maovu.
“Mtoto ni kama
Kitabu, hivyo unavyomtunza ndivyo anavyokua mwema katika jamii, hivyo wazazi
tujitahidi kuwa karibu na watoto wetu kila wakati,” alisema Rabia.
Mradi huo unatekelezwa
kwa kufadhiliwa na Shirika la The Foundation for Civil Society.
Washiriki wa Mafunzo katika Picha ya pamoja tayari kwa mchezo wa kirafiki baada ya mafunzo kama ishara ya upendo. |
PICHA ZOTE NA: GASPARY CHARLES - Micheweni Radio, Pemba. |
Post a Comment