Header Ads

TAMWA: Wanawake Pemba washirikishwe kwenye uongozi na Siasa


ASASI za kiraia Kisiwani Pemba zimetakiwa kuweka mikakati maalum katika shughuli zao ili kuwezesha suala la ushirikishwaji wa Wanawake katika masuala ya uogozi na siasa kufanikiwa katika Nyanja mbalimbali.

Rai hiyo imetolewa na Meneja utetezi kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake - TAMWA- Zanzibar, Haura Mohamed Shamte, katika kikao na viongozi wa Asasi za kiraia Pemba chenye lengo la kuhamasisha Mwanamke kushiriki kikamilifu katika masuala ya uongozi na siasa.

Amesema mwamko wa jamii ya wanawake Kisiwani Pemba kujiingiza katika masuala ya uongozi bado upo nyuma hivyo taasisi za kiraia kupitia shighuli zake wanao wajibu wa kutoa uhamasishaji kwa wanawake kuanzia ndani ya taasisi zao na nje.

Thuwein Issa Thuwein, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Elimu, Mafunzo, ushauri na Utafiri Zanzibar- JEMUUZA- amesema umefika wakati wanawake kuungana pamoja ili kutafuta namna ya kuweza kujitokeza kugombania nafasi mbalimbali za kisiasa na kushinda katika chaguzi.

Nae Bakia Juma Khamis, mmoja wa wanawake waliothubutu kugombea nafasi ya Ubunge, amesema changamoto kuu inayowarudisha nyuma wanawake kisiasa na kushindwa kufika mbali zaidi ni Rushwa iliyotawala katika jamii.

Amesema wanawake wanapogombania nafasi wengi wao hushindwa kwenye uchaguzi kutokana na hawana uwezo wa kutoa rushwa.

Kikao hicho cha viongozi wa Asasi za kiraia Pemba ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa uhamasishaji Wanawake kuingia na kuwania nafasi mbalimbbali za uongozi unaotekelezwa  na chama cha waandishi wa habari wanawake- TAMWA - kwa kushirikiana na Klabu ya waandishi wa habari Pemba -PPC- .

#SautiYaMicheweni, #Micheweni #Pemba #Zanzibar



No comments