DC Wete: Mradi wa VIUNGO umewekeza nguvu kwenye Ujenzi wa Uchumi Endelevu kwa Wakulima Zanzibar
Mkuu wa Wilaya ya Wete, Dkt. Hamad Omar Bakar. |
MKUU wa Wilaya ya Wete, Dkt. Hamad Omar Bakar amesema mbinu za utekelezaji mradi wa VIUNGO Zanzibar kuwaendeleza wakulima unajenga misingi imara itakayowezesha uchumi endelevu kwa wakulima Zanzibar kupitia kilimo hicho.
Amesema
kuweka mazingira ya uendelevu wa uzalishaji hata baada ya mradi kumaliza muda
wake ni hatua muhimu ambayo miradi mingi inashindwa kutekeleza na kupelekea
kukosa matokeo chanya kwa walengwa.
Mkuu
huyo wa wilaya ametoa kauli hiyo katika kikao cha kamati tendaji ya Wilaya za
Micheweni na Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba na maafisa wa mradi huo cha kujadili
changamoto zinazowakabili wakulima wa mazao ya Viungo, mboga na matunda katika
wilaya hiyo ili kuzitafutia ufumbuzi kwenye ngazi husika.
Dkt.
Hamad ambaye pia ni kaimu mkuu wa Wilaya ya Micheweni amepongeza watekelezaji
wa mradi huo People's Development Forum (PDF), Chama Cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) na Community Forests Pemba
unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia mpango wa AGRI-CONNECT Tanzania
kwa hatua waliyoipiga kuwaendeleza wakulima wa mazao hayo ili kuwaondoa katika
wimbi la umasikini.
Ameeleza
ikiwa miradi yote inayotekelezwa kwenye jamii itakuwa na mbinu bora za
kuwezesha uendelevu wa shughuli itasaidia kukuza ustawi wa Jamii na kuondoa
changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta mbalimbali.
"Niwapongeze
sana katika hili na niwaombe tuendelee kuwawezesha wananchi ili kujenga uchumi
endelevu ambao utaongeza ajira na kutatua changamoto za kijamii kama vile
afya," alieleza.
Katika
hatua nyingine alieleza kuwa uwepo wa fursa ya mradi huo kwa wananchi Zanzibar
unaisaidia serikali kufikia malengo yake ya kukuza uchumi wa wananchi na
kuongeza ajira.
Alieleza,
"tunafahamu shughuli za kilimo ni sehemu ya ajira kwa wananchi, hivyo
nikupongezeni sana kwani kupitia mradi huu wananchi wengi hasa vijana wanapata
ajira na kujiendesha kiuchumi jambo ambalo linairahisishia serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kufikia lengo la kuongeza ajira kwa wananchi wake kupitia
kilimo."
Said
Hemed Shaame, afisa kilimo wilaya alisema changamoto kubwa ambayo bado
inawakabili wakulima ni kukosa miundombinu rafiki inayoweza kuwahakikishia
uendelevu wa uzalishaji wa mazao hayo kwa wingi ili kukidhi mahitaji ya soko.
Nae
Bizume Haji Zume, afisa usitawi wa jamii wilaya hiyo alieleza bado kuna kikwazo
cha ukosefu wa taaluma ya uhifadhi na na uchakataji wa mazao kwa wazalishaji na
kushauri kuongezwa nguvu katika utoaji wa taaluma hiyo waweze kuzalisha kwa
kuzingatia viwango na ubora unaohitajika sokoni.
Mapema
afisa uwezeshaji kiuchumi wa mradi huo, Nairat Abdalla alisema mradi unatumia
kamati za Wilaya kama chombo na jukwaa muhimu la kufuatilia changamoto zilizopo
kwa wakulima na kuzitafutia utatuzi wa pamoja kwa ngazi husika.
Alieleza
kupitia kamati hizo ambazo zinajumuisha maafisa na wataalam kutoka idara
mbalimbali ngazi ya wilaya, zinawawezesha wakulima kuwasilisha changamoto zao
na kuwezesha ufikiaji wa ongezeko la mnyororo wa thamani kwenye mazao.
Kikao
hicho cha kamati tendaji ya mradi ngazi ya wilaya kimejumuisha maafisa kutoka
idara mbalimbali za wilaya wakiongozwa na Katibu tawala, afisa usitawi, afisa
Mipango, afisa kilimo, Mwenyekiti wa masheha, afisa biashara, afisa ushirika, afisa
maji pamoja na afisa sera wilaya.
Mradi
wa Viungo unatekelezwa kwa lengo la kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao ya
mboga, matunda na Viungo kwa kuongeza thamani na uzalishaji mwingi wa mazao
bora kwa lengo la kupata masoko na kukuza uchumi jumuishi Zanzibar.
Post a Comment