KIJALUBA chawafundisha walimu mbinu usimamizi vikundi vya wenye Ulemavu
JUMLA ya Viongozi 86, Unguja 40 na Pemba 46 wa vikundi vya kuweka na kukopa kupitia mradi wa KIJALUBA iSAVE wamepatiwa mafunzo maalum ya usimamizi wa uchukuaji mikopo na sheria za vikundi ili kuimarisha ustawi wa uchumi wa wanachama kwenye vikundi vya watu wenye ulemavu.
Mafunzo hayo ambayo ni
utekelezaji mradi wa KIJALUBA iSAVE ZANZIBAR unaotekelezwa kwa mashirikiano ya
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania,Zanzibar (TAMWA-ZNZ), na
Shirikisho la Jumuiya za Watu wenye
Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA) kupitia ufadhili wa Jumuiya ya watu wenye ulemavu
ya Norway (NAD) yamekuja kufuatia zoezi la uundaji wa vikundi ambavyo
vinawashirikisha watu wenye ulemavu kukamilika na kuanza kutoa mikopo kwa
wanachama.
Katika mafunzo hayo viongozi wamefundishwa
pia misingi bora ya kuweka kumbukumbu katika vikundi vyao ili kuepusha migogoro
inayotokana na upotevu wa taarifa muhimu za wanachama kwenye kikundi.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo
kutoka Pemba Bakari Haji alisema mafunzo hayo yatakwenda kusaidia wahusika
kutekeleza majukumu yao na kuongeza kasi ya ufikiaji mafanikio ya watu wenye
ulemavu katika vikundi vyao na kuondokana na utegemezi kiuchumi.
Nae mwezeshaji kutoka Unguja
Muhidini Ramadhan aliwashauri viongozi wa vikundi kusimamia na kuyatumia
mafunzo hayo waliopewa ili waweze kuendesha vikundi kwa mujibu wa muongozo wa
mradi ili kukuza uchumi jumuishi kwa watu wenye ulemavu katika jamii.
Wakizungumza wakati wa
mafunzo hayo walimu wa vikundi wamesema mafunzo yatawasaidia kutekeleza
majukumu yao na kuvisimamia vikundi hivyo kwa kutoa mwongozo wa uendeshaji
vikundi hasa kwa wenye ulemavu ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Mohamed Ali, msimamizi na
mwalimu wa vikundi Unguja alishukuru kutolewa kwa mafunzo hayo kwani licha ya
kuwa na uzoefu katika usimamizi wa vikundi lakini ameongeza ujuzi zaidi wa
namna ya kusimamia vikundi vya watu wenye ulemavu kutokana na kuhitaji
usimamizi maalum.
Alieleza watu wenye ulemavu
wanahitaji kupatiwa mbinu na usimamizi rafiki ili kuhakikisha rasilimali za
vikundi hazipotei na badala yake kuleta manufaa kwao kujikomboa kiuchumi jambo
ambalo litatekelezwa kupitia ujuzi walioupata.
Nao viongozi wa vikundi hivyo
wameshukuru kupatiwa mafunzo hayo na kuahidi kwenda kuyatumia vyema na
kuyafikisha kwa wanakikundi wenzao ili waweze kiuendesha vikundi kwa mujibu wa
muongozo na hivyo kujikwamua kiuchumi.
Mradi wa KIJALUBA ni mradi
jumuishi unaolenga kuwakomboa kiuchumi watu wenye ulemavu ambao unatekelezwa
kwa majaribio ndani ya wilaya mbili za Zanzibar, kwa Unguja wilaya ya Kusini na
wilaya ya Chake chake Pemba ambapo tayari umeunda jumla ya vikundi 43.
Post a Comment