Header Ads

Vijana watakiwa kutumia mitandao kupata fursa za ustawi wao kujiepusha Udhalilishaji



MKURUGENZI wa jinsia, wanawake na watoto kutoka Wizara ya Maendeleo, Jinsia, Wazee na watoto Zanzibar, Siti Abasi amewataka vijana kuitumia vizuri mitandao ya kijamii ili kuepukana na vitendo vya udhalilishaji mitandaoni.

Aliyasema hayo katika mkutano wa wadau Zanzibar kujadili ripoti ya masuala mbalibali ya kitaifa yanayohusu usitawi wa vijana, nafasi ya wanawake katika vyombo vya maamuzi, rushwa na uwajibikaji katika taifa ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Shirika la Foundation For Civil Society (FCS)

Alisema mitandao ya kijamii imekua ikitumiwa vibaya hivyo ni vyema kuitumia vizuri mitandao hiyo.

Alibainisha kutokana na matumizi mabaya ya mitandao hiyo, inapelekea kuwepo kwa ongezeko la rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kijinsia unaotokana na vijana kujirushwa kwenye mitandao huyo.

“Rushwa ya ngono ni kubwa na kuna kesi za vijana na watoto wa kike wakijirusha wakiwa watupu kupitia mitandao ya kijamii,” alieleza Mkurugenzi huyo.

Aidha aliongeza, "mitandao imekuja kutumika vibaya na sio kibiashara kama ambavyo vijana wetu wanazifanya na kama wangalitumia vizuri vijana wengi wangekuwa na ajira zao binafsi.”

Mkurugenzi Siti alisema Wanawake wengi wamejiajiri lakini changamoto kubwa hawajui kutumia mitandao kutangaza biashara zao.

Akizungumza katika mkutano huo Almasi Muhamed kutoka Zanzibar Youth Forum, alisema taarifa za upatikanaji wa fursa Kwa vijana zinawafikia kwa muda usio sahihi.

Alisema vijana wanatumia vibaya mitandao badala ya kuitumia kwa shughuli zinazowapatia tija lakini wanatumia kwa kuangalia mambo ambayo si muhimu kwao.

Aidha alisema mifumo ya elimu imeshindwa kuwasaidia vijana na wengi wao wanasoma Kwa ajili ya kufaulu masomo yao jambo ambalo haijengi kumuandaa kijana kiajira na inahitaji marekebisho.

“Mifumo ya elimu bado imeshindwa kuwasaidia vijana kujiimarisha kiujuzi na haimuandai kijana kuwa na uwezo wa kujiajiri. Wengi wanasoma kwa ajili ya kufaulu mitihani ya masomo yao jambo ambalo kunahitajika marekebisho kwenye mifumo ya elimu yetu.” Alieleza Almas.

Mapema Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa alisema imefika wakati Serikali iwatambue wafanyakazi wa majumbani kwa kutambua mchago wa kazi zao na kipato chao kitambulike.

Aidha Dk Mzuri, alisema “bado kuna asilimia ndogo ya adhabu ambazo zinatolewa katika kesi za udhalilishaji ikilinganishwa na nchi zingine ikiwemo Unganda ambayo hutoa adhabu kubwa kwa wadhalilishaji.”

Mkutano huo wa wadau ulioandaliwa na TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Foundation For Civil Society umewashirikisha wadau kutoka taasisi na asasi mbalimbali za kiraia kujadili mikakati  inayohusu ustawi wa vijana, nafasi ya wanawake katika vyombo vya maamuzi, rushwa na uwajibikaji katika taifa.

No comments